1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine, Uingereza zasaini mkataba wa ushirikiano

16 Januari 2025

Waziri Mkuu wa Uingereza Kier Starmer na Rais Volodymyr Zelensky wamesaini mkataba wa ushirikiano, ambapo Starmer ameihakikishia Kiev kwamba nchi yake itaendelea kuisaidia kikamilifu kukabiliana na uvamizi wa Urusi.

Ukraine Kier Starmer
Waziri Mkuu wa Ukraine, Kier Starmer, (kushoto) akiwasili mjini Kiev siku ya Alhamis (Januari 16).Picha: Carl Court/Getty Images

Starmer na Zelensky wamesaini mkataba huo wa miaka 100 wenye lengo la kuimarisha mafungamano ya kiusalama na uhusiano wa nchi zao.

"Leo ni siku ya kihistoria, mahusiano yetu yamekuwa makubwa kuliko ilivyowahi kuwa hapo kabla." Alisema Zelensky mara tu baada ya kusaini mkataba huo.

Kwa upande wake, Starmer alisema kuwa serikali yake ingeliipa Ukraine mfumo wa ulinzi wa anga unaotembea, ambao alitarajia ungelikidhi mahitaji ya Kiev.

Soma zaidi: Keir Starmer kusaini mkataba wa ushirikiano na Ukraine

Starmer aliwasili mjini Kiev kwa ziara ya kushitukiza mchana wa Alhamis (16 Januari), akionesha uungaji mkono wa nchi yake kwa Kiev baada ya takribani miaka mitatu ya uvamizi wa Urusi.

Taarifa ya Ofisi yake ya Downing Street ilisema kuwa mkataba huo wa kihistoria, unaojumuisha masuala ya ulinzi, biashara, nishati na sayansi, ni njia ya kuipa nguvu Ukraine.

Kabla ya kusaini mkataba huo, viongozi hao wawili waliweka mashada ya maua kwenye ukuta wa kumbukumbu ya wale waliouawa kwenye vita na Urusi.

Ukuta huo, ulio nje ya Nyumba ya Watawa ya Mtakatifu Michael mjini Kiev, umepambwa kwa picha za wahanga hao. 

Mashambulizi ya droni za Urusi

Kusainiwa kwa mkataba huo kulifanyika masaa machache baada ya jeshi la anga la Ukraine kudai kwamba limezindunguwa droni 34 kati ya 55 zilizorushwa na Urusi usiku wa kuamkia leo. Kwa mujibu wa jeshi hilo, droni 18 zilishindwa kufikia shabaha zake.

Mojawapo ya nyumba zilizoshambuliwa na droni za Urusi mjini Kiev.Picha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Kwa upande wake, Ukraine ilisema nayo ilikuwa imelishambulia ghala la mafuta kwenye mkoa wa Voronezh nchini Urusi.

Soma zaidi: Ukraine yazidungua droni 34 kati ya 55 zilizorushwa na Urusi

Mkuu wa majeshi wa Ukraine ameandika kupitia mtandao wa Telegram kwamba kwa uchache droni tatu zilimelishambulia ghala hilo na kusababisha moto.

Kwa mujibu wake mkuu huyo wa jeshi, ghala hilo lilikuwa linahifadhi mafuta kwa ajili ya jeshi la Urusi.

Urusi yakanusha tuhuma za Tusk

Kwa upande mwengine, Ikulu ya Kremlin imesema tuhuma zilizotolewa na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk, kwamba Urusi ilikuwa inapanga matendo ya kigaidi kwenye anga la Poland na mataifa mengine hazina msingi wowote. 

Waziri Mkuu wa Poland, Donald Tusk.Picha: Antoni Byszewski/Fotonews/Newspix/IMAGO

Tusk alitoa tuhuma hizo siku ya Jumatano (Januari 15) baada ya mkutano wake na Zelensky mjini Warsaw.

Soma zaidi: Rais Zelensky wa Ukraine afanya mazungumzo na waziri mkuu wa Poland Donald Tusk

Waziri mkuu huyo wa Poland alikuwa akizungumzia vifurushi vilivyoripuka kwenye maghala ya usambazaji bidhaa barani Ulaya.

Maafisa wa usalama wa Magharibi walidai kuwa miripuko hiyo ilikuwa sehemu ya majaribio ya njama za Urusi kuziripua ndege za mizigo zinazoelekea Marekani.

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, aliwaambia waandishi wa habari mjini Moscow kwamba hizo ni tuhuma zisizokuwa na mashiko yoyote yale. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW