Ukraine yadai kupata mafanikio uwanja wa mapambano
15 Juni 2023Ukraine imedai kuwa imepata mafanikio fulani katika uwanja wa vita kupitia kampeni yake ya kujibu mapigo inayolenga kuyarejesha maeneo yote yaliyokamatwa na Urusi tangu kuzuka kwa vita zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Ganna Malyar amearifu kwamba ndani ya muda wa siku 10 zilizopita vikosi vya nchi hiyo vimepiga hatua umbali wa kilometa 3 ndani ya mji wa Bakhmut, ulio kitovu cha mapambano yanayoendelea.
Wakati hayo yakiarifiwa mkuu shirika la kudhibiti nishati ya atomiki duniani, IAEA, Rafael Grossi amekitembelea kinu cha nyuklia cha Zaporizhzia nchini Ukraine ambacho ndiyo kikubwa zaidi barani Ulaya.
Ziara yake imelenga kutathimini kitisho kinachokikabili kinu hicho baada ya kushambuliwa kwa bwawa kubwa la maji la Kakhovka ambalo lilitumika kupooza mitambo ya kinu cha Zaporizhzia.