1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine baada ya uchaguzi wa bunge

4 Oktoba 2007

Vyama vya kisiasa nchini Ukraine vimeanza mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto baada ya miezi kadhaa ya mvutano wa kisiasa uliofuatiwa na uchaguzi wa bunge uliomalizika mwishoni mwa wiki.

Rais Viktor Yuschenko wa Ukraine
Rais Viktor Yuschenko wa UkrainePicha: AP

Rais Viktor Yuschenko ametoa mwito wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa vyama vyote vikuu nchini humo.

Lakini mwito huo umezusha hali ya sintofahamu.

Mwito huo wa rais Viktor Yuschenko anaelemea upande wa nchi za Magharibi wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kwa vyama vyote vya kisiasa ikiwa ni pamoja na upande wa upinzani unaolemea Urusi baada ya ushindani mkali katika uchaguzi wa bunge uliomalizika nchini humo hakika umezusha wimbi zito la kisiasa.

Matamshi ya rais Yuschenko yamezusha maswali mengi iwapo chama cha kiongozi huyo cha Ukraine Yetu kitabakia katika msimamo wake hasa baada ya rais huyo kuonekana kana kwamba amelegeza uzi pale alipomkaribisha mpinzani wake mkubwa wa kisiasa waziri mkuu Viktor Yanukovych katika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo.

Baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo wa Jumapili ambapo chama cha rangi ya Chungwa kinacho ongozwa na bibi Yulia Tymoschenko mshirika wa rais Yuschenko kilipata fursa ya kujinyakulia ushindi japo kwa tafauti ndogo, rais Viktor Yuschenko aliwashangaza wengi pale badala ya kusherehekea ushindi huo wa mshirika wake alitumia nafasi hiyo kuwataka wapinzani wake wa kisiasa wasaidie katika kuunda serikali hatua ambayo imewaudhi washirika wengi wa kiongozi huyo wa Ukraine.

Wadadisi wamegawanyika katika mitazamo yao kuhusu mwito huo wa rais Yuschenko.

Baadhi yao wanasema mwito huo umetolewa kwa kuwa kiongozi huyo ni shupavu na baadhi yao wanahisi kuwa kiongozi huyo ni muonga.

Kinachojitokeza hapa ni kuwa mchezo wa kisiasa ndio kwanza umeanza nchini Ukraine ambayo zamani ilikuwa chini ya Urusi na yenye takriban raia milioni 47 waliogawanyika kihisia kati ya Urusi na Umoja wa Ulaya.

Yuiry Pavlkeno afisa wa ngazi ya juu kwenye chama kinachomuunga mkono rais Yuschenko amesema matamshi ya kiongozi huyo yasieleweke kuwa anataka kuunda serikali ya mseto pamoja na mpinzani wake waziri mkuu Yanukovych bali anataka tu kuwe na maelewano mazuri ya kisiasa kati yao.

Baada ya kumalizika uchaguzi wa siku ya Jumapili rais Viktor Yuschemnko alitarajiwa mara moja kuanza mazungumzo na bibi Yulia Tymoschenko kiongozi mwenye ushawishi mkubwa ndani ya chama cha rangi ya Chungwa kilichomuingiza madarakani rais huyo miaka mitatu iliyopita.

Chama cha bibi Yulia Tymoschenko cha rangi ya Chungwa kimekataa katakata kushirikiana na chama cha majimbo cha waziri mkuu Viktor Yanukovych.

Licha ya kwamba kulifanyika mazunguzo ya awali kati ya pande mbili za rais Yuschenko na bibi Tymoschenko ambayo yalijadili juu ya kuunda baraza la mawaziri ambalo moja kwa moja litamvua cheo chake waziri mkuu Viktor Yanukovych ambae chama chake pia kimepata viti si haba ila tu hakina mshirika madhubuti wa kuunda nae serikali ya mseto.

Wadadisi hapa wanasema huenda nyota ya bibi Tymoschenko imeanza kuzimika na labda rais Yuschenko atamtelekeza na kuungana na upande wa upinzani licha ya kwamba bibi Tymoschenko amepata ufanisi mkubwa wa kisiasa.

Mchambuzi wa maswala ya kisiasa wa mjini Kiev Kost Bondarenko anasema iwapo bibi Yulia Tymoschenko atapuuza nafasi ya kuunda serikali ya mseto na chama cha Ukraine Yetu cha rais Viktor Yuschenko basi kiongozi huyo atakuwa amepata sababu nzuri ya kuepukana na chama cha rangi ya Chungwa.

Mchambuzi huyo wa kisiasa anasema, nia hasa ya rais Yuschenko ni kuvunja makali ya bibi Tymoschenko au pia ya waziri mkuu Yanukovych na huu ni msingi madhubuti kabla ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2010.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW