Ukraine yaishambulia Urusi kwa mamia ya droni
25 Machi 2026
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema Jumatano kwamba Ukraine imerusha mamia ya ndege zisizo na rubani ikiyalenga maeneo nchini Urusi usiku kucha, katika kile kilichoelezwa kuwa shambulio kubwa zaidi la ndege zisizo na rubani za Ukraine tangu vita vilipoanza. Wizara hiyo imesema jumla ya ndege zisizo na rubani 398 za masafa marefu zilizuiliwa katika maeneo tofauti ya Urusi.
Maafisa wa Urusi wamethibitisha kwamba moto umezuka katika bandari ya Ust-Luga, eneo muhimu la usafirishaji wa mafuta na gesi katika bahari ya Baltic, takriban kilomita 100 kutoka mji wa St Petersburg. Hakuna mtu aliyejeruhiwa. Majengo yaliharibiwa katika kisiwa cha Baltic cha Kotlin, ambacho ni makao ya kambi muhimu ya meli za jeshi la majini la Urusi katika bahari ya Baltic.
Watu wasiopungua 13 walijeruhiwa siku ya Jumanne baada ya jengo la ghorofa kulengwa katika shambulio la mchana katikati ya jiji la magharibi la Lviv nchini Ukraine, karibu na mpaka wa Poland, kulingana na maafisa wa kikanda. Waziri mkuu Yulia Svyrydenko alisema shambulio hilo lilichoma moto jengo lililounganishwa na kanisa la Mtakatifu Andrew la karne ya 17 la jiji hilo, ambalo ni sehemu ya eneo la turathi za dunia za Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO.
Meya wa Lviv, Andriy Sadovy, ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba shambulizi hilo lililenga eneo la katikati ya jiji.
"Sijawahi kuona kitu kama hiki katika kumbukumbu yangu, kwa sababu hayo yalikuwa mashambulizi yaliyolengwa kwenye majengo ya makazi leo na mashambulizi yaliyolengwa katikati ya Lviv - ni eneo la UNESCO. Hawakupiga risasi hapa wakati kulipokuwa na Wajerumani, wakati kulipokuwa na wapiganaji wa bunduki, kila mtu alijaribu kuilinda. Lakini kama unavyoona, Warusi hawana kitu kitakatifu, wanashambulia. Nadhani tunapaswa kuuambia ulimwengu wote kuhusu jambo hili leo."
Mashambulizi ya Ukraine yakata umeme eneo la Belgorod
Wakati huo huo, karibu watu nusu milioni waliachwa bila umeme katika eneo la Belgorod nchini Urusi baada ya mashambulio ya Ukraine kuathiri miundombinu ya nishati. Gavana wa eneo hilo Vyacheslav Gladkov alisema kukatika kwa umeme kuliathiri takriban watu 450,000 katika wilaya kadhaa, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa eneo la Belgorod, huku wakazi wengi pia wakikabiliwa na usumbufu wa kupasha joto na usambazaji wa maji.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema mfumo wa ulinzi wa anga wa Urusi umeangusha ndege zisizo na rubani 389 za Ukraine zilizokuwa zikiingia, katika shambulio kubwa zaidi lililoripotiwa usiku kucha katika maeneo ya Urusi na Crimea tangu vikosi vya Moscow vilipoivamia Ukraine zaidi ya miaka minne iliyopita.
Ndege hizo zisizo na rubani zilisimamishwa katika maeneo 13 ya Urusi pamoja na Rasi ya Crimea, ambayo Urusi iliichukua kinyume cha sheria kutoka Ukraine mwaka wa 2014.
Alexander Drozdenko, gavana wa mkoa wa Leningrad kaskazini mwa Moscow, amesema ndege zisizo na rubani 56 zilipigwa risasi, na moto ukazuka katika bandari ya bahari ya Baltic ya Ust-Luga kutokana na shambulio la Ukraine.
Vikosi vya Ukraine pia vilifanya shambulio la kombora katika eneo la Belgorod kwenye mpaka na Ukraine usiku kucha, na kuharibu miundombinu ya nishati. Gavana wa eneo hilo Vyacheslav Gladkov alisema umeme, maji na vifaa vya kupasha joto vilivurugwa.
Uokoaji wa shirika la OSCE wawahatarisha wafanyakazi wake Ukraine
Wakati haya yakiarifiwa, ripoti ya siri kuhusu harakati ya uokoaji wa shirika la usalama na ushirikiano la Ulaya OSCE wa wachunguzi wake kutoka Ukraine ambao ulifanywa bila mpangilio baada ya Urusi kuvamia miaka minne iliyopita inaashiria jinsi ilivyowaweka wafanyakazi hao katika hatari kubwa ya usalama. Shirika la habari la AFP limefichua ripoti hiyo, huku shirika hilo likijitahidi kutuma ujumbe nchini Ukraine kufuatilia usitishaji wowote wa mapigano.
Uchunguzi wa ndani ulioonekana na AFP unakosoa maandalizi ambayo hayakukamilika wala kutosha ya shirika hilo na ukosefu wa tathmini ya kuaminika kuhusu usalama na mpango madhabuti wa uokoaji uliozingatia taarifa za hali halisi katika uwanja wa vita wa kuwaondoa nchini humo.