1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukosefu wa usalama waongezeka Somalia kuelekea uchaguzi

29 Machi 2022

Somalia inasogea uchaguzi wa rais ambao tayari umecheleweshwa, lakini wasiwasi unaongezeka kuhusu visa vingi vya mashambulizi ya kigaidi.

Somalia I Gewalt im Wahlkampf: 18 Tote nach Anschlag
Picha: Hassan Ali Elmi/AFP/Getty Images

Wanamgambo wameimarisha mashambulizi dhidi ya wawaniaji, maafisa wao na hata majeshi ya kigeni nchini humo. Viongozi wa Somalia wamesema ni sharti hatua muafaka za kumaliza machafuko hayo zichukuliwe ili kuwezesha uchaguzi kufanyika kwa amani. 

Mnamo Jumapili Machi 27, usiku kaskazini mwa Somalia. Wanamgambo waliishambulia kambi ya kijeshi ya Af-Urur na kuwaua wanajeshi wanne.

Shambulio la Al-Shabaab laua watu kadhaa Mogadishu

Shambulizi hilo limejiri wiki moja tu baada ya mashambulizi mengine mawili makubwa; moja katika mji mkuu Mogadishu na jingine Beledwayne eneo la kati nchini Somalia. Zaidi ya watu 50 waliuawa kwenye mashambulizi hayo.

Maelfu wakimbilia Mogadishu kutokana na ukame, njaa

Kukithiri kwa visa vya ukosefu wa usalama kumeanza kuibua mashaka kuhusu uchaguzi ujao wa urais kufanyika katika mazingira ya amani. Mchambuzi wa kisiasa na kiusalama Mohamed Mubarak ameeleza kwamba "Kuna sababu tatu kuu ambazo zimechochea ongezeko la machafuko Somalia. La kwanza ni kusitishwa kwa mashambulizi ya angani kutumia ndege zisizohitaji rubani- 'drones' dhidi ya wanamgambo hao. Ya pili ni kwamba huu ni mwezi kabla ya mfungo wa Ramadhan. Wanamgambo hao aghalabu huanza mashambulizi yao wakati kama huu hadi Ramadhan. Sababu ya tatu ni kwamba huu ni msimu wa uchaguzi na kawaida wanamgambo wanajaribu kuuvuruga uchaguzi kwa kufanya mashambulizi."

​​​​Kumekuwa na ongezeko la visa vya mashambulizi nchini SOmalia, mnamo wakati nchi hiyo pia ikikumbwa na mvutano wa kisiasa kati ya rais na waziri mkuu kuhusu usimamizi wa vyombo vya usalama.Picha: Farah Abdi Warsameh/AP Photo/picture alliance

Hussein Moalim Mohamud, mshauri wa zamani wa Rais Mohamed Farmajo kuhusu masuala ya usalama wa kitaifa amesema mvutano wa kisiasa kati ya rais na Waziri Mkuu umetoa fursa kwa wapiganaji hao wenye itikadi kali za dini ya Kiislamu kufanya mashambulizi.

UN, washirika wa Somalia wawataka viongozi kutatua mzozo

"Ongezeko la mashambulizi kama haya hutokea mara moja moja hasa wakati wanamgambo wa Alshabaab wanapohisi kuna udhaifu katika serikali. Wanajaribu kujipenyeza ili kuvuruga uchaguzi. Mvutano huu kati ya Rais na Waziri Mkuu kuhusu ni nani anasimamia vikosi vya usalama hakika umesababisha kuwepo mwanya mkubwa, na wanamgambo wa Alshabaab wanautumia mwanya huo,” amesema Hussein Moalim Mohamud.

Mohamud anaamini machafuko hayo hayahusiani kwa vyovyote vile na kukamilika kwa muda wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika- AMISOM. Hata hivyo Hodman Ahmed ambaye ni mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu na vilevile mkosoaji wa vikosi vya kigeni nchini humo anatofautiana na mtizamo wa Mohamud.

Mvutano kati ya Rais Mohamed Abdullahi Mohammed maarufu kama Farmajo na Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble (Kulia) unadaiwa kutoa fursa kwa wanamgambo wa Alshabaab kufanya mashambulizi.Picha: Abdirahman Yusuf/AFP/Getty Images

"Siku moja tu kabla ya shambulizi la Hallane, washirika wa Somalia, mashirika ya kimataifa, maafisa wa serikali, walikubaliana kuhusu mipango na sera ya mpito kwa Somalia. Lakini kilichofuata ni milipuko na mauaji. Kusudi la haya yote ni kutaka muda wa AMISOM urefushwe. Sera ya kigeni ndiyo huchochea haya,” amesema Hodman Ahmed.

Ujumbe huo wa AMISOM ulioundwa mwaka 2007 unatarajiwa kubadilishwa na ujumbe mpya wa mpito wa Umoja wa Afrika utakaonda sambamba na mipango ya mpito ya Somalia, kulisaidia jeshi la nchi hiyo inayozongwa na machafuko kuchukua usukani katika mapambano dhidi ya wanamgambo.

Mwandishi: Mohamed Odowa

Tafsiri: John Juma