1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine waanza uchunguzi wa ajali ya ndege

10 Januari 2020

Maafisa wa Iran na Ukraine wameanza uchunguzi wa ajali ya ndege ya shirika la ndege la Ukraine iliyoanguka karibu na uwanja wa ndege mjini Tehran.

Iran Teheran | Sucharbeiten nach Flugzeugabsturz
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS/R. Fouladi

Kulingana na mamlaka ya safari za anga ya Iran, wachunguzi wa ajali hiyo wanajikita kuchunguza visanduku viwili vyeusi vya kurekodi taarifa za safari ya ndege ambavyo hata hivyo vimeharibika. Aidha wachunguzi kutoka Ukraine kwa upande wao wamekuwa wakizingatia uwezekano wa mazingira ambayo huenda yalisababisha ajali hiyo, ikiwa ni pamoja na iwapo ndege hiyo ilidunguliwa na makobora yanayotengenezwa Urusi aina ya Tor.

Watu wote 176 waliokuwa kwenye ndege hiyo ya Boeing 737 walikufa, huku wengi wa wahanga wakiwa ni raia wa Iran na Canada. Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau amesema ushahidi unahitimisha kwamba ndege hiyo ilidunguliwa na kombora lililorushwa na Iran kutokea ardhini. Iran inakana madai hayo, ikitaka kuwasilishwa ushahidi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesalia katika tahadhari akisema mazingira ya kudunguliwa bado hayajathibitishwa. Iran inasisitiza kwamba ndege hiyo ilianguka kutokana na matatizo ya kiufundi huku Ukraine ikisema huenda ilipata hitilafu ya injini. Mashirika ya ndege ya Ujerumani, Lufthansa na la Norway yamesitisha safari zake na Tehran.

Rais wa ukraine, Volodymyr Zelensky amejiwekea tahadhari kubwaPicha: Imago Images

Kulingana na wizara ya mambo ya kigeni ya Ukraine, Marekani tayari imempatia rais Zelensky taarifa muhimu kabla ya mazungumzo ya simu na waziri wa mambo ya kigeni Mike Pompeo kuhusiana na ajali hiyo. Zelenskiy na waziri wa wizara hiyo Vadymir Prystaiko wamekutana na wawakilishi wa Marekani kupewa taarifa hizo zitakazotumiwa na wachunguzi hao, ingawa waziri huyo hakuelezea aina ya taarifa hizo ama kile kinachoelezewa.

Kiongozi wa juu zaidi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq Ayatollah Ali al-Sistani amelaani mashambulizi ya Marekani na Iran na kuonya kuhusu kuzorota kwa hali ya usalama nchini humo na eneo zima la Mashariki ya Kati. Matamshi haya yalitolewa na mwakilishi wake Ahmed al-Safi kwenye swala ya Ijumaa, kiongozi huyo amesema mashambulizi hayo yalikuwa ni ukiukwaji wa uhuru na kwa maana hiyo hakuna taifa lolote la nje litakaloamua kuhusu mustakabali wa Iraq. Amesema "Iraq inatakiwa kujisimamia yenyewe, kutawaliwa na watu wake. Wageni hawatakiwi kuwa na jukumu la kufanya maamuzi. taifa hili linatakiwa kutawaliwa kulingana na matakwa ya watu wake."

Mjini Washington baraza la wawakilishi limepiga kura ya kumzuia rais Donald Trump kuchukua hatua zaidi za kijeshi nchini Iran.

Katika hatua nyingine, Ujerumani imesema hii leo kwamba bado inataka kuulinda mkataba wa nyuklia wa Iran mwaka 2015, huku ikipingana na mwito wa Marekani wa kuzitaka nchi za Ulaya kuachana na mkataba huo. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Ujerumani Rainer Breul amesema lengo la Ujerumani ni kuulinda mkataba huo kwa sababu bado inaamini kwamba bado ni muhimu katika kuizuia Iran kumiliki silaha za nyuklia.

Matamshi ya Ujerumani yanaungwa mkono na Ufaransa na Uingereza, ambao pia wamesisitiza kuendelea kutekeleza majukumu yao kwenye mkataba huo. Mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya wamekutana mjini Brussels kutafuta njia ya kulegeza hali tete iliyojitokeza wiki iliyopita.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW