Ukraine yasema imedungua droni za Urusi
27 Desemba 2023Kulingana na Gavana wa mkoa wa Odesa kwa upande wa Ukraine mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 35 aliuawa kwa kuangukiwa na vifusi kutoka ndege iliyodunguliwa na kuanguka katika eneo la makaazi.
Wizara ya mambo ya ndani ya Ukraine imesema watu wengine wanne, akiwemo mtoto wa miaka sita, pia walijeruhiwa.
Soma pia: Zelensky awasifu wanajeshi wake kwa kudungua ndege za Urusi
Haya yanajiri saa chache baada ya vikosi vya Urusi kushambulia kwa kombora kituo kimoja cha treni kwenye mji wa Kherson wakati mamia ya watu wakisubiri usafiri ili kutoroka mapigano.
Waziri mambo ya ndani wa Ukraine Ihor Klymenko ameandika kupitia mtandao wa Telegram kwamba afisa mmoja wa polisi ameuwawa na wengine wawili wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo.
Aidha waziri huyo amesema hivi sasa zaidi ya watu 100 wanapangiwa kuondoka eneo hilo kwa kutumia mabasi kupelekwa eneo salama. Mji wa Kherson ulikuwa chini ya udhibiti wa Urusi katika siku za mwanzo za vita lakini ulikombolewa na vikosi vya Ukraine miezi michache baadaye.
Mjio huo unapatikana kwenye jimbo la kusini mwa Ukraine lenye jina sawa na hilo na ambalo Urusi ilidai kulikamata mwaka uliopita licha ya ukweli kwamba hadi sasa bado imeshindwa kuchukua udhibiti kamili.
Urusi yapata pigo
Kwa upande wa Urusi Ikulu ya Kremlin hapo jana ilikiri kuwa shambulizi la Ukraine liliharibu meli yake ya kivita katika bandari ya Crimea ya Feodosia katika kile Ukraine na washirika wake wa Magharibi walichokiita kuwa ni kikwazo kikubwa kwa jeshi la wanamaji la Urusi.
Soma pia:Urusi yaendeleza mashambulizi ya droni wakati Ukraine ikijiandaa na sikukuu ya Krismasi
Ukraine inadai kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba ndege zisizo na rubani kwa ajili ya matumizi ya vita vya Urusi dhidi ya Kyiv.
Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha moto kwenye eneo la bandari, na kufuatiwa na mlipuko mkubwa na moto.
Gavana aliyechaguliwa na Moscow, Sergei Aksyonov, aliandika kwenye mtandao wa Telegraph kwamba kutokana na shambulizi hilo, mtu mmoja aliuawa na wengine wawili walijeruhiwa.
Waziri wa ulinzi wa Uingereza Grant Shapps kupitia mtandao wa Twitter aliandika kwamba "uharibifu huu wa hivi karibuni dhidi ya jeshi la wanamaji la Putin unaonyesha kwamba wale wanaoamini kuwa kuna mkwamo katika vita vya Ukraine wanakosea!"
Shapps ameongezea kusema kwamba udhibiti wa Urusi katika Bahari Nyeusi sasa unapingwa.