1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yapigwa tena; mawaziri wa Marekani kuzuru Kyiv

24 Aprili 2022

Maafisa wa Ukraine wamesema vikosi vya Urusi vilijaribu kuvamia kiwanda cha chuma kinachowahifadhi wanajeshi na raia mjini Mariupol katika jaribio la kusambaratisha upinzani wa mwisho majini Mariupol.

Ukraine-Krieg - PK | Präsident Selenskyj in Kiew
Picha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, wakati huo huo, ametangaza kuwa atakutana Jumapili katika mji mkuu wa taifa lake na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, na waziri wa ulinzi wa Lloyd Austin. Ikulu ya White House ilikataa kuzungumzia ziara hiyo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Zelenskyy alitoa maelezo kidogo kuhusu maandalizi ya mkutano huo lakini alisema alitarajia matokeo madhubuti, "sio zawadi tu au aina fulani ya keki, tunatarajia vitu maalum na silaha mahususi.'' 

Itakuwa ni safari ya kwanza ya maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani kwenda Kyiv tangu vita vilipoanza Februari 24. Akiwa ziarani Poland mwezi Machi, Blinken aliingia kwa muda mfupi katika ardhi ya Ukraine kukutana na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo. Mkutano wa mwisho wa Zelenskyy wa ana kwa ana na kiongozi wa Marekani ulikuwa Februari 19 na Makamu wa Rais Kamala Harris.

Soma zaidi: Kaburi jengine la pamoja lagunduliwa Mariupol

Katika mashambulizi ya mkesha wa Pasaka ya ki Orthodox, vikosi vya Urusi vimeyashambulia majiji na miji kusini na mashariki mwa Ukraine. Mtoto mwenye umri wa miezi 3 alikuwa miongoni mwa watu wanane waliouawa wakati Urusi ilipofyatua makombora ya kasi kubwa dhidi ya mji la bandari ya Bahari Nyeusi wa Odesa, maafisa wamesema. Zelenskyy amesema watu wengine 18 walijeruhiwa.

Magari ya kijeshi ya Urusi yakitembea katika eneo linalodhibitiwa na waasi wanaotaka kujitenga mjini Mariupol, Ukraine, Jumamosi, Aprili, 23, 2022.Picha: Alexei Alexandrov/AP Photo/picture alliance

"Vita vilianza mtoto huyu akiwa na mwezi mmoja. Unaweza kufikiria nini kinatokea?'' Zelenskyy alisema. "Hao ni wanaharamu tu. ... Sina maneno mengine kwa hilo, wanaharamu tu.''

Jeshi la Ukraine limesema Jumamosi liliharibu kituo cha kamandi ya Urusi mjini Kherson, mji wa kusini ambao uliangukia mikononi mwa wanajeshi wa Urusi mwanzoni mwa vita.

Kituo hicho cha kamandi kilipigwa siku ya Ijumaa, na kuua majenerali wawili na kumjeruhi vibaya mwingine, shirika la ujasusi la kijeshi la Ukraine lilisema katika taarifa. Jeshi la Urusi halikutoa kauli yoyote juu ya madai hayo, ambayo hayakuweza kuthibitishwa.

Oleksiy Arestovych, mshauri wa Zelenskyy, alisema katika mahojiano ya mtandaoni kwamba maafisa waandamizi 50 wa Urusi walikuwa kwenye kituo hicho cha kamandi wakati kinashambuliwa.

Soma pia: Marekani yaongeza msaada Ukraine, Urusi ikidai ushindi Mariupol

Hatima ya Waukraine waliozingirwa katika kiwanda cha chuma mjini Mariupol, ambapo Urusi inasema vikosi vyake vimechukua sehemu nyingine ya mji huo, haikujulikana mara moja. Mapema Jumamosi, kitengo cha kijeshi cha Ukraine kilitoa video iliyoripotiwa kuchukuliwa siku mbili mapema ikiwaonyesha wanawake na watoto waliojificha chini ya ardhi, wengine kwa muda wa miezi miwili, wakisema wanatamani kuliona jua.

"Tunataka kuona anga yenye amani, tunataka kupumua katika hewa safi,'' mwanamke mmoja kwenye video hiyo alisema. `"Hujui maana ya kula kwetu, kunywa chai iliyotiwa tamu. Kwetu sisi hilo ni jambo la furaha.''

Watu wamoja

Urusi ilisema imechukua udhibiti wa vijiji kadhaa kwingineko katika eneo la mashariki la Donbas na kuharibu maeneo 11 ya jeshi la Ukraine kwa usiku mmoja, yakiwemo maghala matatu ya mizinga. Mashambulizi ya Urusi pia yalishambulia maeneo yenye watu wengi.

Shinikizo laongezeka kwa Ujerumani kutuma silaha nzito Ukraine

02:05

This browser does not support the video element.

Waandishi wa shirika la habari la Associated Press walishuhudia makombora katika maeneo ya makazi ya Kharkiv, jiji la pili kwa ukubwa nchini Ukrainia; mkuu wa mkoa Oleh Sinehubov alisema watu watatu waliuawa. Katika mkoa wa Luhansk wa Donbas, Gavana Serhiy Haidai alisema watu sita walikufa katika shambulio la makombora katika kijiji cha Gorskoi.

Katika mji wa Sloviansk, ulioko kaskazini mwa Donbas, AP ilishuhudia wanajeshi wawili wakiwasili hospitalini, mmoja wao akiwa amejeruhiwa vibaya. Akiwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu nje ya nyumba yake iliyoharibiwa mjini Sloviansk, Anna Direnskaya mwenye umri wa miaka 70, alisema, "Nataka amani."

Mmoja wa wazungumzaji wengi wa asili ya Kirusi mashariki mwa Ukraine, Direnskaya alisema anatamani Warusi wangeelewa kwamba Waukraine si watu wabaya na kwamba hakupaswi kuwepo na uadui kati yao. "Kwa nini hii inatokea?" alisema. "Sijui.''

Wakati maafisa wa Uingereza wakisema kuwa vikosi vya Urusi havijapata mafanikio mapya makubwa, maafisa wa Ukraine wametangaza amri ya kutotoka nje kwa nchi nzima kabla ya Jumapili ya Pasaka, katika ishara ya namna vita hivyo vilivyosababisha uvurugaji na kitisho kwa nchi nzima.

Umuhimu wa Mariupol

Mji wa Mariupol umekuwa shabaha muhimu ya Urusi na umechukua umuhimu mkubwa katika vita. Kukamilisha utwaji wake kutaipa Urusi ushindi wake mkubwa zaidi, baada ya mzingiro wa takriban miezi miwili kuigeuza sehemu kubwa ya mji huo kuwa magofu yanayofuka moshi.

Hatua hiyo itawapokonya Ukraine bandari muhimu, kuwaweka huru wanajeshi wa Urusi kupigana kwingineko na kuanzisha ukanda wa ardhini kuelekea rasi ya Crimea, ambayo Moscow iliiteka mwaka wa 2014. Wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi wanadhibiti maeneo ya Donbas.

Mshauri wa ofisi ya rais wa Ukraine, Oleksiy Arestovych, amesema vikosi vya Urusi vilianzisha tena mashambulizi ya anga kwenye kiwanda cha Azovstal na pia walikuwa wakijaribu kukivamia, katika mabadiliko dhahiri ya mbinu. Siku mbili kabla ya hapo, Rais wa Urusi Vladimir Putin alikuwa ametoa amri ya kutotuma wanajeshi badala yake kukizingira kiwanda hicho.

Mfanyakazi wa uokozi akimsaidia mkaazi kuondoka baada ya shambulio mjini Odessa, kusini mwa Ukraine. Shambulio la Urusi liliripotiwa kuuwa watu wasiopungua watano.Picha: State Emergency Service of Ukraine/AFP

Mapema Jumamosi, Kikosi cha Azov cha jeshi la ulinzi wa taifa la Ukraine, ambacho wanachama wake ndiyo wamejificha kwenye kiwanda hicho, kilitoa video ya takriban dazeni mbili za wanawake na watoto. Maudhui yake hayakuweza kuthibitishwa kwa uhuru. Lakini ikiwa ni kweli, itakuwa ni ushahida wa kwanza wa video wa namna maisha yalivyo kwa raia walionaswa chini ya ardhi huko.

Soma pia:Macron, Scholz waepuka kutaja mauaji ya Ukraine kuwa "halaiki"

Video hiyo inaonyesha askari wakiwapa peremende watoto wanaoshukuru kwa kutumia ngumzi. Msichana mmoja mdogo anasema yeye na jamaa zake "hawajaona anga wala jua'' tangu walipoondoka nyumbani Februari 27.

Naibu kamanda wa kikosi hicho, Sviatoslav Palamar, aliambia AP kuwa video hiyo ilirekodiwa siku ya Alhamisi. Kikosi cha Azov kina mizizi yake katika batalioni ya Azov, ambayo iliundwa na wanaharakati wa mrengo mkali wa kulia mnamo 2014 mwanzoni mwa mzozo wa kujitenga mashariki mwa Ukraine na kuzusha ukosoaji kutokana na baadhi ya mbinu zake.

'Zaidi ya raia 20,000 wameuawa'

Zaidi ya watu 100,000, idadi hii ikiwa imeshuka kutoka kwa idadi ya wakaazi 430,000 wa kabla ya vita, wanaaminika kubaki Mariupol ambako wanakabiliwa na uhaba wa chakula duni, maji au joto la majumbani. Mamlaka nchini Ukraine zinakadiria kuwa zaidi ya raia 20,000 wameuawa mjini humo.

Soma pia:UN: Zaidi ya raia milioni 4.9 wa Ukraine wameikimbia nchi hiyo

Licha ya hayo, jaribio jengine la kuwaondoa wanawake, watoto na watu wazima kutoka Mariupol lilishindikana siku ya Jumamosi. Petro Andryuschenko, mshauri wa meya wa Mariupol, alisema vikosi vya Urusi havikuruhusu mabasi yaliyopangwa na Ukraine kuwapeleka wakaazi hadi Zaporizhzhia, jiji lililo umbali wa kilomita 227 (maili 141) kaskazini-magharibi.

Kiwanda cha chuma cha Azovstal kikiwa kimeharibiwa vibaya kufuatia shambulizi la vikosi vya Urusi mjini Mariupol.Picha: Peter Kovalev//ITAR-TASS/IMAGO

"Majira ya saa tano asubuhi, wakaazi wasiopungua 200 wa Mariupol walikusanyika karibu na kituo cha maduka cha Port City, wakisubiri kuhamishwa,'' Andryuschenko aliandika kwenye chaneli ya Telegram. "Jeshi la Urusi lilikwenda hadi walipokusanyika wakaazi  haowa Mariupol na kuwaamuru kutawanyika, kwa sababu sasa kutakuwa na mashambulizi.''

Wakati huo huo, alisema, mabasi ya Urusi yalikusanyika umbali wa karibu mita 200. Wakazi waliopanda basi hizo waliambiwa walikuwa wakipelekwa katika eneo linalokaliwa na watu wanaojitenga na hawakuruhusiwa kushuka, Andryuschenko alisema. Akaunti yake haikuweza kuthibitishwa kwa uhuru.

Dhamana za usalama

Katika shambulio dhidi ya Odesa, wanajeshi wa Urusi walirusha takriban makombora sita, kulingana na Anton Gerashchenko, mshauri wa waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine.

"Wakazi wa jiji hilo walisikia milipuko katika maeneo tofauti,'' Gerashchenko alisema kupitia Telegram. "Majengo ya makaazi yalipigwa. Tayari inajulikana kuhusu mwathirika mmoja. Alichomeka ndani ya gari lake katika ua wa moja ya majengo.''

Mkutano wa waandishi wa habari wa Zelenskyy ulifanyika katika kituo cha treni ya chini ya ardhi cha Kyiv, ambapo alisimama wakati treni ilipopita kwa kelele. Mfumo wa treni za chini ya ardhi, unaojumuisha kituo chenye kina kirefu zaidi ulimwenguni, ulivutia watu wengi mapema katika vita wakati umati wa watu ulipojificha huko.

Kuhusu ziara inayotarajiwa Jumapili ya maafisa wa Marekani, Zelenskyy alisema: "Ninaamini kwamba tutaweza kupata makubaliano kutoka Marekani au sehemu ya mpango huo wa kuipa Ukraine silaha ambayo tulikubaliana hapo awali. Mbali na hilo, tuna maswali ya kimkakati kuhusu dhamana ya usalama, ambayo ni wakati wa kuijadili kwa kina, kwa sababu Marekani itakuwa mojawapo ya nchi viongozi wa usalama kwa taifa letu.''

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW