Ukame wayaweka maisha ya mtoto wa kike hatarini, Kenya
15 Februari 2023Unapowasili kwenye eneo la Kitengela, vumbi na upepo mkali ndio unaokukaribisha.Mvua hazijanyesha kwa muda mrefu na ijapokuwa msimu wa masika unasubiriwa hali ni mbaya. Nyumbani kwa Mama Joyce Kampus ni kutupu.Sehemu ya kuhifadhia mifugo iko wazi kwani wamesafirishwa hadi maeneo ya mbali kusaka malisho.
Jinsi ya kuulinda udongo dhidi ya ukame
Kwa mujibu wa afisi ya Umoja wa mataifa ya uratibu wa misaada,msimu ujao wa mvua wa mwezi Machi hadi Mei huenda ukafeli kwa mara ya sita mfululizo.Hali hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa kuvuruga mazingira na uhaba wa chakula katika eneo la pembe ya Afrika.
Njaa na ukame vimewasukuma baadhi ya wazazi kuwaoza mabinti zao mapema kama njia ya kupata hela za kukidhi mahitaji ya kila siku.Teresia Salonik alikuwa anafuga wanyama na kutunga shanga lakini sasa anashindwa kwani biashara ya maziwa imekufa kwasababu ya ukame
Watu zaidi wanahitaji chakula katika eneo la Pembe ya Afrika
Eneo la Pembe ya Afrika linakabiliana na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika muda wa miaka 40.Takwimu rasmi zinaashiria kuwa watu milioni 36 katika mataifa ya Ethiopia, Kenya na Somalia wanahitaji chakula.
UN: Watu milioni 22 wakabiliwa na njaa pembe ya Afrika
Ripoti mpya ya afisi ya bajeti ya bunge inabainisha kuwa 9% pekee ya ardhi ya Kenya inayoweza kustahimili kilimo ndiyo iliyofanyiwa kazi.Kwa upande wake, Rais William Ruto ameahidi kuiongeza kasi ya kuwashirikisha wadau wa sekta ya binafsi kuchimba mabwawa ili kufanikisha kilimo cha kumwagilia ili sehemu hiyo ifikie ekari milioni 3.
Tathmini ya afya ya uzazi ya mwaka 2022 imebaini kuwa ukeketaji umepungua kutoka 21% hadi 15% Hata hivyo ndoa za utotoni za lazima zinarejesha nyuma juhudi za kupambana na kadhia hiyo, linatahadharisha shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.
Thelma Mwadzaya/DW, Nairobi.