1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine: Hatutaisamehe Urusi kwa mauaji ya Bucha

31 Machi 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Ukraine haitayasamehe majeshi ya Urusi kwa mauaji ya kiholela waliyoyafanya katika mji wake wa Bucha.

Ukraine Butscha | Jahrestag der Befreiung von Butscha | Selenskyj mit Golob, Sandu, Plenkovic, Heger
Picha: Ukrainian Presidential Press Service/Handout via REUTERS

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema hayo wakati Kyiv ikiadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kukombolewa kwa mji wa Bucha uliokuwa umekaliwa na majeshi ya Urusi. Mjio huo hata hivyo ulirejeshwa mikononi mwa Ukraine mwishoni mwa mwezi Machi mwaka jana baada ya Urusi kuachana na jaribio la kuudhibiti mji mkuu, Kyiv. 

Zelensky alinukuliwa akisema kwenye maadhimisho hayo mjini Bucha ambako bendera ya Ukraine ilikuwa ikipeperuka ya kwamba uovu wa Urusi utazikwa hapohapo Ukraine na kamwe hawatakuwa na nguvu ya kuinuka tena. Akasema ubinadamu utashika hatamu.

Soma Zaidi: Amnesty: Urusi imefanya uhalifu wa kivita, Ukraine

Rais wa Ukraine aliwavalisha medali wanajeshi walifanikisha kuurejesha mji huo na jamaa wa wanajeshi waliofariki wakati wa mapambano pia walipokea medali kwa niaba yao.

Picha za miili ya watu iliyokuwa imelala katika mitaa ya Bucha zilisambaa ulimwenguni kote baada ya Ukraine kuudhibiti tena mji huo. Kyiv ikasema zaidi ya watu 1,400 waliuawa mjini Bucha wakati wanajeshi wa Urusi walipoukali mji huo. Miongoni mwao kulikuwa na watoto 37 na zaidi ya watu 175 walikutwa katika makaburi ya pamoja na kwenye vyumba vya mateso.

Rais Volodymyr Zelensky akimkabidhi medali mmoja ya wanajeshi waliofanikisha vita vya kuurejesha mji wa Bucha.Picha: Gleb Garanich/REUTERS

Hadi sasa Urusi imekanusha vikali madai ya vikosi vyake kufanya mauaji hayo, ubakaji na mateso na kuiacha miili ya wahanga ikiwa imetapakaa kwenye mitaa ya mji huo wa Bucha baada ya kukimbia.

Belarus yaionya Ukraine kusahau kuvishinda vita dhidi ya Urusi.

Wachunguzi wa kimataifa hivi sasa wanakusanya ushahidi wa uhalifu wa kivita katika miji ya Irpin, Bucha na kwingineko. Zelensky anauelezea Bucha kama mfano wa mauaji ya kiholela yaliyofanywa na wanajeshi wa Urusi nchini humo.

Kwingineko, huko Belarus Rais Alexander Lukashenko amesema leo kwamba Urusi inaweza kupeleka silaha zake za nyuklia nchini humo, baada ya mapema wiki hii rais Vladimir Putin kutangaza kwamba Urusi inalenga kupeleka makombora ya kuongozwa ya masafa marefu na mafupi nchini Belarus, zinazohofiwa kuibua kitisho kikubwa hata zaidi.

Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amewaambia WaUkraine kusahau kwamba watavishinda vita dhidi ya Urusi.Picha: BelTA/Maxim Guchek/REUTERS

Anatoa matamshi hayo wakati wasiwasi ukiongezeka juu ya mzozo kati ya Urusi na Ukraine na fikra kwamba mataifa ya magharibi yanataka kuivuruga Urusi na Belarus, huku akiowaonya waUkraine kusahau kabisa fikra ya kushinda kwenye vita hivyo.

''Hii leo pande zote zinajua kabisa kwamba haiwezekani kushinda. Zaidi ya yote, WaUkraine wanadhani watashinda. Huu ni ujinga. Haiwezekani kulishinda taifa lenye nguvu kinyuklia. Ikiwa Urusi itahisi kuwa inashindwa, itatumia silaha kali zaidi."

Na huko Moscow, Urusi Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov amesema sera mpya ya kigeni ya nchi hiyo iliyoidhinishwa na Rais Putin inayaelezea mataifa ya Magharibi kama kitisho kikubwa cha Moscow.

Tangazo la Lavrov linatolewa wakati uhusiano kati ya Urusi na Magharibi ukiwa umeingia kwenye mgogoro kufuatia uamuzi wake wa kuivamia Ukraine. Lavrov amesema katika mkutano wa baraza la usalama uliorushwa kwenye televisheni ya kwamba sera hiyo imetambua asili ya kitisho hicho dhidi ya usalama na maendeleo ya Urusi, ambayo imechochewa na hatua za mataifa maadui.

Soma Zaidi: Jumuiya ya kimataifa yakemea mpango wa nyuklia wa Putin

Marekani inatajwa moja kwa moja kama mchochezi mkuu na kiongozi wa chuki dhidi ya Urusi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW