1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine yaendeleza mashambulizi Moscow

6 Oktoba 2026

Mapigano kati ya Urusi na Ukraine yameingia hatua mpya baada ya Ukraine kufanya moja ya mashambulizi makubwa zaidi ya ndege zisizo na rubani kuelekea Moscow.

Moscow 2026 |
Moshi mzito umetanda katika kiwanda cha kusafisha mafuta kufuatia kile ambacho mamlaka zinasema ni shambulizi la droni la Ukraine mjini Moscow.Picha: REUTERS

Mamlaka za Urusi zimesema takribani droni 650 zilirushwa usiku kucha, huku mifumo ya ulinzi wa anga ikidaiwa kudungua nyingi kabla hazijafika kwenye malengo yake. Shambulizi hilo limemuua kijana mmoja mwenye umri wa miaka 20 na kujeruhi watu sita katika vitongoji vya Moscow. Vilevile, nyumba kadhaa ziliripotiwa kuharibika.

Mashambulizi hayo yanajiri wakati pande zote mbili zikiongeza mashambulizi ya masafa marefu dhidi ya miundombinu muhimu. Ripoti za mashuhuda zinaeleza kuwa miongoni mwa maeneo yaliyolengwa ni kituo cha uzalishaji wa mafuta karibu na Moscow. Ukraine imekuwa ikiyalenga mara kwa mara maeneo ya nishati ya Urusi kwa lengo la kudhoofisha mapato yanayotumika kufadhili vita.

Wakati huo huo, mashambulizi ya Urusi ndani ya Ukraine yanaendelea kusababisha madhara makubwa. Katika mji wa Kharkiv mashariki mwa Ukraine, mabomu ya anga yaliwaua watu sita na kujeruhi zaidi ya hamsini, huku operesheni za uokoaji zikiendelea kwenye majengo yaliyoporomoka.

Zelensky ahimiza mazungumzo

Licha ya kuongezeka kwa mashambulizi, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema bado ana matumaini ya mazungumzo.

Rais Zelensky asema Ukraine iko tayari kwa mazungumzo kinachohitajika ni utayari wa Urusi.Picha: Antti Aimo-Koivisto/Lehtikuva/picture alliance

Zelensky amesema anatarajia Marekani kusaidia kuratibu mkutano wa pande tatu mwezi Oktoba kwa lengo la kusaka suluhisho la kumaliza vita.

"Bila shaka, tunatumia kila njia inayowezekana kuongeza juhudi za kidiplomasia. Natarajia kwamba mwezi Oktoba,  Marekani utaweza kuandaa mkutano wa pande tatu. Timu yetu iko tayari kwa mkutano huo. Kinachohitajika sasa ni utayari kutoka upande wa Urusi. Diplomasia nayo inapaswa kuwa moja ya vipaumbele vya Urusi. Hadi sasa, wamejikita tu katika kufanya mashambulizi dhidi ya Ukraine na shughuli za kuyumbisha utulivu barani Ulaya.”

Katika hatua nyengine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, ameonya kuwa Urusi huenda ina malengo yanayozidi mipaka ya Ukraine. Wadephul amesema kauli za Rais Vladimir Putin za zamani kuhusu kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti zinaibua wasiwasi kwamba Moscow inaweza kuwa na nia ya kurejesha ushawishi wake katika baadhi ya mataifa jirani.

Amesema nchi kama Georgia, Moldova pamoja na mataifa ya Baltiki yanapaswa kuwa macho. Kwa mujibu wa waziri huyo, kwa kuwa mataifa ya Baltiki ni wanachama wa NATO, tishio lolote dhidi yao lingehusisha pia washirika wote wa muungano huo, wakiwemo Ujerumani.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW