1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Ukraine yachukua udhibiti wa mji wa Kherson

11 Novemba 2022

Vikosi vya Ukraine vimetaja kuchukua udhibiti wa maeneo kadhaa yaliyoachwa na Urusi katika mji wa kimkakati wa Kherson huku mapigano makali yakiripotiwa huko Mykolaiv.

Ukraine Armee rückt weiter vor
Picha: Anatolii Stepanov/AFP/Getty Images

Maafisa wa jeshi la Ukraine wamesema wanaendelea kuchukua udhibiti wa maeneo kadhaa yaliyojaa mabomu ya kutegwa ardhini na ambayo yameachwa na Urusi. Mamlaka za nchi hiyo zimebaini kuwa bendera za Ukraine zimerejea mahali pake na kuwa jamii katika maeneo 41 zimekombolewa.

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Oleksii ReznikovPicha: Andre Pain/AFP

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Oleksii Reznikov ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa itachukua angalau wiki moja hadi Urusi kujiondoa moja kwa moja katika mji wa Kherson, kwa kuwa bado kuna wanajeshi wa Urusi wanaokadiriwa kufikia 40,000 katika eneo hilo. Lakini Urusi imethibitisha kuwa imekamilisha zoezi la kuwaondoa wanajeshi wake wote huko Kherson huku ikiendelea kunadi kuwa eneo hilo bado ni sehemu ya Urusi na wala haijutii kitendo cha kuunyakua mji huo.

Jeshi la Ukraine laimarika

Wanajeshi wa Ukraine wakirusha kombora huko KhersonPicha: REUTERS

Hii ni mara ya tatu wanajeshi wa Ukraine kufanikiwa kuwatimua wavamizi wa Urusi. Mara ya kwanza ilikuwa mwezi Machi walipojaribu kuudhibiti mji mkuu Kyiv. Kisha mwezi Septemba, vikosi vya Urusi vilirejeshwa nyuma katika mkoa wa kaskazini mashariki wa Kharkiv.

Soma zaidi:Putin 'sio mshukiwa pekee' katika uhalifu nchini Ukraine 

Hayo ameyakumbushia pia Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy katika hotuba yake kwa taifa jana usiku na kusema ukombozi unaendelea: "Yanayotokea sasa yamepatikana kwa mapigano ya makali ya miezi kadhaa. Yamepatikana kwa ujasiri, maumivu, na hasara. Sio tu kwamba adui anaondoka. Ni Waukraine wanaowatimua wavamizi kwa gharama kubwa. Kama ilivyo kuwa hapo awali mashariki mwa nchi yetu katika mkoa wa Kharkiv, na kaskazini katika mikoa ya Kyiv, Sumy, na Chernigiv. Sasa ni mikoa ya Mykolaiv na Kherson."

Mykolaiv, UkrainePicha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Wakati hayo yakiarifiwa, Watu sita wameuawa mapema leo katika shambulio la kombora la Urusi kwenye jengo la ghorofa kusini mwa Ukraine katika mji wa Mykolaiv. Meya wa mji huo Oleksandr Senkevych amesema vikosi vya uokozi vinaendelea na juhudi za kuwatafuta manusura huku rais Zelenskiy akilitaja shambulio hilo kuwa "jibu la kikatili" la Urusi kutokana mafanikio ya vikosi vyake kwenye uwanja wa mapambano.

Soma zaidi: Urusi yaamuru kuondoa vikosi kutoka mji wa Ukraine wa Kherson

Kushoto: Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akiwa na Jake Sullivan, Mshauri wa usalama wa kitafa wa Marekani walipokutana Kyiv Novemba 4, 2022.Picha: Ukrainian Presidential Press Office/AP Photo/picture alliance

Marekani imesema itatuma dola milioni 400 za ziada kama msaada wa kijeshi kwa Ukraine, huku kukiwa na wasiwasi kuwa msaada wa kifedha unaoelekezwa katika vita dhidi ya Urusi, unaweza kupungua kidogo ikiwa chama cha Republican kitachukua udhibiti wa Baraza la Wawakilishi baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini humo.

Mshauri wa usalama wa kitaifa Jake Sullivan amesema awamu hii mpya ya msaada itajumuisha vifaa muhimu vya ulinzi wa anga. Viongozi wa Ukraine wanashinikiza misaada zaidi ya silaha ili kuitumia vyema fursa hii ya kuvifurusha vikosi vya Urusi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW