Poland yasema kumekuwa na shambulizi karibu na mpaka wake
17 Septemba 2026
Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema kuwa wanafuatilia hatua zitakazochukuliwa kufuatiwa uamuzi wa bunge hilo la Marekani.
"Hatua hiyo inaangukia katika kundi la vitendo visivyo vya kirafiki, na bila shaka kuwekewa vikwazo zaidi na Marekani kutafanya juhudi za kufikia suluhu ya amani nchini Ukraine kuwa ngumu zaidi.''
Baraza la wawakilishi la Marekani launga mkono vikwazo dhidi ya Urusi
Jana Jumatano, Baraza la Wawakilishi la Marekani linaloongozwa na chama cha Republican lilipitisha vikwazo hivyo kwa kura 262 dhidi ya 159, na kutoa idhini ya mwisho ya bunge kwa juhudi kubwa zaidi za kisheria za Marekani dhidi ya Moscow tangu Donald Trump aliporejea madarakani.
Trump amesema atasaini sheria hiyo, ambayo ilipitishwa kwa urahisi katika bunge la Seneti mwezi uliopita kwa kura 86 dhidi ya 11.
Sheria hiyo inalenga sekta za nishati na ulinzi za Urusi, Rais Vladimir Putin na maafisa wengine waandamizi, pamoja na kile ambacho Moscow inakiita meli za siri za mafuta zinazotumiwa kukwepa vikwazo vya Magharibi.
Pia inampa Trump mamlaka ya kutoza ushuru wa hadi asilimia 100 kwa wanunuzi wakubwa wa mafuta na gesi ya Urusi, ikiwemo uwezekano wa kuzilenga China na India, katika jitihada za kukata mapato yanayofadhili vita vya Moscow nchini Ukraine.
Kwa upande wake, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amepongeza kupitishwa kwa sheria hiyo akisema ni hatua yenye "ishara kubwa ya maana" na akawashukuru wabunge wa Marekani.
Katika taarifa, Zelensky amesema muswada huo ni kile alichokiita silaha ya nguvu inayoweza kusitisha vita hivyo na kuifikisha Urusi katika hatua ambayo italazimika kuchagua amani.
Pia amesema vikwazo vinapaswa kuwa vikali ili juhudi zote za amani, ikiwemo juhudi za pamoja za kidiplomasia na Marekani, Ulaya na marafiki wao ziweze kufanikiwa.
Poland yasema kumekuwa na shambulio lingine karibu na mpaka wake
Waziri mkuu wa Poland Donald Tusk, amesema kumekuwa na shambulizi lingine karibu sana na mpaka wa Poland, katika eneo ambalo haliko mbali na Dorohusk ambapo inadaiwa kituo cha mafuta kimeshambuliwa tena.
Tusk amesema haya baada ya kukutana na Kansela wa Austria Christian Stocker mjini Warsaw.
Amelieleza tukio hilo kuwa mlipuko mkubwa huku walinzi wa mpaka wa Poland wakisema kivuko karibu na kijiji cha Dorohusk hakikushambuliwa moja kwa moja.
Baada ya tukio hilo, waziri wa ulinzi wa Poland Wladyslaw Kosiniak-Kamysz aliandika ujumbe kwenye mtandao wa X kwamba shambulizi hilo lilifanyika kilomita chache kutoka mpakani, lakini hakukuwa na ukiukaji wa anga ya Poland na kuongeza kuwa Urusi haisitishi vitendo vyake vya uchokozi.
Kwengineko, Shirika la Greenpeace limesema leo kuwa Moscow inahujumu kwa makusudi usambazaji wa umeme katika kiwanda cha nyuklia cha Zaporizhzhya kilicho chini ya udhibiti wa Urusi, katika juhudi za kuilaumu Ukraine kwa kuhatarisha usalama wa kituo hicho.