1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Ukraine yabaini vipuri vya China kwenye silaha za Urusi

Angela Mdungu
24 Septemba 2024

Mshauri wa wa Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine Vladyslav Vlasiuk, amesema asilimia 60 ya vipuri vya silaha zilizopatikana kwenye silaha za Urusi katika uwanja wa mapambano nchini Ukraine, vinatoka China.

Jengo lililoharibiwa na mashambulizi ya Urusi eneo la Donesk , Ukraine
Mashambulizi ya Urusi ndani ya UkrainePicha: Ukraine National Police via AP/picture alliance

Mshauri huyo wa Zelensky ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema hayo yamebainika baada ya baada ya kuzungumza na makampuni kadhaa ya utengenezaji wa silaha.

Ameeleza pia kuwa sehemu muhimu za vifaa vinavyotumiwa katika kuchunguza, droni na makombora pia zimebainika kuwa zilitoka Marekani, Uholanzi, Japan, Uswisi na mataifa mengine ya magharibi.

Licha ya uhusiano mkubwa wa kibiashara kati ya Urusi na China, Beijing imeendelea kukanusha mara kadhaa kuipatia Moscow silaha au vipuri na kuongeza kuwa haihusiki na mzozo wa Ukraine.

Soma zaidi: G7 wahofia vifaa vya kijeshi vya China kwa Urusi

Pamoja na vikwazo vingi ilivyowekewa Urusi baada ya uvamizi wake nchini Ukraine mwaka 2022, Moscow imeendelea kutumia vifaa vyake vya kijeshi vyenye vipuri kutoka mataifa ya Magharibi.

Mshauri wa Zelensky, amesema Umoja wa Ulaya unaweza kufanya juhudi zaidi ili kuzuwia bidhaa za Magharibi kuingia Urusi ikiwemo kuichukulia hatua kampuni ya nyuklia ya Rosatom ambayo Ukraine inaamini imekuwa ikitumia mitandao yake kulipa vifaa jeshi la Urusi.

Wafanyakazi wa zimamoto wakijaribu kuuzima moto uliotokana na mashambulizi ya Urusi nchini UkrainePicha: uncredited/Ukraine Ministry of Internal Affairs/dpa/picture alliance

Mashambulizi yaendelea kuripotiwa ndani ya Ukraine

Wakati hayo yakijiri, mamlaka za Ukraine zimesema leo Jumanne kuwa Urusi imefanya mashambulizi katika mkoa wa Poltava na kuharibu miundombinu ya umeme. Mashambulizi hayo yamesababisha umeme kukatika katika maeneo 20.

Gavana wa Poltava Filip Pronin amesema, mabaki yaliyoanguka kutoka katika droni zilizorushwa yamesababisha uharibifu katika nyumba kadhaa lakini hakuna majeruhi.

Taarifa ya jeshi la Ukraine imesema vikosi vyake vilifanikiwa kuzidungua droni 66 na kushindwa kuzizuia nyingine 13 kati ya droni 81 zilizorushwa kutoka Urusi.

Soma zaidi: Shambulizi la Urusi laua watatu nchini Ukraine

Mamlaka nchini humo zimeeleza zaidi kwamba zimefanikiwa kuzima moto uliozuka kwenye maeneo mawili ya Kyiv. Gavana Ruslan Kravchenko amesema moto huo ulitokana na mashambulizi ya Urusi ya usiku wa kuamkia leo.

Sehemu ya uharibifu uliotokana na mashambulizi ya droni ya Urusi nchini UkrainePicha: National Police of Ukraine in Sumy region/REUTERS

Katika shambulio jingine, watu 16 wamejeruhiwa baada ya Urusi kufanya mashambulizi ya anga katika mji wa Zaporizhzhya.

Majengo 13 yameharibiwa kutokana na mashambulizi hayo. Mji huo uko kilometa 60 kutoka kilipo kinu cha nyuklia cha  Zaporizhzhya.

Hayo yanajiri wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiwa mjini New York anakotarajiwa kuhutubia katika Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mzozo wa Ukraine unatarajiwa kuwa sehemu ya mada zitakazopewa uzito kwenye mkutano huo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW