1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine yaanza mashambulizi kuyakomboa maeneo yake

Saleh Mwanamilongo
12 Juni 2023

Ukraine imesema kuwa imevikomboa vijiji vitatu kusini-mashariki mwa nchi hiyo katika ushindi wa kwanza wa mashambulizi yake yaliyokuwa yakitarajiwa.

Jeshi la Ukraine ladai kukomboa vijiji vitatu kutoka mikononi mwa jeshi la Urusi
Jeshi la Ukraine ladai kukomboa vijiji vitatu kutoka mikononi mwa jeshi la UrusiPicha: Nicolas Cleuet/Le Pictorium/IMAGO

Picha kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha wanajeshi wa Ukraine wakisherehekea katika makazi jirani ya Blahodatne na Neskuchne katika jimbo la Donetsk. Naibu waziri wa ulinzi wa Kyiv alisema eneo la Makarivka nalo litakombolewa hivi karibuni.

Mafanikio makubwa ya kijeshi ya Ukraine katika eneo la Zaporizhzhia yatawezesha vikosi vyake kushikilia daraja  linalounganisha Urusi na eneo la Crimea, ambayo itakuwa ni pigo kubwa kwa Urusi. Moscow bado haijathibitisha kuanguka kwa kijiji chochote, badala yake inazungumza juu ya kuzima mashambulizi ya Ukraine katika eneo hilo.

Waendesha mshtaka wa jimbo la Kherson wamesema  watu watatu waliuawa na wengine 23 kujeruhiwa Jumapili wakati Urusi iliposhambulia kwa makombora boti ya uokoaji ikiwaondoa raia kutoka eneo linalodhibitiwa na Urusi. Msemaji wa jeshi la Ukraine Valeriy Shershen amesema wamewashika wanajeshi kadhaa wa Urusi na wapiganaji wanaowaunga mkono kufuatia mapigano ya hapo jana Jumapili.

Mashambulizi ya makombora

Juhudi za uokoaji huko Dnieper baada ya bwawa kuharibiwaPicha: AP/picture alliance

Rais Volodymyr Zelensky alithibitisha kwamba mashambulizi ya kukabiliana na Urusi yameanza, huku akiituhumu Urusi kuwashambulia raia wa Ukraine.

''Magaidi wa Urusi wanaendelea kushambulia kwa makombora njia za uokoaji, sehemu za uokoaji, na boti ambazo watu wanaokolewa. Leo, kutokana na moja ya makombora haya, watu 3 wameuawa, rambirambi zangu kwa jamaa na marafiki. Watu wengine walijeruhiwa, ikiwa ni pamoja na polisi wawili.'',alisema Zelensky.

Kwingineko, Ukraine inasema Urusi imelipua bwawa jingine katika eneo la Zaporizhzhia, kufuatia uharibifu wa jengo kuu la Nova Kakhovka siku ya Jumatatu, ambalo lilisababisha mafuriko makubwa.

Maafisa wa Ukraine wanasema watu saba walifariki na watu 35 wakiwemo watoto saba bado hawajulikani walipo kufuatia mafuriko makubwa yaliyotokana na uharibifu wa bwawa hilo. Ukraine na Urusi zinatupiana lawama katika uharibifu wa bwawa hilo.

Urusi na Ukraine zabadilishana wafungwa 

Ukraine yawapokea wafungwa wake wa kivita 95 kutoka UrusiPicha: Coordination Headquarters for the Treatment of Prisoners of War/Handout/REUTER

Huku hayo yakijiri, Ukraine na Urusi walibadilishana wafungwa wa kivita. Mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine, Andriy Yermak amesema kuwa  Kyiv iliwarejesha wanajeshi 95 ambao walikamatwa na Warusi katika vita  vya miji ya Bakhmut na Mariupol na kwa upande wake Urusi iliwapokea wanajeshi wake 90 katika ubadilishaji mpya wa wafungwa.

Katika juhudi za kuisaidia Ukraine, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatarajiwa kukutana leo na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na kiongozi wa Poland Andrzej Duda mjini Paris, Ufaransa kabla ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya kujihami ya  NATO mwezi ujao.

Chanzo: AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW