Ukiukaji wa haki za binadamu nchini Iran wachunguzwa
15 Februari 2010Matangazo
Katika kikao cha hii leo mjini Geneva Uswisi,wajumbe wa Uingereza, Ufaransa na Marekani wameeleza wasiwasi wao kuhusu ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaotokea nchini Iraq tangu uchaguzi wa mwezi wa Juni mwaka jana. Afisa mwandamizi katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani,Michael Posner anaeshughulikia masuala ya demokrasia na haki za binadamu amelaani vitendo vya kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa dini nchini Iran. Yeye ametoa mwito kwa Iran ikomeshe moja kwa moja vitendo vya mateso katika jela na vituo vya polisi. Nae Balozi wa Ufaransa Jean Baptiste Mattei amesema, hali ya haki za binadamu imezidi kuwa mbaya nchini Iran tangu miezi minane iliyopita. Amesema,serikali inatumia nduvu dhidi ya umma unaodai haki zao kwa amani. Wakati huo huo, Marekani na Uingereza zimeitaka Iran iwaruhusu nchini humo wachunguzi wa Umoja wa Mataifa na wataalamu wengine wa masuala ya haki za binadamu,walionyimwa ruhusa tangu mwaka 2005. Balozi wa Uingereza, Peter Gooderham amesema, ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaendelea nchini Iran, licha ya Teheran kujiwajibisha kuheshimu uhuru wa kimsingi. Lakini Balozi wa Iran, Mohammad Javad Larijani alie pia Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Iran, akiungwa mkono na Cuba na Venezuela ameitetea nchi yake. Amesema Iran inatekeleza kikamilifu wajibu wake wa kimataifa kuhifadhi haki za binadamu na kuongezea kuwa tuhuma dhidi ya Iran ni jitahada za Marekani na nchi zingine za magharibi, kuitia vishindo Jamhuri hiyo ya Kiislamu, zikihofia kuwa Iran ina mpango wa kutenegeneza silaha za nyuklia. Mara kwa mara,suala la haki za binadamu hutumiwa na nchi za magharibi kama chombo cha kuendeleza maslahi yao ya kisiasa. Kauli hiyo imetolewa siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton kutamka mjini Doha,Qatar kuwa vitendo vya uchokozi vya Iran vinaifanya jumuiya ya kimataifa kutokuwa na chaguo jingine ila kuichukulia hatua kali zaidi. Lakini mwanaharakati wa Iran, Shirin Ebadi alietunukiwa Zawadi ya Amani ya Nobel amehimiza kuiwekea Iran vikwazo vya kisiasa. Yeye ameonya kuwa vikwazo zaidi vya kiuchumi vitawaathiri zaidi wananchi. Mwandishi: Martin,Prema/RTRE Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed
Matangazo