1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yachukua udhibiti wa eneo la Kyiv kutoka kwa Warusi

3 Aprili 2022

Ukraine imesema imechukua udhibiti wa eneo zima la Kyiv baada ya wanajeshi wa Urusi kurudi nyuma kutoka katika baadhi ya miji muhimu karibu na mji huo mkuu. Kuna hofu ya kutegwa mabomu ya ardhini

Ukraine | Russland-Ukraine Krieg | Ukrainische Soldaten in Bucha
Picha: Zohra Bensemra/REUTERS

Naibu waziri wa ulinzi Ganna Maliar ameandika kwenye ukurasa wa Facebook hapo jana kwamba miji ya Irpin, Bucha, Gostomel na eneo zima la Kyiv imekombolewa kutoka kwa mvamizi.

Soma pia:Miji ya kusini mwa Ukraine yashambuliwa na Urusi

Miji hiyo ilikuwa imeharibiwa vibaya kutokana na mapigano na raia wengi waliuawa. Meya wa miji hiyo amesema watu 280 walizikwa katika kaburi la pamoja katika mji wa Bucha na miili mignine ikiwa imesambaa kwenye mji huo huku mamlaka zikisema karibu watu 200 waliuawa katika mji wa Irpin tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

Vifaru vya Urusi viliharibiwa viungani mwa KyivPicha: Maxym Marusenko/NurPhoto/Picture alliance

Ukraine imesema askari wa Urusi wanaondoka kwenye maeneo ya kaskazini na wanaonekana kujielekeza zaidi upande wa mashariki na kusini mwa Ukraine.

Kwenye ujumbe wake wa video kwa taifa jana usiku, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema wanajeshi wa Ukraine wanaoyakomboa maeneo ya karibu na Kyiv na Cherhiniv hawawaruhusu Warusi kuondoka bila mapambano, lakini "wanawashambulia. Wanamuangamiza wanayeweza." Rais huyo kwa mara nyingine ameomba msaada wa zana za kisasa za kviita kutoka kwa nchi za magharibi kama vile ndege na mifumo ya kuyaharibu makombora.

Timu ya Msalaba Mwekundu haijafika Mariupol

Mapambano ya Moscow yaliyoelekezwa mashariki mwa Ukraine pia yameufanya mji wa kusini mashariki wa Mariupol kuwa uwanja wa vita. Mji huo wa bandari katika Bahari ya Azov upo katika eneo la Donbas kunakozungumzwa Kirusi na wengi, ambako wanaharakati wa kujitenga wanaoungwa mkono na Moscow wamekabiliana na askari wa Ukraine kwa miaka nane.

Timu ya Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu ilitumai kuwahamisha wakaazi wa Mariupol jana Jumamosi lakini haikufika mjini humo. Siku moja kabla, maafisa mjini humo walisema msafara wa shirika hilo ulizuiwa na askari wa Urusi.

Mariupol imezingirwa na wanajeshi wa Urusi kwa zaidi ya mwezi mmoja na kukabiliwa na mashambulizi makali Zaidi katika vita hiyo. Karibu watu 100,000 wanaaminika kubaki mjini humo, kutoka idadi ya watu 430,000 ya kabla ya vita, na wanakabiliwa na uhaba wa maji, chakula, mafuta na dawa.

Rais Zelensky anasema sehemu kubwa ya askari wa Urusi wamedhibitiwa karibu na Mariupol, ambapo walinzi wa mji huo wanaendelea kupambana. "Shukrani kwa upinzani huu, shukrani kwa ujasiri na ustahimilivu wa miji yetu mingine, Ukraine imejipa muda zaidi, muda unaoturuhusu kuzima mbinu za adui wetu na kudhoofisha uwezo wake." Amesema Zelensky.

Mwandishi Habari wa DW Nick Connolly mjini Kyiv anasema Urusi inakabiliwa na shinikizo kubwa la kuhakikisha raia wanatolewa kwa njia salama kutoka Mariupol. "Hii ni habari kubwa kimataifa – inaangaziwa sana, kwamba kuna shinikizo kubwa kwa Urusi kuwezesha hilo,” amesema Connolly.

Karibu watu 10,000 waandamana Uswisi kupinga vitaPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Nakala ya mkataba wa Amani imefikia hatua nzuri – ripoti

Shirika la Habari la Interfax Ukraine limeripoti kuwa Urusi imeonyesha ishara kuwa rasimu ya mkataba wa amani umefikia hatua muhimu. Ikimtaja mjumbe wa Ukraine katika mazungumzo hayo David Arakhamia, shirika hilo limeripoti kuwa mazungumzo yamefikia hatua ya mashauriano ya moja kwa moja.

Arakhamia inaripotiwa kuwa ameiambia televisheni ya Ukraine kuwa Urusi imekubali msimamo wa jumla wa Ukraine isipokuwa tu msimamo wake kuhusu Crimea. Amesema ikiwa Rais wa Urusi Vladmir Putin atakubali kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, huenda mahala pa mkutano huo pakwa ni nchini Uturuki. Arakhamia amesema Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan aliwapigia simu viongozi hao wawili Ijumaanna "kuonekana kuthibitisha kutoka upande wake kuwa wako tayari kupanga mkutano siku chache zijazo.”

Afp, reuters, ap, dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW