1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Makombora ya Urusi yauwa watu wawili na kujeruhi 10

Daniel Gakuba
25 Aprili 2023

Watu wawili wameuawa na wengine 10 wamejeruhiwa katika shambulizi la Urusi, lililoharibu jengo katika mji wa Kupiansk mashariki mwa Ukraine, wakati jeshi la Ukraine likiandaa mashambulizi ya kuyakomboa maeneo yake.

Ukraine I Raketenangriff auf Museum in Kupiansk
Jengo lililoharibiwa vibaya katika mji wa Kupiansk, UkrainePicha: REUTERS

Kulingana na duru za maafisa wa Ukraine, jeshi la Urusi limetumia makombora chapa S-300 kuulenga mji wa Kupiansk ulio katika mkoa wa Kharkiv, na kulivunja jengo la kuhifadhi historia ya kikanda lililo katikati ya mji. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameweka mtandaoni video inayoonyesha jengo hilo likiwa limeporomoshwa, na waokoaji wakifanya tathmini ya madhara yaliyotokea.

Soma zaidi: Urusi, mataifa ya Magharibi uso kwa uso Baraza la Usalama

Kiongozi huyo wa Ukraine amesema na hapa namnukuu, ''nchi ya kigaidi inafanya kila iwezalo kuiangamiza Ukraine, kuharibu historia yake, utamaduni wake na watu wake. Inawauwa Waukraine kwa njia za kishenzi kabisa,'' mwisho wa kumnukuu.

Zelenskiy alisema kuwa mtu wa kwanza aliyeuawa alikuwa mfanyakazi wa jumba la makumbusho, na baadaye gavana wa mkoa wa Kharkiv, Oleh Syniehubov amethibitisha kuwa mwili wa mhanga mwingine wa shambulizi hilo umepatikan kutoka chini ya kifusi cha jengo. Mbali na waliopoteza maisha, amearifu gavana Syniehubov watu wengine 10 wamejeruhiwa, watatu miongoni mwao wakilazimika kulazwa hospitalini.

Makombora chapa S-300 yaliyotumiwa na Urusi kuupiga mji wa KupianskPicha: Sergei Savostyanov/ITAR/TASS/imago

Hofu kuwa Kupiansk yaweza kutekwa tena na Urusi

Mji wa Kupiansk ulikamatwa na Urusi mwanzoni mwa uvamizi wake dhidi ya Ukraine, lakini ulirejea tena mikononi mwa Ukraine mwezi Septemba katika kampeni ya kushitukiza ya kuyakomboa maeneo yake. Hivi sasa kuna hofu kuwa yumkini Urusi inanuia kuukamata tena mji huo, na tangu mwezi Machi Ukraine imewahimiza wakaazi walio dhaifu kiafya kuanza kuuhama.

Soma zaidi:Urusi yadai kukamata maeneo zaidi ya Bakhmut 

Haya yanajiri huku Kiev ikiandaa operesheni nyingine kabambe ya kuifurusha Urusi kutoka kwenye ardhi yake, ikitegemea zana mpya za kijeshi inazopatiwa na washirika wake wa magharibi. Sambamba na azma hiyo, Rais Zelenskiy amefanya mkutano na makamanda wakuu wa jeshi la nchi yake, na kurejelea mwito kwa nchi washirika kuharakisha msaada wa silaha.

Ukraine inatarajiwa kuanzisha operesheni ya kuyakomboa maeneo yake yanayokaliwa na UrusiPicha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Urushi yatishia tena kutumia silaha za nyuklia

Kwa upande mwingine, aliyekuwa rais wa Urusi Dmitry Medvedev ambaye ni mshirika wa karibu wa rais wa Urusi Vladimir Putin, amesema ulimwengu ni mgonjwa mahtuti na yumkini uko kwenye ukingo wa vita vipya vya dunia. Akizungumza leo katika kiwanda cha kuunda makombora, Medvedev amezionya nchi za magharibu kutobeza utayari wa Urusi kutumia silaha zake za nyuklia ikiwa itakabiliwa na shambulio la kutishia usalama wake.

Soma zaidi: Washirika wa Ukraine wakutana Ujerumani kujadili msaada zaidi

Na katika juhudi za kuhifadhi mshikamano na Ukraine, Umoja wa Ulaya unajaribu kutafuta njia ya kutuliza wasiwasi wa wanachama wake, ambao sekta zao za kilimo zinatishiwa na nafaka nafuu kutoka Ukraine.

 

Vyanzo: rtre, dpae, ape

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW