1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaiomba Ujerumani silaha za kujilinda dhidi ya Urusi

5 Februari 2022

Tofauti na washirika wake wa NATO, Uingereza na Marekani, Ujerumani imekataa kuipatia Ukraine silaha kuisaidia kujilinda katika uwezekano wa uvamizi wa Urusi. Kyiv inaitaka Berlin kubadili sera hiyo na kutuma silaha.

Ukrainische Soldaten
Uingereza inasema imeipatia Ukraine silaha 2,000 za kushambulia vifaru, Kyiv inataka Ujerumani pia iipe sialaha.Picha: Pavlo Palamarchuk/AP/dpa/picture alliance

Ukraine imtuma ombirasmi kwa serikali ya Ujerumani kwa ajili ya msaada wa "silaha za kujihami", kwa mujibu wa ripoti ya gazeti.

Katika barua iliyonukuliwa na gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung, ubalozi wa Ukraine umeiomba Berlin kutoa jibu la haraka, kutokana na hali tete ya kiusalama na kitisho cha uvamizi wa Urusi.

Moscow imepeleka maelfu ya wanajeshi kwenye mpaka wa Ukraine, na kusababisha hofu kwamba inapanga kumvamia jirani yake huyo mdogo. Jumuiya ya kujihami ya mataifa ya magharibi NATO, pia imeonya juu ya idadi kubwa ya wanajeshi wa Urusi wanaopelekwa nchini Belarus.

Urusi inakanusha kupanga uvamizi. Imedai uhakikisho kadhaa wa kiusalama kutoka mataifa ya magharibi, ikiwemo kwamba Ukraine kamwe haitajiunga na NATO na kwamba muungano huo wa kijeshi uondoe vikosi vyake kutoka eneo la Ulaya Mashariki.

Soma pia: Urusi na Belarus zajiandaa kwa luteka kubwa ya kijeshi

Katika kujibu matakwa ya Urusi, NATO na Marekani zimesema madai yote mawili hayana mashiko na badala yake zimependekeza mazungumzo zaidi kuhusu makombora na kupunguza kwa wanajeshi.

Wanajeshi wa Ukraine wakiwa katika uwanja wa mazoezi, Feruari 03, 2022.Picha: Pavlo Palamarchuk/AP/dpa/picture alliance

Katika barua iliyonukuliwa na Süddeutsche Zeitung, Ukraine inatoa maombo kadhaa makhsusi ya vifaa vya kujilinda, ikiwemo mifumo ya makombora ya masafa ya kati ya kudungua ndege, bunduki za kudungua ndege zisizotumia rubani, kamera za uchunguzi, mifumo ya ufuatiliaji ya kielektroniki, vifaa vya kuona usiku na risasi.

Kyiv inatafuta "msaada wa mara moja katika upatikanaji wa haraka wa mifumo ya silaha za aina ya kujihami," inasema barua hiyo, kwa mujibu wa gazeti la Süddeutsche Zeitung.

Ujerumani yaondoa uwezekano ya kutoa silaha

Washirika wa NATO, Marekani, Uingereza na mataifa ya Baltic yametuma silaha nchini Ukraine. Lakini Ujerumani imeweka wazi kwamba haitofuata mkondo huo. Mpaka sasa, Berlin imetoa kofia 5,000 za kujihami na imesema inapendelea suluhisho la kidiplomasia.

Serikali ya Ujerumani, inayoundwa na chama cha siasa za mrengo wa kati-kushoto cha SPD, chama cha watetezi wa mazingira cha die Grüne, na kile kinachoegemea biashara cha Free Democrats, FDP,  ina sera kali ya uuzaji wa silaha ambayo hairuhusu kuuza silaha katika maeneo yenye mizozo.

Soma pia: Marekani, NATO watoa jibu la maandishi kwa masharti ya Urusi

Sera sawa na hiyo ilikuwepo chini ya muungano uliyopita ulioongozwa na Angela Merkel. Lakini pamoja na hayo, mwaka 2021 ulishuhudia rekodi ya mauzo ya silaha zenye thamani ya euro bilioni 9.35, sawa na dola bilioni 10.65. Lakini kumekuwa na miito ya kupitia upya sera ya mauzo ya silaha ya Ujerumani.

"Tufungue mjadala juu ya iwapo Ujerumani inapaswa kubadili msimamo huu," Viola von Cramon, mbunge wa bunge la Ulaya kutoka chama cha Kijani na makamu mwenyekiti wa ujumbe wa bunge hilo nchini Ukraine, aliiambia DW.

Alisema pia Ujerumani inapaswa kuchukuwa msimamo mkali zaidi kuelekea Urusi, na kuelezea wasiwasi kuhusu pendekezo la Uturuki kuwa mpatanishi kati ya Moscow na Kyiv.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akiwa katika mkutano na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, mjini Kyiv, Februari 03,2022.Picha: Ukrainian Presidential Press Service/REUTERS

"Nina wasiwasi zaidi kwamba mwishowe, kiongozi muimla, asiefuata demokrasia kama (Rais wa Uturuki Recep Tayyip) Erdogan, atapata ushawishi zaidi katika kanda hii, nchini Ukraine, kuliko sisi Waulaya," alisema. "Ni wazi kabisaa kwamba hii ni katika maslahi yetu kuibakisha Ukraine kwenye njia ya kujiunga na upande wa magharibi.

Mkakati pacha Ukraine

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz wiki hii alitetea uamuzi wa kutopeleka silaha Ukraine na kusema serikali yake ilikuwa inafuata mkakati pacha: kuahidi vikwazo vikali dhidi ya Urusi iwapo itaivamia Ukraine na kupendekeza mazungumzi juu ya njia za kutuliza hali.

Soma pia: Biden: Urusi itaivamia Ukraine

Alexander Graf Lambsdorf, naibu na mwenyekiti wa kundi la wabunge wa chama cha FDP katika bunge la Ujerumani Bundestag, aliiambia DW kuwa mauzo ya silaha hayataleta tofauti kubwa.

"Tuna hali ambamo vikosi vya jeshi la Ukraine ni dhalili kijeshi mbele ya vikosi vya jeshi la Urusi kwa kiwango ambacho hakiwezi kujazwa na utoaji wa silaha," alisema.

Watoto nchini Ukraine wahofia kifo

01:50

This browser does not support the video element.

"Tumetoa msaada kwa ajili ya ulinzi wao wa mtandaoni, tumetoa mafunzo ya kijeshi kwa maafisa kutoka vikosi vya jeshi la Ukraine, tumetuma hospitali ya wazi nchini Ukraine, tunaisaidia nchi hiyo kiuchumi na kisiasa, hivyo kuna njia kadhaa ambamo Ujerumani inaisaidia Ukraine, ukamilifu wake, na mamlaka yake ya kisiasa," alisema.

Soma pia: Marekani yaipa Ukraine dola milioni 200 kuimarisha ulinzi wake

Nchini Ujerumani, asilimia 71 ya watu wamesema wanapinga kutoa silaha za Ujerumani kwa Ukraine na asilimia 20 wanaunga mkono, kwa mujibu wa uchunguzi wa Infratest dimap uliofanywa kwa niaba ya shirika la utangazaji wa umma la ARD na kuchapishwa siku ya Alhamisi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock anatarajia kusafiri kwenda Ukraine wiki ijayo, wakati kansela Olaf Scholz ataelekea huko baadae mwezi huu,  baada ya kumtembelea rais wa Marekani Joe Biden wiki ijayo.

Chanzo: AFP,DPA

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW