1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine: Mashambulizi ya Urusi yawaua watu 3 Odessa

14 Juni 2023

Maafisa wa Ukraine wamesema kuwa watu watatu wameuawa na wengine 13 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya makombora ya Urusi yaliyotokea kwenye mji wa bandari wa Odessa.

Ukraine Krieg | Angriff auf Odessa
Picha: State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Kamandi ya operesheni ya jeshi la kusini imeeleza Jumatano kuwa kombora aina ya Kalibr limeshambulia ghala la chakula na kusababisha moto, ambapo watu watatu waliuawa na wengine saba walijeruhiwa katika eneo hilo.

Jeshi la Ukraine limesema jumla ya makombora manne chapa Kalibr yalirushwa mapema Jumatano asubuhi kwenye mji huo.

Kwa mujibu wa jeshi hilo, watu wengine sita walijeruhiwa katika shambulizi lililoilenga miundombinu ya kiraia, ikiwemo kituo cha biashara, kituo cha mafunzo, eneo la makaazi, pamoja na migahawa na maduka.

Vikosi vya Ukraine vyasonga mbele

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Hanna Maliar amesema vikosi vya jeshi la nchi hiyo vimeripoti kusonga mbele na kufanikiwa kwenye maeneo kadhaa katika hatua za awali za mashambulizi ya kuyarudisha maeneo yanayodhibitiwa na Urusi, licha ya vikosi vya Urusi kuongeza mashambulizi ya anga.

Maliar amesema vikosi vya Ukraine vimesonga mbele umbali wa mita 200-500 kwenye maeneo mbalimbali ya mapambano kuzunguka mji wa Bakhmut katika jimbo la Donetsk, na umbali wa mita 300-350, kusini mwa jimbo la Zaporizhzhia.

Watu wakiwa nje ya vibaraza kwenye jengo la makaazi ambalo limeshambuliwa Odesa Picha: Lyashonok Nina/Ukrinform/ABACA/IMAGO

Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema kuanza kwa mashambulizi ya Ukraine kunaweza kumfanya Rais wa Urusi, Vladimir Putin atambue kuwa hawezi kushinda kwenye uwanja wa mapambano, na analazimika kutafuta suluhusho kwa njia ya amani.

"Tunaona kwamba Ukraine inapiga hatua na wanaikomboa ardhi yao. Maendeleo haya ni ushahidi wa ujasiri unaoonyeshwa na vikosi vya Ukraine pamoja na kujitolea kwao," alifafanua Stoltenberg.

Msaada wa NATO unaleta mabadiliko ya kweli

Akizungumza kabla ya mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa NATO baadae wiki hii, Stoltenberg amesema maendeleo hayo pia yanaonyesha kuwa msaada unaotolewa na washirika wa muungano huo wa kijeshi unaleta mabadiliko ya kweli katika uwanja wa vita.

Ama kwa upande mwingine, Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amesema nchi yake imeanza kupokea silaha za nyuklia kutoka Urusi.

Lukashenko amesema wamepokea makombora na mabomu kutoka Urusi, huku akibainisha kuwa mabomu hayo yana nguvu mara tatu zaidi ya yale yaliyodondoshwa Hiroshima na Nagasaki.

Rais wa Belarus Alexander LukashenkoPicha: Mikhail Klimentyev/Kremlin/Sputnik/REUTERS

Wakati huo huo, bunge la Urusi limesema limepiga kura kuonyesha uungaji wake mkono wa awali kwa sheria itakayoiruhusu wizara ya ulinzi kusaini mikataba na watuhumiwa au waliokutwa na hatia ili kwenda kupigana Ukraine.

Hata hivyo, watu waliokutwa na hatia ya uhalifu wa kingono, uhaini, ugaidi au itikadi kali, hawatoandikishwa katika mpango huo.

Huku hayo yakijiri, maafisa wa Urusi wamesema ziara ya Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Matumizi ya Nishati ya Nyuklia IAEA, Rafael Grossi katika kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia imesogezwa mbele hadi Alhamisi. Grossi alitarajiwa kukitembelea kinu hicho Jumatano, baada ya uharibifu mkubwa katika bwawa la Kakhovka.

(DPA, AFP, AP, Reuters, DW)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW