1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine yaomba msaada zaidi wa kijeshi

12 Desemba 2022

Waziri Mkuu wa Ukraine, Denys Shmyhal ameomba msaada zaidi wa kijeshi ikiwemo mitambo ya kurushia makombora aina ya Patriot na mifumo ya teknolojia ya juu ya kuzuia makombora ili kukabiliana na mashambulizi ya Urusi.

Ukraine Donbass US M777  Haubitze
Picha: AP Photo/Efrem Lukatsky/picture alliance

Shmyhal amekiambia siku ya Jumatatu kituo cha redio cha Ufaransa, LCI kwamba Urusi inataka kuizamisha Ulaya kwa wimbi jipya la wakimbizi wa Ukraine kutokana na kushambulia miundombinu ya Ukraine na kusababisha kukatika kwa umeme na maji na kuwaacha mamilioni ya watu wakipigwa na baridi kali.

Kauli hiyo ameitoa huku ikiripotiwa kuwa Urusi imefanya mashambulizi kwenye majimbo ya mashariki mwa Ukraine, siku ya Jumatatu ambako Urusi inajaribu kuifanya kuwa maeneo ya mapambano.

Hadi sasa hakuna nchi ambayo imeipatia Ukraine mitambo ya kurushia makombora aina ya Patriot, ingawa Ujerumani ilitoa mitambo hiyo kwa nchi jirani ya Poland ambayo ni mshirika wake wa Jumuia ya Kujihami ya NATO.

Shmyhal amesema zaidi ya mashambulizi 1,000 ya Urusi katika miundombinu muhimu ya Ukraine kuanzia mwezi Oktoba, huenda yakachochea wimbi jingine la wahamiaji kuelekea Ulaya.

Waziri Mkuu wa Ukraine, Denys ShmyhalPicha: JOHN THYS/AFP

Hayo yanajiri siku moja baada ya Rais wa Marekani, Joe Biden kuihakikishia Ukraine kuhusu msaada zaidi wakati ambapo Urusi inaendelea kushambulia gridi za umeme, huku wakaazi wengi katika jimbo la kusini la Odessa wakiwa hawana umeme.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa Biden alizungumza jana kwa njia ya simu na Rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky kusisitiza kuhusu msaada wa kiusalama, kiuchumi na kiutu kwa Ukraine, wakati mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu muhimu yakiendelea.

Akilihutubia taifa kwenye ujumbe wake wa usiku wa kuamkia Jumatatu, Zelensky amesema msaada huo hausaidii tu katika uwanja wa mapambano, bali pia kudumisha utulivu wa uchumi wa taifa la Ukraine.

Ukraine yashambulia eneo linalodhibitiwa na Urusi

Katika uwanja wa mapambano, Ukraine imedai kufanya mashambulizi kadhaa ya makombora katika eneo linalodhibitiwa na Urusi siku ya Jumapili. Taarifa ya maafisa waandamizi wa kijeshi haikueleza maeneo hasa yaliyolengwa, lakini imesema maeneo yaliyoshambuliwa ni pamoja na mabweni na maghala.

Aidha, jeshi la Ukraine limesema Urusi ilianzisha jana mashambulizi na kwamba bado kuna hatari kutoka kwa adui wake huyo kwamba inaweza kufanya mashambulizi ya maroketi na ndege zisizo na rubani katika miundombinu ya nishati ya Ukraine na eneo lote la nchi hiyo.

Soma zaidi: Urusi yaishutumu Marekani

Ama kwa upande mwingine, Urusi imeishutumu Marekani kwa kutokuchukua mbinu nzuri za kujenga kuhusu mazungumzo ya kidiplomasia mjini Istanbul, lakini imesema mji huo wa Uturuki ni sehemu sahihi kwa mawasiliano kama hayo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Vershinin amesema Jumatatu, kuwa Istanbul ni sehemu nzuri kwa mazungumzo ya kidiplomasia. Wanadiplomasia wa Urusi na Marekani walikutana siku ya Ijumaa mjini Istanbul kuzungumzia masuala kadhaa ya kiufundi katika uhusiano wao kama vile visa.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell Picha: EU Parlament

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umekubali kuongeza euro bilioni mbili katika mfuko ambao umekuwa ukitumika kama msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema Jumatatu kuwa umoja huo bado umejizatiti kuipatia Ukraine msaada wa silaha pamoja na washirika wake wengine.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Brussels, wamefikia makubaliano ya kisiasa ya kuongeza euro bilioni mbili zaidi kwa ajili ya msaada wa fedha wa mwaka ujao. Kiasi hicho kinaweza kuongezeka hadi euro bilioni 5.5 ifikapo mwaka 2027, iwapo nchi wanachama zitakubali baadae ikiwa kuna hitaji la kufanya hivyo.

Wanadiplomasia wa Ulaya kuiwekea Urusi vikwazo vipya

Mawaziri hao wanatarajiwa pia kuweka vikwazo vipya kwa Urusi kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine. Pia watajadili sera pana za Umoja wa Ulaya nchini Ukraine, ikiwemo mafunzo ya kijeshi kwa vikosi vya kijeshi vya Ukraine.

Nao viongozi wa kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7, wanatarajiwa kukutana Jumatatu kuzungumzia vita vya Ukraine, ambapo na Rais Zelensky atahudhuria pia. Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz ndiyo mwenyeji wa mkutano huo unaofanyika kwa njia ya video. Mkutano huo unafanyika baada ya Zelensky kuzungumza na viongozi wa Marekani, Uturuki na Ufaransa.

(DPA, AP, AFP, Reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW