1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukiukwaji wa sheria walemaza Utawala bora Afrika

Admin.WagnerD3 Oktoba 2016

Nchi za Mauritius, Botswana,na Cape Verde, zimechukua nafasi tatu bora katika utawala bora zikifuatiwa na Ushelisheli na Namibia huku Afrika kusini ikiorodheshwa nambari sita.

Mo-Ibrahim-Index für Regierungsführung in Afrika, 29.09.2014 in London
Picha: Barefoot Live

Utawala bora  barani Afrika umeimarika kidogo sana katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita, huku kudorora kwa usalama na kutofuata sheria kukirudisha nyuma hatua zilizopigwa katika nyanja nyinginezo kama za haki za kibinadamu na uchumi. Ripoti hiyo ya utafiti ambayo imezinduliwa na wakfu wa Mo Ibrahim kuhusu utawala bora  wa Afrika inatathmini Afrika katika vigezo vinne vikuu.

Utafiti wa Wakfu wa Mo Ibrahim umeonesha kwamba nchi za Mauritius, Botswana,na  Cape Verde,zimechukua nafasi tatu bora katika utawala bora zikifuatiwa na  Ushelisheli na Namibia huku Afrika kusini ikiorodheshwa nambari sita. Kwa ujumla utafiti huo wa Faharasa umeonesha kwamba bara hilo la Afrika limejiongezea pointi moja tu ikilinganishwa na utafiti uliofanywa mwaka 2006 hiyo ikiwa ni miaka kumi iliyopita. Utafiti huo unaonesha kuwa katika kila nchi kumi, tatu zimeshuka daraja, huku mataifa yenye uwezo mkuu kiuchumi mathalan Afrika kusini na Ghana yakipungukiwa zaidi.

Rais wa Mauritius Ameenah Gurib-Fakim Picha: DW/N. Ackbarally

Utafiti huo ambao ndio wa kina zaidi barani Afrika unatathmini nchi 54 za Afrika, katika misingi ya usalama, haki za binadamu, udhibiti wa uchumi, sheria kuhusu haki, uchaguzi ulio wazi, masuala ya ufisadi, miundo msingi, umaskini, afya na elimu.

Utafiti huo unaonyesha kuwa katika kila nchi kumi, tatu zimeshuka daraja, huku mataifa yenye uwezo mkuu kiuchumi mathalan Afrika kusini na Ghana yakipungukiwa zaidi.

Kwenye ripoti ya utafiti huo unaofanywa na wakfu wake kwa lengo la kukuza utawala bora na uimarishaji wa uchumi barani Afrika, Mfanyibiashara Mo Ibrahim amesema "dhana iliopo hivi sasa  ni jinsi ya kukabiliana na athari za bei za bidhaa na changamoto dhidi ya demokrasia. Lakini hayo si masuala yanayohitaji kupewa kipaumbele. Vipengele vinne vikuu vinavyokuza usalama na utawala wa kisheria vimedorora. hii inalirudisha  nyuma bara la Afrika na inasalia kuwa changamoto kuu kwa mustakabali wake".

Afrika Kusini imepata upungufu mkubwa zaidi, hali ambayo watafiti wametaja kuwa ni hali ya kutia khofu. Licha ya kuwa nchi iliyoendelea kiviwanda barani Afrika, Afrika Kusini imekumbwa na changamoto za kiuchumi, uhaba wa nishati, ukosefu wa ajira, huku raia wakitamaushwa na uongozi wa rais Jacob Zuma na chama chake cha ANC.

Jengo lililoshambuliwa SomaliaPicha: Reuters/F. Omar

Kitengo ambacho Afrika ilipiga hatua bora ni katika matumizi ya teknolojia na muundo wa kidijitali. Miongoni mwa waafrika watano, mmoja anayo simu yenye uwezo wa kuingia kwenye mtandao. Ibrahim anasema watu kuweza kutumia teknolojia ni hatua nzuri zaidi.

Kadhalika Afrika limeimarika katika kitengo cha kisiasa na haki za binadamu. Kitengo hiki kinatathminiwa kwa msingi wa jinsi serikali inavyowaruhusu watu kushiriki kwenye shughuli za kisiasa, na jinsi mashirika yasiyo ya kiserikali yanaruhusiwa kutekeleza majukumu yao bila ya woga au unyanyasaji. Ivory Coast ilitajwa kunawiri katika kufanya uchaguzi uliotizamwa kuwa huru na haki.

Somalia ilishika mkia kwenye utafiti huo. Mataifa mengine ya mwisho ni Sudan, Jamhuri ya Afrika ya kati na Libya. Wakfu wa Mo Ibrahim ulizinduliwa mwaka 2006.

Mwandishi: John Juma/RTRE/

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW