1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Ukraine: Urusi inaendelea kushambulia eneo la Donbas

Hawa Bihoga
16 Agosti 2024

Jeshi la Ukraine limesema vikosi vya Urusi vinaendelea kuushambulia mkoa wa Donbas, ambapo mapigano makali yanaripotiwa hasa katika eneo la Pokrovsk huku Moscow ikisema Kyiv ilijaribu kushambulia daraja lake la Crimea.

Ukraine | Sumy | Wanajeshi wa Ukraine
Wanajeshi wa Ukraine wakiwa katika gari la kivita.Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa ripoti ya jeshi la Ukraine, Warusi walifanya mashambulizi kadhaa ya ndege na makombora, lakini mashambulizi hayo yalizuiwa. Urusi imekuwa ikijaribu kuuleta mkoa wote wa Donbas chini ya udhibiti wake.

Pande zote mbili pia zimeripoti kudungua droni kadhaa za upande mwingine baada ya kushambuliana. Urusi inaendeleza mashambulizi katika mkoa wa Donbas hata baada ya uvamizi wa Ukraine katika mkoa wake wa Kursk.

Katika sehemu ya kampeni yake ya kujilinda, Ukraine ilianzisha operesheni ya mashambulizi ya ardhini katika ardhi ya Urusi kwa mara ya kwanza Agosti 6, ambapo vikosi vya jeshi la Ukraine vilichukuwa udhibiti wa dazeni kadhaa za vijiji katika mkoa huo.

Wanablogu wa kijeshi nchini Urusi, wameripoti mapigano makali na kwamba wanajeshi wa Ukraine wamepata hasara kubwa katika eneo la Kursk, lakini Ukraine haijatoa tamko rasmi.

Soma pia:Ukraine: Uvamizi Kursk walenga "mazungumzo ya haki"

Maafisa wa mkoa wa Kursk wameendelea kuhamisha wakazi kutoka majumbani mwao leo Ijumaa, ambapo kaimu gavana wa mkoa huo Alexei Smirnov alitoa vidio ikionesha wafanyakazi wa kujitolea wakiwasaidia wazee kutoka wilaya ya Glushkovo baada ya gavana huyo kuamuru wahamishwe jana, katika ishara kwamba vikosi vya Ukraine huenda vilikuwa vinasonga mbele kuelekea eneo hilo.

Gavana Smirnov pia alitembelea wanajeshi wanaotibiwa katika moja ya hospitali ya mji baada ya kujeruhiwa katika mapigano, huku akiahidi ushindi.

"Nina hakika kwamba kwa uungaji mkono wa jamii yetu sasa hivi, tutashinda na kulikomboa eneo letu. Na kisha tutaishi maisha ya amani."

Urusi yasema Ukraine bado inashambulia maeneo yake

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema mashambulizi ya Ukraine yalikuwa bado yanaendelea kuzuiwa na kwamba mtiririko wa msaada kutoka nchi jirani ulikuwa umekatwa, kauli ambazo hazikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru.

Katika upande wa Ukraine, wakuu wa majeshi wanasema wanajeshi wanaendelea kusonga mbele na wameripotiwa kuchukuwa udhibiti wa vijiji zaidi ya 80 katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,500.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

02:23

This browser does not support the video element.

Hata hivyo waangalizi huru wa kijeshi wanayataja madai hayo kuwa yaliotiwa chumvi na kusema eneo halisi linaweza kuwa nusu ya kile inachodai Ukraine.

Soma pia:Jeshi la Ukraine ladungua droni tano za Urusi

Katika hatua nyingine, Urusi imesema imeharibu makombora 12 yaliotengenezwa nchini Marekani chapa ya ATACM, yaliofyatuliwa na Ukraine kuharibu daraja linoloiunganisha Urusi na rasi ya Crimea, ambayo Moscow iliinyakuwa miaka 10 iliyopita.

Ukraine imesema mara kwa mara kwamba inataka kuharibu daraja hilo mara itakapopata uwezo wa kijeshi, kwa sababu lilijengwa kinyume cha sheria.

Na katika taarifa nyingine, naibu waziri mkuu wa Poland, Krzysztof Gawkowski, amekanusha kuhusika kwa nchi yake katika hujuma dhidi ya bomba la kusafirisha gesi kutoka Urusi kwenda Ujerumani mwaka 2022.

Kauli hiyo imekuja baada ya mkuu wa zamani wa ujasusi wa Ujerumani August Hanning, kuituhumu Poland kwa kushikirikiana na Ukraine katika hujuma hiyo.