1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukoaji au uhalifu? Wafanyakazi wa misaada washtakiwa Ugiriki

15 Januari 2026

Wafanyakazi 24 wa mashirika ya kutoa misaada wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20 gerezani, ikiwa watakutwa na hatia ya kuratibu wahamiaji kuingia Ugiriki kinyume cha sheria.

Mytilene, Ugiriki 2016 | Wakimbizi wa Syria wakiwa Lesbos
Boti iliyokuwa na wakimbizi wa Syria katika Bahari ya Aegean March 2016 Picha: Guillaume Pinon/NurPhoto/picture alliance

Kesi hiyo inayoanza kusikilizwa tena Januari 15, huko Mytilene, mji mkuu wa Kisiwa cha Lesbos imeelezwa kuwa ''kubwa zaidi iliyoonyesha mshikamano wa kuzifanya huduma za uokozi kuwa uhalifu barani Ulaya.'' 

Pieter Wittenberg, raia wa Uholanzi, ni mmoja kati ya watu 24 wanaoshitakiwa kwa kuwasaidia wakimbizi waliokuwa wanavuka bahari kutoka Uturuki kuelekea Ugiriki. Wittenberg ameiambia DW kuwa hatarajii chochote, lakini amejiandaa kwa lolote.

Kesi hii inajulikana kama ''kesi ya Mardini'' kutokana na mmoja wa washtakiwa ambaye ni raia wa Syria, Sarah Mardini. Sarah ni mwanaharakati na muogeleaji mahiri.

Lakini kesi hii ni zaidi ya matendo waliyoyafanya wafanyakazi hao 24 wa mashirika ya kutoa misaada. Kesi hiyo inayotarajiwa kukamilika ndani ya siku chache zijazo, imekuwa mtihani wa jinsi nchi wanachama za Umoja wa Ulaya zinavyoweza kufikia hatua ya kuwashtaki wale wanaohusika katika kazi za kutoa misaada ya kibinaadamu katika mipaka yao.

Sarah Mardini ni nani?

Mnamo mwaka 2015, Sarah Mardini alikimbia Syria akiwa na mdogo wake Yusra. Wawili hao walivuka Bahari ya Aegean kwa kutumia boti kutoka Uturuki kwenda Lesbos.

Wakati boti yao iliyokuwa imejaa watu kupita kiasi ilipoanza kuzama, wasichana hao wawili waliokuwa na umri wa miaka 19 na 17 wakati huo, waliruka ndani ya maji na kuogoelea kwa muda wa saa tatu hadi katika pwani ya Ugiriki, wakiivuta boti nyuma yao.

Kwa kufanya hivyo, waliyaokoa maisha ya abiria wengine. Ndugu hao baadae waliendelea na safari yao hadi Ujerumani, kwa kupitia kile kinachojulikana kama ''njia ya Balkan'', ambako waliomba kupewa hifadhi. Yusra Mardini alishiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Rio ya mwaka 2016, kama sehemu ya Timu ya Olimpiki ya Wakimbizi.

Sarah Mardini anashtakiwa kwa makosa kadhaa pamoja na wafanyakazi wengine 23 wa kutoa misaadaPicha: Jemal Countness/Getty Images

Hadithi yao ya kusisimua na kutia moyo iliuvutia ulimengu na hatimaye maisha yao yakaigizwa katika filamu ya Netflix ya ''The Swimmers''. Aidha, makala kadhaa katika majarida maarufu ya mitindo yaliwaonyesha Yusra na Sarah kama mipano mipya ya kuigwa.

Mwaka 2016, Sarah Mardini alirejea Lesbos kufanya kazi katika shirika lisilokuwa la kiserikali la Kituo cha Kimataifa cha Huduma za Dharura, ERCI, kuwasaidia wakimbizi wengine. Miaka miwili baadae, alikamatwa na kushtakiwa kwa makosa kadhaa ya uhalifu.

Wafanyakazi watano kati ya 24 wa mashirika ya kutoa misaada walioshtakiwa, akiwemo Sarah Mardini, waliwekwa kizuizini kwa miezi mitatu kabla kesi yao haijaanza kusikilizwa. Mashtaka dhidi ya Mardini na washtakiwa wengine ni pamoja na ujasusi, kuisaidia mitandao ya wafanyabiashara za magendo, kuwa wanachama wa kundi la uhalifu na kutakatisha fedha. Iwapo watakutwa na hatia, wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20 gerezani.

Kwa nini kesi ya Mardini ni muhimu?

Hukumu itakayotolewa itakuw pigo kubwa sio tu kwa kazi za kiutu, bali pia kwa haki za msingi za binaadamu wakati ambapo Umoja wa Ulaya na Ugiriki zinapitisha sera za uhamiaji zinazozidi kuwa na vizingiti. Hukumu ya kesi hii, itakuwa mfano wa kisheria nchini Ugiriki na Umoja wa Ulaya.

Pia itapeleka ujumbe kwamba kuwasaidia wakimbizi kunaweza kukuingiza katika makosa ya uhalifu na adhabu kali, ambazo zinaweza kuwazuia watu wanaofanya shughuli za kujitolea na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kutoa mchango mzuri katika masuala ya wakimbizi.

Mardini alikamatwa pamoja na Sean Binder raia wa Ujerumani na Ireland, na Nassos Karakitsos raia wa Ugiriki, Agosti 21, 2018 na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela, kabla ya kuachiwa kwa dhamana mwishoni mwa mwaka 2018. Walishtakiwa kwa makosa ya ujasusi, utakatishaji wa fedha, matumizi mabaya ya masafa ya redio na kughushi nyaraka.

Mnamo Januari 2023, Mahakama ya Makosa ya Jinai ya Mytilene ilitupilia mbali mashtaka hayo kutokana na kukosekana ushahidi na kasoro za kiuratibu na uendeshaji wa kesi. Miaka saba baada ya kukamatwa kwao, upande wa utetezi unadai kwamba bado kuna mashaka kuhusu asili na chanzo cha kisheria kuhusu ushahidi wa awali.

Pieter Wittenberg anasema amejiandaa kwa lolotePicha: Manolis Lagoutaris/AFP

Mapema Desemba 2025, Mahakama ya Rufaa ya Lesbos, ilianza kusikiliza mashtaka ya ziada, ikiwemo biashara haramu ya binaadamu na kuwa wanachama wa kundi la uhalifu.

Ushahidi ni upi?

Akizungumza na DW baada ya siku ya pili ya kesi yao Desemba 5, 2025, Sean Binder alisema kwamba ''mmoja angeweza kudhani baada ya miezi kadhaa ya upelelezi na miaka saba ya kucheleweshwa kesi hiyo, kungekuwa na ushahidi mwingi dhidi yetu, hoja ya kushawishi kuhusu kwa nini tunaweza kuwa na hatia.'' 

Kulingana na Binder, shahidi wa upande wa waendesha mashtaka, mlinzi wa pwani, ''alidhoofisha msingi wa kesi ya mshtaka, akithibitisha kwamba tulishirikiana naye.''

Waendesha mashtaka wanadai kuwa Mardini na wenzake waliitumia kazi ya kutoa huduma za kiutu kama njia ya kujikinga ili kuratibu shughuli na makundi ya wanaofanya biashara za magendo.

Mardini amejitetea akisema kuwa hakuna ushahidi wa yeye kujihusisha na uhalifu, na kwamba matendo yake yalilenga tu kuokoa maisha katika bahari na kutoa msaada kwa watu waliozongwa na matatizo makubwa.

Wakili wake, Zacharias Kesses, pia anasema kwamba shirika la misaada ambalo Mardini alikuwa anafanya kazi, liliwasiliana na mamlaka za pwani ya Ugiriki na kubadilishana taarifa.

Shirika la ERCI, ambalo Sarah Mardini alifanya kazi Picha: ERCI

Anthi Pazianou, mwandishi habari mwenye makaazi yake Lesbos, amekuwa akiripoti kuhusu mzozo wa wakimbizi kwenye kisiwa cha Lesbos kwa muongo mmoja. Anaielewa vizuri hali iliyojitokeza katika kisiwa hicho mwaka 2015, wakati idadi kubwa ya Wasyria ilipowasili Ugiriki.

Pazianou, anabainisha kuwa kazi ya kutoa misaada ya kiutu ilikuwa muhimu sana wakati huo kutokana na kosefu wa msaada wa kitaasisi kwa wakimbizi na ukweli kwamba kisiwa hicho kilizidiwa na wimbi la wakimbizi wanaowasili kwa njia ya bahari.

''Wanaojitolea waliratibu kuhusu upatikanaji wa chakula cha wakimbizi na nyaraka zao na walikuwa wakiwasiliana moja kwa moja na polisi,'' Pazianou aliiambia DW.

Mashirika yasiyo ya kiserikali yameikosoa kesi hiyo

Kwa miaka saba iliyopita, mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binaadamu ikiwemo Amnesty International, yamekuwa yakiifuatilia kwa karibu kesi hiyo. ''Kuwaacha watu wafe ni uhalifu,'' anasema Michalis Bakas mwanaharakati mwenye makaazi yake Lesbos. ''Ni jambo la ajabu linaloendelea na kwamba watu wengi wameuamia kwa miaka mingi.''

''Mashtaka hayana msingi na yanapaswa kufutwa mara moja,'' alisema Wies De Graeve, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Flanders la Ubelgiji, ambalo ni tawi la shirika la Amnesty International.

''Kesi hii haikupaswa kuwepo hapo awali. Tuna wasiwasi sana. Tunachokiona ni mshikamano wa kuzifanya huduma za uokozi kuwa uhalifu,'' aliiambia DW.

Aidha, akizungumza na DW, afisa wa shirika la Amnesty International nchini Ugiriki, Christos Dimopoulos amesema kwamba kesi hiyo inaangazia mfumo jumla wa jinsi Ugiriki na Ulaya kwa sasa zinashughulikia wimbi la wahamiaji na zinaeleza simulizi kuhusu haki za binaadamu ambayo sio nzuri hata kidogo.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limelaani vikali hatua ya kufanya huduma za uokozi kuwa uhalifu, huduma kama zile ambazo Mardini alishiriki, na mwaka 2023, Bunge la Ulaya lilitoa wito wa kuchukua hatua zaidi za umoja huo ili kuokoa maisha baharini.

Sophia Koufoupoulou, mtafiti wa kujitegemea kuhusu wimbi la wahamiaji nchini Ugiriki, amekuwa akifuatilia wimbi la wakimbizi huko Lesbos kwa zaidi ya miaka 20. Kwa mujibu wa Koufoupoulou, simulizi kuhusu uhamiaji imebadilika Ulaya; na hasa nchini Ugiriki.

Sean Binder akizungumza na waandishi habari nje ya mahakama huko Mytilene Januari 2023Picha: Manolis Lagoutaris/AFP

''Tulipokuwa tukizungumza kuhusu mshikamano na misaada ya kibinaadamu nchini Ujerumani na Ugiriki mwaka 2015, wafanyakazi wa kujitolea walisifiwa. Sasa tumeingia katika enzi ambapo Waziri wa Uhamiaji wa Ugiriki mwenyewe anawataja wahamiaji kwa njia isiyofaa kwa serikali inayodaiwa kuwa ya mrengo wa wastani,'' Koufoupoulou aliiambia DW.

Mawakili upande wa washtakiwa wanadai kuwa sio mwendesha mashtaka wala rais wa Mahakama ya Rufaa, ambaye aliipeleka kesi hiyo kwa ajili ya kusikilizwa, hawakuipitia upya au kutathimini kesi hiyo. Mawakili wanasema kwamba wote wawili walishindwa kutambua ukosefu kamili wa ushahidi.

Kesses, wakili wa Sarah Mardini aliiambia DW kwamba ''kesi hiyo haikupaswa kufika mahakamani kwa sababu haijakidhi mahitaji. Sehemu kubwa ya kesi hiyo tayari iliamuliwa mwaka 2023.'' Kesses pia anakosoa ukweli kwamba mahakama ya Ugiriki ilishindwa kushughulikia kesi ya Mardini haraka na kwa ufanisi.

Nini kinafuata?

''Tunaingia katika awamu ya mwisho wa kesi na tunasubiri kwa hamu kubwa wa tathmini ya ushahidi wote tuliowasilisha,'' alifafanua Kesses. Washtakiwa pia wana hamu ya kusikia kesi hiyo inakamilika, kwani imechukua muda wa miaka minane na imewaweka katika msongo mkubwa wa mawazo.

''Tunasubiri kwa hamu kubwa kesi ianze kusikilizwa Januari 15 na 16 na kulimaliza jinamizi hili. Kwa sababu ni jinamizi kwetu,'' alisema mshtakiwa Nasos Karakitsos wakati akizungumza na DW.

Karakitsos anasisitiza kuhusu umuhimu wa matokeo mazuri kwa wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada ya kibinaadamu kwa ujumla, akisema kwamba ingekuwa vizuri sio kwao tu, bali kwa kila mtu aliyeingia kwenye visiwa hivyo na kujitolea kusaidia kwa miaka yote hiyo.

Hukumu ya kesi hiyo inatarajiwa kutolewa Januari 16 au 17. Vyovyote vile itakavyokuwa, wataalamu wa sheria wanasema uamuzi huo unaweza kuathiri jinsi kazi ya mashirika ya kutoa misaada inavyofanywa na kusimamiwa katika mipaka ya Ulaya.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW