1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Ukraine yaendelea kuipigania Bakhmut

4 Aprili 2023

Jeshi la anga nchini Ukraine limesema limefanikiwa kuzuia mashambulizi yaliyofanywa na ndege zisizotumia rubani za Urusi usiku mzima wa kuamkia leo. Kulingana na jeshi hilo, jumla ya mashambulizi 17 yalizuiwa.

Krieg in der Ukraine
Picha: Sergey Shestak/AFP

Kulingana na jeshi la anga la nchini Ukraine ndege hizo zisizotumia rubani ni zile zinazotengenezwa nchini Iran za Kamikaze, na 14 miongoni mwa nyingine zilidunguliwa. 

Jeshi la Ukraine aidha limesema kulishuhudiwa milipuko katika eneo la mji wa pwani wa Odessa, ambako mamlaka ziliripoti uharibifu wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na biashara. Kulingana na jeshi la Ukraine karibu mashambulizi 70 pia yalizuiwa na Urusi.

Mapigano bado ni makali katika mji wa Bakhmut ulioko mashariki mwa mkoa wa Donesk, jeshi hilo limesema. mapema, mkuu wa wanamgambo mamluki wa Urusi wa Wagner Yevgeny Prigozhin, alitangaza kulikamata jengo la utawala la mji huo akimaanisha kimsingi mji huo uko chini ya himaya yao, ingawa Kyiv inasema huo ni uwongo mtupu.

Hata hivyo wataalamu wa taasisi ya masomo kuhusu vita ya nchini Marekani ya ISW inayaunga mkono madai ya Prigozhin baada ya kuzichunguza picha kwa kina. Kulingana na wataalamu hao, wanamgambo wa Wagner wanazidi kuingia katikati ya mji huo unaozozaniwa tangu majira ya joto ya mwaka uliopita wakisaidiwa na wanajeshi wa kawaida wa Urusi.

Mpiganaji wa kundi la Wagner akiwa amesimama mbele ya moja ya majengo yaliyoharibiwa huko BakhmutPicha: Valentin Sprinchak/TASS/IMAGO

Soma Zaidi: Urusi yadai kuiteka Bakhmut, mwanablogu wake maarufu auwawa

Mchakato wa kuwaondoa wakazi kwenye mji huo umekuwa mgumu, wakati wanajeshi wa Ukraine wakijaribu kuwaokoa kwa kutumia magari ya kivita, hii ikiwa ni kulingana na wafanyakazi wa kujitolea katika makazi wanakopokelewa wakazi hao. Mmoja ya waliofanikiwa kuondoka Bakhmut aliyetambulishwa kwa jina moja Liudmyla alisema alikuwa akilia njia nzima kwa sababu hakuweza kuondoka na watoto wake wawili ambao walikuwa eneo jingine la Bakhmut.

"Nilipokuwa njiani kwenye gari la kijeshi, nilipiga kelele, nililia kama ng'ombe...njia nzima. Niliwaomba msamaha watoto kwamba nimeondoka, lakini wao walibaki.," alisema mama huyo.

Picha ya midoli inayoashiria watoto wanaodaiwa kutekwa na Urusi kutoka nchini Ukraine.Picha: Nicolas Maeterlinck/AFP

Tukiondoka Bakhmut, huko Moscow, kamishna wa haki za watoto aliyekuwa akituhumiwa kwa uhalifu wa kivita na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya uhalifu, ICC sambamba na rais Vladimir Putin amesema jana kwamba madai hayo ya ICC yalikuwa ya uwongo na yasiyo wazi. ICC ya mjini The Hague ilitoa waranti wa kukamatwa Putin na kamishna huyo wa Urusi, Maria Lvova-Belova kwa kuwahamisha kinyume cha sheria watoto kutoka maeneo ya Ukraine yanayokaliwa na Urusi.

Lvova-Belova ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Moscow kwamba wazazi walitoa idhini ya watoto hao kuchukuliwa kwa ajili ya mustakabali bora ya maisha yao.

Wakati huohuo, kamishna huyo, amesema Urusi imewapokea wakimbizi milioni 5 kutoka mkoa wa Donbass, na miongoni mwao ni watoto 730,000 tangu Februari 2022, ambao wamekwenda nchini humo na wazazi ama walezi wao.

Na huko Brussels, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema China ina wajibu wa kimaadili wa kuchangia katika kuanzisha mchakato wa amani nchini Ukraine na haitakiwi kuunga mkono uvamizi wa Urusi chini Ukraine. Amesema hayo wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergey Lavrov akiyasifu mahusiano baina yao na China. Lavrov amesisitiza kwamba Putin na rais wa China Xi Jinping walifikia makubaliano ya kimkakati wakati alipozuru taifa hilo wiki mbili zilizopita na kuongeza kuwa wako tayari kushirikiana bega kwa bega katia kulinda maslahi ya mataifa hayo mawili.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW