1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine na Urusi zawekeana vikwazo vya biashara

Admin.WagnerD24 Desemba 2015

Bunge la Ukraine Alhamisi (24.12.2015) limepiga kura kuipa serikali haki ya kuiwekea Urusi vikwazo vya kiuchumi baada ya nchi hiyo kusema kwamba itaisitisha kanda ya biashara huru na Ukraine kuanzia Januari Mosi

Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk .
Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk .Picha: picture-alliance/dpa/A. Kravchenko

Muswada huo wa sheria ulioungwa mkono na wabunge 291 kati ya wabunge 420 utaanza kutekelezwa baada ya kusaniwa na rais.

Rais Vladimir Putin wa Urusi wiki iliopita aliamuru katika agizo la rais kusitishwa kwa biashara huru na Ukraine kutokana na kile ilichokitaja kuwa mazingira yasio ya kawaida yenye kuathiri maslahi na usalama wa uchumi wa Urusi.

Hatua hiyo ya Urusi inalipiza kisasi hatua ya Ukraine ya kuwa na makataba huru wa kibishara na Umoja wa Ulaya ambao unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi ujao na ambao Urusi inasema utapelekea kufurika kwa bidhaa za Ulaya nchini Urusi na kudhoofisha ushindani wa bidhaa zake inazozisafirisha kwenda Ukraine.

Kulihami soko la Ukraine

Waziri Mkuu wa Ukraine Arseny Yatsenyuk ameliambia bunge kabla kupigwa kwa kura hiyo kuwa Ukraine ilikuwa imepanga kuchukuwa hatua za vikwazo kuanzia mwezi wa Januari kama ilivyofanya Urusi dhidi ya nchi yake.

Majeno yalioharibiwa ni taswira ya kawaida nchini Ukraine.Picha: DW/F. Warwick

Amekaririwa akisema " Tutalihami soko la ndani la Ukraine.Urusi itapata jibu kutoka serikali ya Ukraine kwa njia ya vikwazo vya biashara na vikwazo dhidi ya bidhaa za Urusi sawa na vile nchi hiyo ilivyoiwekea Ukraine."

Rais Petro Poroshenko wa Ukraine amesema wiki iliopita kwamba alikuwa amesikitishwa na uamuzi huo wa Urusi wa kukomesha biashara nafuu na Ukraine lakini alikuwa tayari kugharamika na uamuzi huo kwa kuwa na mkataba huru wa biashara na Umoja wa Ulaya ambao utaanza kutekelezwa kikamilifu hapo Januari Mosi.

Vita vya biashara

Ukraine imesema vita vyake vya biashara na Urusi yumkini vikaigharimu nchi hiyo dola milioni sita hapo mwakani au asilimia 0.6 ya faida yake ya biashara.

Utata kuhusu mkataba ya kibiashara kati ya Ukraine na Umoja wa Ulaya ndio chanzo cha machafuko mjini Kiev ambayo yaliishia kwa kupinduliwa kwa rais aliekuwa mshirika wa Urusi hapo mwaka 2014.Baadae Urusi ikalinyakuwa jimbo la Crimea na kuunga mkono uasi wa kutaka kujitenga mashariki mwa nchi hiyo hatua ambayo imepelekea kuzuka kwa mzozo mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa kwa miongo mingi kati ya Urusi na mataifa ya magharibi.

Urusi mara kwa mara imekuwa ikielezea wasi wasi wake kwamba makubaliano ya biashara huru kati ya Ukraine na Umoja wa Ulaya yumkini yakafurika soko la nchi hiyo kwa biadhaa za Ulaya na mazumngumzo ya pande tatu na Umoja wa Ulaya yaliokuwa yakifanyika kwa miezi kadhaa kutafuta ufumbuzi yameshindwa kuwa na tija.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Iddi Ssessanga