1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Ukraine yakanusha kuhusika kulipua bomba la Nord Stream 2

15 Agosti 2024

Ukraine leo imekanusha kuhusika na mashambulizi yaliyoharibu bomba kubwa la kusafirisha gesi kutoka Urusi kwenda Ulaya la Nord Stream 2.

Nord Stream 2 | Milipuko| Urusi| Ukraine
Gesi ikivuja baada ya kulipuliwa kwa sehemu ya bomba la gesi la Nord Stream 2, Septemba, 2022.Picha: NDR

Afisa wa ngazi ya juu wa Ukraine Mykhailo Podolyak ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba nchi yake haikuwa na dhima yoyote kwenye milipuko iliyotokea Septemba 2022 iliyoharibu bomba la gesi la Nord Stream 2.

Podolyak ambaye ni mshauri wa rais wa Ukraine badala yake ameiinyooshea kidole cha lawama Urusi akisema kitendo hicho kingeweza kufanywa na upande ulio na uwezo mkubwa wa kiufundi na kifedha. Na kwa maelezo yake Urusi ndiyo ilikuwa na sifa zote hizo, na kwa hivyo ndiyo ilihusika.

Mashambulizi kadhaa yaliyolilenga bomba hilo na jingine la Nord Stream 1 yanayosafirisha gesi kutokea Urusi hadi Ujerumani yalitokea kiasi miezi saba baada ya Urusi kuivamia kijeshi Ukraine. 

Ukraine yajaribu kujitenga na tuhuma baada ya kuhusishwa 

Matamshi ya Podolyak yanafuatia ripoti kadhaa zilizotolewa siku za hivi karibuni zinazoihusisha Ukraine na hujuma zilizoulenga mtandao huo wa bomba la kusafirisha gesi wa kupitia chini ya Bahari ya Baltiki ambao ujenzi wake uligharimu mabilioni ya dola.

Sehemu ya bomba la Nord Stream 2 upande wa Ujerumani.Picha: Fabrizio Bensch/REUTERS

Ijumaa iliyopita jarida la Marekani la Wall Street liliripoti kuwa maafisa wa ngazi ya juu wa Ukraine walihusika na kilichotokea.

Jumatano ya wiki hiyo hiyo, waendesha mashtaka nchini Poland walisema walipokea waranti ulitolewa na Ujerumani wa kumkamata raia wa Ukraine anayehusishwa na shambulizi la bomba la Nord Stream 2.

Hata hivyo wakati msako umeanzishwa mwanaume huyo aliyetambulishwa kwa majina ya Volodymyr Z alikuwa amekwishaondoka Poland.

Kwenye utetezi wake Podolyak amesema Ukraine haikushiriki kwa lolote kwenye mashambulizi dhidi ya Nord Stream 2 na kuongeza kwamba nchi yake haikunufaika chochote kutokana na uharibifu uliotokea.

Uchunguzi wa Sweden wanaonesha mashambulizi yalikuwa ya kudhamiria

Rais Vladmir Putin wa Urusi aliyalaumu mataifa ya magharibi kuhusika na milupiko ya Nord Stream 2.Picha: Valery Sharifulin/AP/picture alliance

Uharibifu wa bomba hilo ulifuatiwa na miezi kadhaa ya kutupiana lawama kati ya Urusi na mataifa ya magharibi, kwa kila upande kuutuhumu mwingine kuhusika na hujuma hiyo.

Urusi ilikwishazilaumu bila kificho Marekani, Uingereza na Ukraine kwa milipuko hiyo ikisema ilikuwa ni kwa dhamira ya kutatiza usambazaji wa gesi ya Urusi kulifikia soko la Ulaya. Nchi zote tatuzilikanusha madai hayo.

Ujerumani, Denmark na Sweden zilifungua uchunguzi wa mkasa huo na wachunguzi wa Sweden walibaini ushahidi wa vilipuzi kwenye mabaki ya sehemu ya bomba iliyoharibiwa.

Uchunguzi wao ulihitimisha kitendo hicho kilifanywa kwa makusudi.

Mapambano yaendelea Ukraine na Urusi baada ya uvamizi wa mkoa wa Kursk

Mabomu kwenye uwanja wa mapambano Kursk.Picha: ROMAN PILIPEY/AFP

Wakati hayo yakiripotiwa, Urusi imeendelea kupambana kuvidhibiti vikosi vya Ukraine vilivyovuka mpaka na kuingia kwenye mkoa wa mpakani upande wa Urusi wa Kursk.

Inaarifiwa Moscow imetoa amri nyingine ya kuhamishwa maelfu ya watu kutoka mkoa huo kuwaepusha na maafa ya mapigano yanayoendelea.

Gavana wa mkoa huo Alexey Smirnov amewarai wakaazi wa wilaya ya Glushkovsky kujiandaa kuhamishwa kutokana na kitisho kinachoongezeka cha mashambulizi ya makombora ya vikosi vya Ukraine.

Kwa upande wake Ukraine inayosema imechukua udhibiti wa karibu kilometa za mraba 1,000 za ardhi ya Urusi imesema haioni dalili za jeshi la Urusi kudhoofika katika pande zote za uwanja wa vita.

Imesema licha ya uvamizi wa Kursk, Moscow imeendelea kufanya mashambulizi kwenye maeneo yote ya mstari wa mbele katika ardhi ya Ukraine na haijahamisha vikosi vyake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW