1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Ukraine yadai kutibua njama ya Urusi kumshambulia Zelensky

8 Mei 2024

Mamlaka za usalama nchini Ukraine zimesema zimebaini njama ya Urusi ya kufanya shambulizi dhidi ya Rais Volodymyr Zelensky na wanasiasa wengine wa nchi hiyo.

 Rais Volodymyr Zelensky
Rais Volodymyr ZelenskyPicha: Gints Ivuskans/AFP

Shirika la Ujasusi la Ukraine, SBU, limesema maafisa wawili kutoka idara ya usalama inayohusika na ulinzi wa rais wamekamatwa kuhusiana na kushiriki mpango wa mashambulizi hayo.

Inaarifiwa maafisa hao walivujisha taarifa za siri kwa idara ya ujasusi ya Urusi kwa ahadi ya malipo ya fedha na wamekuwa wakiandaliwa kufanya hujuma dhidi ya rais Zelensky na maafisa wengine wa serikali ya Ukraine.

Taarifa ya SBU imesema waliokamatwa ni maafisa wenye vyeo vya ukanali. Inafahamika Urusi iliwahi kuwatuma makomandoo wake wa kijeshi kwenye mjini Kyiv kumkamata au kumuua rais Zelensky mwanzoni kabisa mwa uvamizi wa Moscow Februari 2022. Hata hivyo mpango huo ulishindwa.