Ukraine yaanza kuzijaribu ndege za kivita za chapa F-16
5 Agosti 2024Marubani wa Ukraine wameanza kurusha kwa majaribio ndege za kivita chapa F-16kwa operesheni za ndani, kulingana na taarifa iliyotolewa na Rais Volodymyr Zelenskiy.
Kiongozi huyo ametangaza kuanza kutumika kwa ndege hizo, wakati alipokutana na marubani wa kijeshi katika kambi ya anga ambayo haikutajwa eneo lake kwasababu za kiusalama.
Kyiv imekuwa ikisubiri kwa muda mrefu kuwasili kwa ndege hizo za kivita chapa F-16 zilizotengenezwa Marekani, zaidi ya miezi 29 baada ya uvamizi wa Urusi. Naye kamanda wa juu wa Ukraine Oleksandr Syrskyi alisema kuwasili kwa ndege hizo kutaokoa maisha ya askari wa nchi hiyo.
Kuwasili kwa ndege hizo ni hatua muhimu kwa Ukraine, ingawa bado haijafahamika ni ndege ngapi zimepelekwa na zitaweza kusaidia kwa kiwango gani katika kuimarisha ulinzi wa anga na kwenye uwanja wa vita.