1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine yakiri kushambulia daraja la Crimea

17 Julai 2023

Jeshi la wanamaji la Ukraine na kikosi cha usalama cha SBU wamekiri kufanya shambulio kwenye daraja la Kerch lililojengwa na Urusi na linalounganisha eneo la Crimea na Urusi. Urusi iliinyakua Crimea mnamo 2014.

Pichani ni sehemu ya barabara iliyoachana kufuatia shambulizi kwenye daraja la Crimea, linalounganisha Urusi Bara na Rasi ya Crimea.
Picha: Сrimea24tv via REUTERS

Hayo yanajitokeza huku Urusi ikitangaza kusimamisha rasmi makubaliano ya usafirishaji wa nafaka na kuongeza kuwa watarejea ikiwa tu masharti ya makubaliano hayo ya kusafirisha nafaka kupitia Bahari Nyeusi yatatimizwa. 

Kulingana na duru za usalama za nchini Ukraine kwa shirika la habari la AFP, jeshi la wanamaji la Ukraine na kikosi cha usalama cha SBU walifanya shambulio hilo la usiku wa jana kwenye daraja la Kerch lililojengwa na Urusi na linalounganisha eneo la Crimeana Urusi. Duru hizo zimesema hiyo ilikuwa ni operesheni maalumu ya SBU na jeshi hilo la majini kwa kutumia droni zinazorushwa kutokea majini, ingawa amekiri haikuwa rahisi kulifikia daraja hilo. Daraja hilo hutumika kama kiungo muhimu cha kupeleka  vifaa kwa wanajeshi wa Urusi wanaopigana nchini Ukraine.

Ikulu ya Kremlin imesema rais Vladimir Putin tayari ametaarifiwa kuhusiana na shambulizi hilo ililoliita la kigaidi kwenye daraja la Crimea ambapo watu wawili waliuawa. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari kwamba Ukraine imehusika na shambulizi hilo na kuongeza kuwa Moscow itachukua hatua za kuzuia kushambuliwa tena kwa daraja hilo ambalo hata hivyo tayari liliwahi kushambuliwa na bomu lililotegwa kwenye lori mwezi Oktoba 2022. Moscow iliituhumu Ukraine kwa shambulizi hilo, ingawa Kyiv, ilikana.

Vita vya Urusi nchini Ukraine vimekuwa vikiyalenga maenei ya kimkakati ikiwa ni pamoja na madarja muhimu.Picha: Alexander Kazakov/Kremlin Pool/IMAGO

Soma Zaidi: Kwa nini Daraja la Kerch ni muhimu kwa Urusi na Ukraine?

Gavana aliyewekwa n Urusi kwenye eneo hilo la Crimea Sergey Aksyonov amezungumzia hali ilivyo baada ya shambulizi hilo. Kulingana na Aksyonov, safari za treni zitaanza tena kabla ya saa tatu za asubuhi kwa majira ya Moscow.

"Kutokana na tukio hilo, safari zilisimamishwa kwenye Daraja la Crimea na sababu zinachunguzwa. Vyombo vya kisheria, wizara ya Hali ya Dharura, vyombo vilivyoidhinishwa katila wilaya ya Krasnodar, Wizara ya Usafirishaji ya Shirikisho la Urusi na Jamhuri ya Crimea wote wiko kwenye eneo hilo. Taarifa itachapishwa kwenye vyanzo rasmi."

Huku hayo yakijiri, Urusi imetangaza muda mfupi uliopita kusimamisha rasmi makubaliano ya usafirishaji wa nafaka na kuongeza kuwa watarejea ikiwa tu masharti yao yatatimizwa. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Urusi, Maria Zakharova amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba ikiwa sehemu ya makubaliano hayo ya nafaka kupitia Bahari Nyeusi yatatekelezwa, Urusi itarejea mara moja kwenye utekelezwaji wake. Tayari Urusi imeuarifu Umoja wa Mataifa, Ukraine na Uturuki juu ya uamuzi huo wa kutoongeza muda wa makubaliano hayo.

Urusi na Ukraine ndio wazalishaji wakubwa wa nafaka na vita kati yao vimesababisha pngezeko la bei kote ulimwenguni.Picha: Mehmet Emin Caliskan/REUTERS

Awali mwanasiasa mmoja mwandamizi alisema Urusi haipaswi kurejea kwenye makubaliano hayo yaliyofikiwa chini ya uratibu wa Uturuki na Umoja wa Mataifa mwezi Julai mwaka uliopita, yakilenga kupunguza wasiwasi wa mzozo wa chakula ulimwenguni kwa kuruhusu usafirishwaji wa nafaka kutoka Ukraine, ambazo zilikuwa zimekwama kufuatia mashaka ya kiusalama yaliyoibuliwa na vita kati ya Urusi na Ukraine.

Muda wa makubaliano hayo ulikuwa unafikia mwisho hii leo baada ya kurefushwa mara kadhaa, lakini Kremlin iliwahi kuashiria huko nyuma kwamba haikuwa inaridhishwa na namna yalivyokuwa yanatekelezwa. Ukraine na Urusi ni wasafirishaji wakubwa wa nafaka na vita kati yao imesababisha bei ya bidhaa hiyo kupanda kote ulimwenguni.

Soma Zaidi:Mkataba wa usafirshaji nafaka unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa warefushwa kwa miezi miwili zaidi. 

Nchini Ukraine kwenyewe, vikosi vya nchi hiyo vimedai kulirejesha eneo la karibu kilomita za mraba 18 za huko mashariki na kusini wiki iliyopita, kufuatia mashambulizi ya kushitukiza dhidi ya vikosi vya Urusi, hii ikiwa ni kulingana na naibu waziri wa ulinzi, Hanna Maliar mapema leo. Hadi sasa eneo la karibu kilomita za mraba 210 yamerejeshwa tangu kuanza kwa mashambulizi hayo mwezi Juni yanayolenga kurejesha maeneo yaliyodhibitiwa na Urusi katika vita hivyo vilivyotimiza miezi 17.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW