Ukraine yakanusha kubadili mkakati wa mashambulizi
11 Aprili 2023Mkuu wa kundi la mamluki la Urusi Wagner, Yevgeny Prigozhin, amesema kwa sasa wanadhibiti asilimia 80 ya mji wa Bakhmut ingawa awali mkuu wa eneo la Donetsk Denis Pushilin alikuwa amedai kwamba ni asilimia 75 ya mji huo uliozingirwa ndio ulioko chini ya udhibiti wa Urusi.
Urusi vile vile imesema kwamba imeharibu hifadhi ya mafuta ya tani 70,000 karibu na mji wa kusini mashariki wa Zaporizhzhia. Pushilin lakini ameonya kuwa bado ni mapema mno kuzungumzia kuanguka kwa mji wa Bakhmut.
Ukraine yabadili mipango ya mashambulizi yake
Haya yote yanafanyika wakati ambapo Ukraine na Urusi zimefanya zoezi la kubadilishana wafungwa, Ukraine ikiwaachilia huru mahabusu 106 wa Urusi na Urusi nayo ikiwaweka huru wafungwa 100 wa Ukraine. Hatua hii imethibitishwa na Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine.
"Leo hii kuna habari nzuri kutoka kwa kikosi chetu, tumefanikiwa kuwarudisha nyumbani watetezi wengine 100, wanaume 80 na wanawake 20. Hawa ni wanajeshi, walinzi wa mpakani, wanajeshi wa jeshi la nchi kavu na angani na walinzi wa kitaifa. Miongoni mwao vile vile ni walinzi wa Azovstal. Hizi ni familia 100 zilizokuwa na furaha ya kikweli kabla Pasaka. Na bila shaka tunaendelea kufanya kazi pamoja kuwarudisha watu wetu wote waliotekwa nyara na Urusi," alisema Zelenskiy.
Huku hayo yakiarifiwa shirika la habari nchini Marekani CNN limeripoti kwamba Ukraine imelazimika kuipangua baadhi ya mipango yake ya kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi kutokana na kuvuja kwa nyaraka za siri za Marekani.
Kulingana na gazeti la Washington Post, Marekani ina mashaka iwapo mpango wa Ukraine wa kulipiza kisasi utawanufaisha katika mapambano yao dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Ukraine na Magharibi wanasajili vijana wafanye mashambulizi Urusi
Gazeti hilo linaripoti kuwa Marekani inahisi kuwa Ukraine haitoweza kuyarudisha katika himaya yake maeneo yaliyonyakuliwa na Urusi ifikiapo kipindi cha machipuko, kutokana na changamoto za kukusanya silaha, vifaa na majeshi.
Haya yanajiri wakati ambapo ikulu ya Kremlin imesema kuwa mwandishi wa jarida la Wall Street Evan Gershkovich alikiuka sheria za Urusi na alishikwa waziwazi kwenye kitendo, wakati ambapo Marekani ilisema kuwa amezuiliwa kimakosa na Urusi.
Aidha mkuu wa huduma za usalama Urusi FSB ameishutumu Ukraine na nchi za Magharibi kwa kuwasajili vijana wa Urusi kufanya mashambulizi nchini mwao. Tuhuma hizo za mkuu huyo wa usalama Urusi Alexander Bortnikov zinakuja wiki moja baada ya Rais Vladimir Putin kutoa shutuma sawa na hizo.
Chanzo: AFP/DPAE