1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaendelea kurejesha maeneo yaliyodhibitiwa na Urusi

12 Septemba 2022

Vikosi vya Ukraine vimeendelea kuyakomboa maeneo yaliyodhibitiwa na wanajeshi wa Urusi, wakati Moscow ikikabiliana na athari za kudhoofishwa nguvu kwa jeshi lake katika eneo la kaskazinimashariki mwa Ukraine.

Ukraine | Wolodymyr Selenskyj
Picha: Sarsenov Daniiar/Ukraine Preside/Planet Pix/ZUMA/picture alliance

Afisa mmoja wa Ukraine amesema mapema leo kwamba vikosi vyake vimefanikiwa kukomboa zaidi ya miji na vijiji 20 hapo jana baada ya Urusi kukiri kwamba itaondoka katika mji wa Izium, ambao ulikuwa ngome yake katika eneo la kaskazinimashariki mwa Ukraine.

Wakati maelfu ya wanajeshi wa Urusi wakiyatelekeza maeneo na kuacha idadi kubwa ya silaha na vifaa vya kijeshi, jana Jumapili walivishambulia kwa makombora vituo vya kusambaza nishati na kusababisha kukatika kwa umeme katika jimbo la Kharkiv na maeneo mengine ya Poltava na Sumy.

Soma Zaidi: Zelensky ayapongeza majeshi yake kuyakomboa maeneo ya kusini

Ukraine ililaani kile ilichokielezea kama ulipizaji kisasi kwa kuwalenga raia ili vikosi vya Urusi visonge mbele. Leo asubuhi, waandishi wa habari wa Reuters waliopo Kharkiv walisema umeme ulikuwa umerejea ingawa maji yalikuwa hayatoki. Moscow inayokana kunuia kuwalenga raia hata hivyo haikutaka kuzungumza chochote.

Soma Zaidi:Ukraine yaanzisha mashambulizi kuyakomboa maeneo ya kusini

Moja ya vifaru vya Urusi vilivyoharibiwa wakati Ukraine ilipokuwa ikiukomboa mji wa Balakliia.Picha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Wizara ya ulinzi ya Uingereza imesema huenda Urusi iliwaagiza wanajeshi wake kuondoka kutoka kwenye maeneo yote ya Kharkiv, magharibi mwa mto Oskil, na kuachana kabisa na eneo hilo lililotumiwa na Urusi kama barabara kuu ya kuingiza vifaa na ambalo limekuwa muhimu sana kwa Urusi katika vita hivyo, hususan, mashariki mwa Ukraine.

Kyiv ambayo tayari imefika Oskil, wakati ilipofanikiwa kurejesha mji wa kimkakati wa Kupiansk juzi Jumamosi, imesema Urusi inazidi kurudi nyuma. Afisa wa jeshi la Ukraine amesema vikosi vya Urusi vimeutelekeza mji wa Svatove katika jimbo la Luhansk, karibu kilomita 20 mashariki mwa Oskil. Hata hivyo, Reuters haikuweza kuthibitisha taarifa hizi.

Mwakilishi wa Urusi kwenye jimbo la Kharkiv Vitaly Ganchev pia amenukuliwa na shirika la habari la Rossiya 24 la Urusi hii leo akisema vikosi vya Urusi na washirika wao walielemewa pakubwa na mashambulizi ya kushtukiza ya Ukraine katika jimbo la Kharkiv wiki iliyopita, ambapo waliyakamata baadhi ya maeneo yaliyodhibitiwa na Urusi hapo kabla. Amekiri hali inazidi kuwa mbaya kila baada ya saa moja na kuongeza kuwa mpaka wa Belgorod, unaopakana na Urusi sasa umefungwa.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akubaliana kufanya mawasiliano na rais wa Urusi Vladimir Putin kuhusu kitisho kwenye kinu cha nyukliaPicha: Ludovic Marin/Pool/AP/picture alliance

Katika hatua nyingine, ikulu ya Kremlin imearifu kwamba jana Jumapili rais wa Urusi Vladimir Putin na Emmanuel Macron wa Ufaransa walizungumza kwa njia ya simu kujadili hali ya usalama katika kinu chaZaporizhzhyia kilichopo Ukraine. Putin alionya kwenye mazungumzo hayo kuhusiana na janga kubwa kutokana na kile alichokitaja mashambulizi ya mara kwa mara ya wanajeshi wa Ukraine kwenye kinu hicho.

Macron kwa upande wake alimwambia Putin kwamba wao ndio wanapaswa kulaumiwa kutokana na kuivamia Ukraine na kuibua kitisho hicho, hii ikiwa ni kulingana na ofisi ya rais Macron, ingawa ilielezwa kwamba hatimaye wakuu hao walielezea utayari wa kufanya mawasiliano yasiyo na mrengo wa kisiasa kuhusiana na suala hilo, wakihusisha pia shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya Atomiki, IAEA.

Soma Zaidi: IAEA kuweka ujumbe wa kudumu katika kinu cha Zaporizhzhia

Mashirika: DW/RTRE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW