Ukraine yaapa kutoiachia Urusi hata sentimita moja mashariki
9 Novemba 2022Mkoa wa Donetsk ni moja ya minne ambayo Urusi ilidai kuinyakua mwishoni mwa mwezi Septemba.
Mapigano yamekuwa yakiendelea katika mkoa huo kati ya jeshi la Ukraine na vikosi vinavyoelemea Urusi tangu 2014, mwaka ambao pia Moscow iliinyakua rasi ya Crimea kutoka Ukraine.
Rais Zelenskiy amesema katika ujumbe wa vidio wa usiku, kwamba shughuli za vikosi vya ukaliaji zinasalia kwa kiwango cha juu kabisaa, zikihusisha mashambulizi ya kila siku, lakini pia akaongeza kuwa vikosi hivyo vya Urusi vinakumbwa na hasara kubwa.
"Amri inabaki ile ile - kusonga mbele kuelekea mpaka wa utawala wa mkoa wa Donetsk. Hatutaachia hata sentimita moja ya ardhi yetu," alisema Zelenskiy na kuwashukuru "mashujaa wote wanaosimama kidete kuitetea Donbas."
Soma pia: Ukraine yataja masharti ya kufanya mazungumzo na Moscow
Meya aliewekwa na Urusi katika mji wa Snihurivka, mashariki mwa mji wa kusini wa Mykolaiv, alinukuliwa na shirika la habari la RIA akisema Jumanne kwamba wakaazi waliona vifaru na mapigano makali yalikuwa yanaendelea.
Gavana wa Ukraine wa mkoa wa Mykolaiv Vitaly Kim, ameashiria kwamba vikosi vya Ukraine ayari vimewatimua wanajeshi wa Urusi kutoka eneo hilo, akinukuu kilichoonekana kuwa mazungumzo kati ya wanajeshi wa Urusi.
Kwenye uwanja wa mapigano mkoani Kherson, Zelenskiy amesema vikosi vya Ukraine vilikuwa vinachukuwa hatua kwa usahihi kutokana na uelewa wao wa mipango ya Urusi.
Milioni nne hawana umeme
Zelenskiy pia ameongeza kuwa karibu watu milioni nne walikuwa hawana umeme katika mikoa 14, pamoja na mji mkuu Kyiv siku ya Jumanne, lakini kwa msingi wa udhibiti na siyo dharura.
Soma pia: Ikulu ya Kremlin yakataa kuthibitisha mazungumzo na Marekani
Vikosi vya Ukraine vimekuwa kwenye mashambulizi katika miezi ya karibuni, huku Urusi ikijipanga kutetea maeneo ya Ukraine inayoendelea kuyakalia, baada ya kuwaita mamia ya maelfu ya askari wa akiba katika kipindi mwezi mmoja uliyopita.
Mchambuzi wa kijeshi mwenye makao yake mjini Kyiv, Oleh Zhdanov, alisema Jumanne kwamba wanajeshi 21 wa Urusi walikuwa wamejisalimisha kwa vikosi vya Ukraine karibu na Svatove katika mkoa wa Luhansk.
Ukraine pia imeishtumu Urusi kwa kupora vifaa na kuharibu miundombinu ya nishati na barabara, wakati vinaondoka katika maeneo yanayorejeshwa na Ukraine.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupiga kura wiki ijayo kuhusu azimio linalotambua kwamba Urusi inawajibika kuilipa Ukraine fidia, kutokana na majeraha, ikiwemo uharibifu wowote uliosababishwa na matendo yanayotambuliwa kuwa makosa kimataifa.
Robo tatu ya mataifa 193 wanachama wa Baraza Kuu ya Umoja wa Mataifa yalipiga kura mwezi Machi kulaani uvamizi wa Urusi na kisha tena mwezi Oktoba kulaani jaribio la Moscow kunyakuwa baadhi ya maeneo ya Ukraine.
Chanzo: Mashirika