1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaendelea kuyakomboa maeneo yake

13 Septemba 2022

Ukraine imeongeza shinikizo kwa wanajeshi wa Urusi wanaoendelea kurudi nyuma katika uwanja wa mapambano katika dhamira ya kuendelea na kasi waliyonayo kwa sasa.

Ukraine-Krieg | Russischer Panzer bei Isjum
Picha: Juan Barreto/AFP

Bendera mpya za Ukraine zenye rangi ya njano na Buluu zilipepea katika majengo marefu zaidi yaliyotelekezwa katika miji iliyoharibiwa karibu na mji wa pili mkubwa wa Ukraine, Kharkiv, wakati wanajeshi wa Ukraine wakikagua vifaru vya Urusi vilivyoteketezwa na kuachwa barabarani.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy katika hotuba yake ya jana usiku alisema vikosi vyake vinaendelea kusonga mbele:

 

Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyyPicha: Ukrainisches Präsidialamt

"Tangu mwanzoni mwa mwezi Septemba hadi leo hii, wanajeshi wetu tayari wamekomboa zaidi ya kilomita 6000 za mraba za eneo la Ukraine, mashariki na kusini. Harakati za askari wetu bado zinaendelea.''

 

Nae Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Hanna Malyar ameliambia leo shirika la habari la Reuters kuwa mapambano bado yanaendelea katika eneo la kaskazini mashariki mwa Ukraine la Kharkiv lakini Vikosi vya Ukraine vinapiga hatua nzuri kwa sababu vina motisha na uendeshaji wake umepangwa vyema. Hata hivyo, madai mengi ya mafanikio ya kijeshi hayakuweza kuthibitishwa kwa uhuru na uwazi.

Soma zaidi: Ukraine yaendelea kurejesha maeneo yaliyodhibitiwa na Urusi

Vikosi vya Urusi vyadhohofika

Kituo cha Urusi kilichoshambuliwa na wanajeshi wa Ukraine Picha: Press service of the Ukrainian Air Assault Forces Command/REUTERS

Idara ya ujasusi ya Uingereza imebaini kuwa, tangu kuanza uvamizi, kikosi muhimu cha Moscow na kinachotegemewa sana na Urusi kama nguvu ya kukabiliana na Jumuiya ya kujihami ya NATO, kimedhohofishwa mno na huenda ikachukua miaka kadhaa kwa Urusi kujenga upya uwezo wake.

Kurudi nyuma kwa vikosi vyake, haikuizuia Urusi kuvishambulia vituo vya Ukraine. Mapema leo, jiji la Lozova katika Mkoa wa Kharkiv lilishambuliwa na kusababisha vifo vya watu watatu na kuwajeruhi wengine tisa, kwa mujibu wa Gavana wa mkoa huo Oleh Syniehubov.

Soma zaidi: Urusi yatangaza kuondoa majeshi yake katika eneo la Kharkiv

Valentin Reznichenko, Gavana wa Mkoa wa Nikopol ambao uko ng'ambo ya Mto Dnieper kutoka Kiwanda cha nyuklia cha Zaporizhzhia, amesema usiku huu wameshambuliwa mara sita, lakini hadi sasa hakuna majeraha yaliyoripotiwa mara moja. Kuendelea kwa mashambulizi kunakiweka kinu kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya katika hali ya hatari. Zelenskyy ameilaumu Urusi kwa kuilenga miundombinu ya nishati katika mashambulizi yake katika siku za hivi karibuni.

Urusi ambayo bado inadhibiti asilimia ishirini ya nchi hiyo imejibu mafanikio ya Ukraine kwa kufanya mashambulizi yaliyolenga miundombinu kadhaa na kusababisha kukatika kwa umeme huko Kharkiv na maeneo mengine.

Vyanzo: (APE,RTRE)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW