Ukraine na Marekani zasaini "makubaliano ya uwekezaji"
1 Mei 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi wa Ukraine Yulia Svyrydenko, aliyetia saini makubaliano hayo mjini Washington, amesema vifungu muhimu vya mkataba huo ni pamoja na kwamba rasilimali zote kwenye eneo la Ukraine na eneo la maji ni mali ya Ukraine.
"Ni taifa la Ukraine ndilo linaloamua nini na wapi pa kutoa," aliandika kwenye X. "Hakuna upande utakaokuwa na nguvu zaidi ya jingine - Hii ikiakisia usawa katika ushirika wa mataifa yote mawili."
Marekani chini ya makubaliano hayo, imefunguliwa milango ya kuchimba madini ya thamani na adimu nchini Ukraine ili iendelee kupata msaada wa Marekani wakati ikiendelea kukabiliana na uvamizi wa Urusi.
Kulingana na Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal, makubaliano hayo yataanzisha ushirikiano sawa kati ya nchi hizo mbili na kudumu kwa miaka 10.
Soma Pia: Trump asema "SAWA" Zelensky kuzuru Marekani kusaini mkataba wa madini
Msaada uliotolewa na Marekani kwa Ukraine kabla ya mkataba kusainiwa hautahesabika. Tofauti na rasimu ya awali, mpango huo hautakinzana na mkakati wa Ukraine wa kujiunga na Umoja wa Ulaya - kifungu muhimu cha Kyiv kwenye makubaliano hayo.
Rais wa Marekani Donald Trump ameshinikiza kupatikana kwa makubaliano kwa miezi kadhaa ambayo anasema yatakuwa ni kama malipo kwa Marekani kufuatia msaada wa kijeshi na kifedha ambayo imeipatia Ukraine.
Mazungumzo, hata hivyo, yalikwama baada ya mkutano uliokwenda mrama baina ya Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, Trump na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance katika Ofisi ya Oval, ambao walimlaumu Rais Zelenskyy kwa kukosa shukrani.
Soma Pia: Mkutano wa Zelensky, Trump wamalizika vibaya
Marekani imekuwa ikisaka malighafi kama urani na lithium
Marekani imekuwa ikiangazia namna ya kupata malighafi zaidi ya 20 kama za titanium, urani, lithium, grafiti na manganese, zinazoonekana kuwa muhimu kwa ajili ya maslahi yake, ikiwa ni pamoja na baadhi abazo si madini kama vile mafuta na gesi asilia.
Aidha Naibu Waziri Mkuu huyo wa Ukraine ameandikwa kupitia mtandao wa X kwamba pamoja na makubaliano hayo na Marekani, wataunda Mfuko ambao utavutia uwekezaji wa kimataifa nchini mwao.
Huku hayo yakifikiwa, Umoja wa Ulaya umesema una "mpango mbadala" unaolenga kuongeza shinikizo la kiuchumi kwa Urusi ikiwa Marekani itafikia makubaliano na Moscow pekee, mwanadiplomasia mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo Kaja Kallas alisema.
"Dalili tunayoiona ni kama wanatafakari kuiacha Ukraine na kwa upande mwingine wasiingie makubaliano na Urusi kwa sababu kuna ugumu," Kallas aliambia gazeti la Financial Times la Uingereza.
"Pia kuna mpango mbadala, lakini tunapaswa kufanya kazi kwanza ule wa kwanza," Kallas alisema.
Aliongeza kuwa Umoja wa Ulaya upo kwenye mazungumzo na Marekani na washirika wengine wa kimataifa ili kuhakikisha vikwazo dhidi ya Urusi vinaendelea kuwepo.