1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Ukraine: Tupo tayari kusitisha mapigano kwa siku 30

10 Mei 2025

Ukraine imesema iko tayari kwa usitishaji mapigano na Urusi kwa muda wa siku 30 kuanzia siku ya Jumatatu.

Ukraine | Washirika wa Ulaya mjini Kyiv
Viongozi wa Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na Poland wakiwa na Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine mjini Kyiv. Viongozi hao wako nchini Ukraine kuonesha mshikamano na taifa hilo. Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Hayo yameelezwa na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo Andrii Sybiha katika wakati viongozi wa mataifa manne ya Ulaya wako mjini Kyiv kwa ziara ya kuonesha mshikamano na taifa hilo lililo vitani.

"Ukraine na washirika wake wako tayari kusimamisha mapigano bila masharti yoyote, kwa maana ya ardhini, angani na baharini kwa muda wa siku 30 kuanzia Jumatatu", ameandika waziri Sybiha kupitia mtandao wa kijamii wa X.

"Iwapo Urusi itakubali na usimamizi kamili wa makubaliano hayo utahakikishwa, usitishaji mapigano na njia za kuimarisha imani ya kila upande, vitafungua njia ya kuanza mashauriano ya uhakika ya amani," ameongeza mwanadipomasia hiyo.

Viongozi wa mataifa manne ya Ulaya ziarani Kyiv 

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ukraine, Andrii Sybiha.Picha: Angela Weiss/AFP/Getty Images

Ujumbe wa Sybiha ameutoa wakati viongozi wa mataifa manne ya Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Poland wamekutana na Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine mjini Kyiv kuongeza uzito wa shinikizo lao kwa Urusi ikubali usitishaji mapigano.

Safari yao imefanyika siku moja baada ya Rais Vladimir Putin wa Urusi kuandaa gwaride kubwa la kijeshi mjini Moscow kukumbuka Siku ya Ushindi dhidi ya utawala wa Wanazi wa Ujerumani.

Siku hiyo ilikwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 80 tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Hiyo ni ziara ya kwanza kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk kusafiri pamoja kuitembelea Ukraine. Waliwasili nchini humo asubuhi ya siku ya Jumamosi wakitumia usafiri wa treni kutokea Poland.

Viongozi hao ni sehemu ya wale wa mataifa yaliyo sehemu ya yanayounda kile kinachofahamika kama "muungano wa hiyari" wa kuisaidia Ukraine, ambayo yamekuwa yakikutana mnamo miezi ya karibu kuandaa jinsi ya kuipiga jeki Ukraine pale mkataba wa amani utakapopatikana.

Baada ya kukutana na Rais Zelenskyy, viongozi hao kwa pamoja walifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Donald Trump wa Marekani kujadili juhudi za amani. Hayo yameelezwa na Waziri Sybiha.

Kabla ya mkutano huo kuanza, chanzo kimoja cha kidiplomasia cha Ufatansa, kilisema viongozi hao watajadili kwa kina pendekezo la usitishaji mapigano kwa siku 30 na iwapo Moscow italikataa, watachukua hatua ya pamoja ya kuiwekea vikwazo vipya Urusi.

Urusi yataka nchi za magharibi zisitishe ufadhili wa kijeshi kwa Ukraine 

Ziara yao inafanyika chini ya kiwingu cha juhudi zinazosuasua za kumaliza vita vya zaidi ya miaka mitatu kati ya Urusi na Ukraine.

Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: JIM WATSON/POOL/AFP/Getty Images

Rais Trump wa Marekani anajaribu kusukuma kupatikana haraka kwa mkataba wa amani jambo ambalo limezusha hamkani ndani ya Ukraine na washirika wake wa Ulaya tangu mwezi Januari.

Kiongozi huyo ametishia kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi na vilevile ameashiria anaweza kuachana na jitihada zake za kusaka amani kati ya pande hizo mbili.

Mnamo siku ya Alhamisi alitoa mwito wa usitishaji mapigano kwa siku 30 ambao mara moja uliungwa mkono na Rais Zelenskyy na viongozi wa Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo Urusi yenywe imesema inaunga mkono pendekezo hilo lakini chini ya masharti kadhaa.

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov amesema ni sharti mataifa ya magharibi yasitishe msaada wao wa kijeshi wanaoipatia Ukraine.

Amesema iwapo hilo halitatimizwa, usitishaji mapigano utakuwa mgumu kutekelezwa kwa sababu, Moscow inaamini utatumika kuinufaisha Ukraine kujipanga upya kijeshi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW