1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yajaribu kuukomboa mji wa Kherson

27 Oktoba 2022

Vikosi vya Ukraine vimeyashambulia maeneo yanayodhibitiwa na Urusi kwenye mji wa kusini wa Kherson katika wakati Moscow inaendelea kuwahamisha maelfu ya wakaazi wa mji huo baada ya mapigano kuchachamaa.

Angriff an Lviv Ukraine
Picha: Pavlo Palamarchuk/ZumaPress/picture alliance

Duru kutoka uwanja wa vita zinasema vikosi vya Ukraine vinasonga mbele kwenye mji wa Kherson na vinauzingira mji huo kutokea upande wa magharibi na kuzishambulia ngome za jeshi la Urusi katika ukingo wa magharibi mwa mto Dnieper unaoutenganisha mji wa Kherson na upande mwingine wa Ukraine.

Ukraine imezidisha mashambulizi yake ikilenga kulikomboa jimbo la Kherson na mji wake mkuu unaoitwa pia Kherson maeneo ambayo yalikamatwa na Urusi katika siku za mwanzo za uvamizi wa Moscow nchini humo Ukraine.

Picha: Dmitry Marmyshev/TASS/IMAGO

Zaidi ya waakazi 70,000 wa mji wa Kherson wamehamishwa katika siku za hivi karibuni. Hayo ni kulingana na gavana wa mji huo aliyewekwa madarakani na Urusi Vladimir Saldo.

Miongoni mwa waliohamishwa ni pamoja na viongozi wa mkoa huo wanaoungwa mkono na Urusi. Wengi wanaohamishwa wanapelekwa kwenye miji jirani inayodhibitiwa na Urusi.

Katika zoezi hilo masanamu ya mashujaa wa Urusi pia yameondolewa ikiwemo lile la Grigory Potemkin, jenerali wa zamani wa kirusi aliyeuasisi mji wa Kherson mnamo karne ya 18.

Vikosi vya Urusi vyasonga mbele huko Donetsk 

Wakati vikosi vya Ukraine vinasonga mbele huko Kherson, jeshi la Urusi limezidisha hujuma zake mashariki mwa Ukraine kwa kuushambulia kwa makombora mji wa Bakhmut ulio kwenye mkoa wa Donetsk.

Picha: privat

Taarifa zinasema vikosi vya Urusi vimepata mafanikio fulani na kusonga mbele kuelekea katikati mwa mji huo. Wakati hayo yakijiri maafisa wa urusi wamezidisha vitisho kwa kuyaonya mataifa ya magharibi kuwa yanaweza kujumuishwa kwenye mzozo unaoendelea.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi Maria Zakharova amesema kadri Marekani inavyoendelea kuisaidia Ukraine kwenye uwanja wa vita ndiyo kitisho kinaongezeka cha kutokea makabiliano ya kijeshi baina ya madola hayo mawili yenye nguvu za nyuklia.

Matamshi yake yanafuatia yale ya afisa mwingine wa Urusi aliyeonya kwamba Urusi huenda iitazilenga satelaiti za kampuni za Marekani na washirika wake iwapo zitatumika katika vita nchini Ukraine. 

Afisa huyo Konstantin Vorontsov, ameyaelezea matumizi ya kijeshi ya satelaiti za kampuni za biashara za Marekani na mataifa mengine ya magharibi katika mapigano nchini Ukraine kuwa jambo "hatari sana".

Hujuma dhidi ya miundombinu umeme zaendelea 

Picha: EPA-EFE/TELEGRAM/V ZELENSKIY OFFICIAL HA

Kwengineko nchini humo, hujuma dhidi ya miundombinu ya nishati zimeendelea kufanywa na vikosi vya Urusi.

Mapema leo Alhamisi Gavana wa mkoa uliko mji mkuu wa Ukraine, Kyiv alisema makombora ya Urusi yalikilenga kituo kimoja cha nishati na kusababisha uharibifu mkubwa. Hujuma hizo zimezidisha wasiwasi nchini Ukraine katika wakati msimu wa baridi unakaribia.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy  amesema hadi sasa mashambulizi ya Urusi yameharibu asilimia 30 ya miundombinu ya nishati nchini Ukraine.

Katika kile kinachoonekana kuwa kisa cha kujibu mapigo, kituo cha umeme kwenye rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Urusi kutoka Ukraine mwaka 2014, kilishambuliwa usiku wa kuamkia leo.

Gavana wa mji mkuu wa Crimea, Sevastopol,  Mikhail Razvozhayev amesema shambulizi hilo la ndege isiyo na rubani ilisababisha uharibifu mdogo na huduma ya umeme haikutatizika.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW