Ukraine yaitaka Marekani kuishinikiza Urusi kumaliza vita
8 Aprili 2026
Serikali ya Ukraine inaitaka Marekani kuongeza shinikizo dhidi ya Urusi ili kusitishwa kwa mapigano na kumaliza vita vinavyoendelea nchini humo.Ukraine imesema kuwa, makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran yanaonyesha kuwa uamuzi thabiti wa Washington unaweza kuleta matokeo chanya kuishinikiza Urusi kumaliza vita Ukraine.
Katika chapisho lake kupitia mitandao ya kijamii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andriy Sybiga, alisema kuwa ni wakati muafaka kwa Marekani kutumia nafasi yake kama ilivyofanya Iran, kulishinikiza taifa la Urusi kusitisha mapigano yanayoendelea.Ukraine imekuwa ikiomba msaada wa kimataifa ili kumaliza vita hivyo ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya raia na kuharibu miundombinu.”Uamuzi wa Marekani unafanya kazi. Tunaamini kuwa sasa ni wakati wa kuwa na uamuzi wa kutosha kuilazimisha Moscow kusitisha mapigano na kumaliza vita vyake dhidi ya Ukraine,” alisema.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kwa upande mwingine, ameiluamu Urusi kwa kuendelea kufanya mashambulizi ya makusudi dhidi ya raia.
Rais huyo amesema anaunga mkono makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran na kwamba,Ukraine iko tayari kuchukua hatua sawia endapo Urusi itasitisha mashambulizi yake.Kiongozi huyo pia amefafanua kwamba, Ukraine imekuwa ikihimiza mara kwa mara kusitishwa kwa vita vinavyoendeshwa na Urusi dhidi ya taifa lake na wananchi wake barani Ulaya, na kwamba inaunga mkono juhudi za kidiplomasia katika Mashariki ya Kati na eneo pana la Ghuba.
Haya yanajiri wakati, mashambulizi ya mizinga na ya anga yaliyofanywa na Urusi yakiwaua watu tisa nchini Ukraine katika mashambulizi yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo jana Jumanne.
Mashambulizi hayo yalitokea wakati Moscow ikidai kuwa droni ya Ukraine iliishambulia nyumba moja nchini Urusi, na kusababisha kifo cha mtoto pamoja na wazazi wake. Uvamiaji wa Urusi dhidi ya Ukraine, ulioanza zaidi ya miaka minne iliyopita, umesababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni kuyahama makazi yao.
Katika miezi ya hivi karibuni, pande zote mbili zimeongeza mashambulizi ya masafa marefu kwa kutumia droni na makombora, yakilenga zaidi miundombinu ya nishati. Urusi inalenga kudhoofisha azma ya Ukraine, huku Kyiv kwa upande wake,ikilenga kupunguza mapato ya sekta ya nishati ya Urusi.
Katika mji wa Kherson kusini mwa Ukraine, ambao awali ulitekwa na Urusi kabla ya kukombolewa mwaka 2022, mashambulizi ya mizinga yaliripotiwa kuua watu wanne na kuwaacha wengine kadhaa na majeraha.Akizungumzia hali hiyo, afisa wa eneo la Kherson, Oleksandr Prokudin, alielezea mashambulizi hayo kuwa mabaya zaidi na kuonyesha picha za waathiriwa.
Mashambulizi ya Kherson yalitokea saa chache tu baada ya shambulizi la droni lakulipiga basi la abiria katika mji wa Nikopol, na kuua watu wanne.
Hata hivyo,amesema,vikosi vya kijeshi kutoka Ukraine zinazoisaidia nchi za Mashariki ya Kati kukabiliana na mashambulizi ya droni za Iran zitaendelea kubaki katika eneo hilo, licha ya Marekani na Iran kukubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa wiki mbili.
Yote haya yakiendelea,Urusi imeishambulia bandari kubwa zaidi ya Ukraine kwenye Mto Danube,Izmail usiku wa kuamkia leo.