1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaadhimisha Siku ya Kitaifa

Admin.WagnerD15 Julai 2026

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, ameungana na viongozi wa Ulaya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Ukraine mjini Kyiv.

Ukraine Kyjiw 2026 | Selenskyj verleiht von der Leyen den Orden Europas
Ukraine Kyjiw 2026 | Selenskyj verleiht von der Leyen den Orden EuropasPicha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Hatua hiyo imekuja wakati vita vya Ukraine na Urusi vikiwa katika mwaka wake wa nne. Ukraine imeadhimisha Siku yake ya Taifa huku mapigano na Urusi yakiendelea na matumaini ya kusitishwa kwa vita yakiwa bado hafifu. Katika maadhimisho hayo, viongozi kutoka mataifa kadhaa ya kusini mashariki mwa Ulaya wamekutana Kyiv kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kuendelea kuiunga mkono Ukraine.

Akiwa katika ziara yake ya kumi na moja nchini humo tangu vita vilipoanza mwaka 2022, Ursula von der Leyen ametangaza ushirikiano mpya kati ya Umoja wa Ulaya na Ukraine wa kutengeneza droni, akisema utachanganya uzoefu wa Ukraine uliopatikana vitani na uwezo wa kiteknolojia na viwanda wa Ulaya.

Ukraine, Kyiv 2026 | Wageni wa Kimataifa katika Siku ya Taifa ya UkrainePicha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Aidha, ametangaza kutolewa kwa euro bilioni moja kutoka mfuko wa Umoja wa Ulaya wa mkopo kwa Ukraine ili kuongeza uzalishaji wa droni na kuimarisha uwezo wa kujilinda."Katika miezi ya hivi karibuni, Ukraine imesaini makubaliano ya ushirikiano wa droni na mataifa kadhaa kutoka Ulaya hadi Mashariki ya Kati. Hii inaonyesha kutambuliwa kwa uzoefu wa kipekee ambao Ukraine imeupata vitani. Kuanzia teknolojia na utengenezaji wa droni, mifumo ya kukabiliana nazo, usambazaji wa vifaa, hadi matumizi ya rada, vituo vya ardhini na ving'amuzi, maarifa hayo yanapaswa kushirikishwa na kutumiwa kwa manufaa ya pamoja."

Umoja wa Ulaya na juhudi za kuimarisha mfumo wa ulinzi wa Ukraine

Von der Leyen amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza uwekezaji katika sekta ya ulinzi na kuiwezesha Ukraine kuimarisha mifumo yake ya ulinzi wa anga kuelekea msimu wa baridi. Katika kipindi hicho, Urusi imekuwa ikishambulia mara kwa mara miundombinu ya umeme na nishati ya Ukraine, hatua ambayo viongozi wa Kyiv wamekuwa wakiitaja kama juhudi za "kugeuza majira ya baridi kuwa silaha."

Katika ziara hiyo, Rais Volodymyr Zelensky pia amemtunuku Von der Leyen Nishani ya Order of Europe, kwa mchango wake katika kuunga mkono safari ya Ukraine kuelekea uanachama wa Umoja wa Ulaya na kusaidia kuimarisha uwezo wa nchi hiyo kujilinda.

Onyo la Urusi kwa mataifa yanayounga mkono Ukraine

Wakati huo huo, Urusi imeonya kuwa haitakubali kikosi chochote cha kijeshi kutoka mataifa yanayoiunga mkono Ukraine kupelekwa nchini humo baada ya makubaliano yoyote ya amani. Moscow imesema hatua hiyo itachukuliwa kuwa tishio kwa usalama wake na kwamba wanajeshi wa kikosi hicho watakuwa malengo halali ya kijeshi.

Siku ya Taifa ya Ukraine huadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Julai kama ishara ya uhuru, mamlaka ya taifa na haki ya wananchi wake kujitawala, wakati nchi hiyo ikiendelea kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa katika vita vinavyoendelea dhidi ya Urusi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW