1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine yasema imedungua ndege 28 za Urusi

12 Oktoba 2023

Ukraine imesema kwamba imedungua ndege 28 za Urusi, huku mamlaka za kusini zikiripoti kwamba mashambulizi yameharibu maghala katika bandari ya Odesa na makazi ya watu binafsi, na kumjeruhi mtu mmoja.

Ukraine Air scouts
Afisa wa jeshi la anga wa UkrainePicha: Hanna Sokolova/DW

Huku haya yakijiri rais wa Urusi Vladimir Putin amewasili nchini Kyrgyzstan kwa ziara ya siku mbili, ikiwa ni safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu kutolewa kwa waranti wa kukamtwa na Mahakama ya Uhalifu ICC. 

Soma pia: Shambulio la Urusi lauwa watu 51 Kharkiv, Ukraine

Kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram jeshi la anga la Ukraine limesema kwamba vikosi vyake vimedungua droni 28 aina ya Shahed chapa 136/131 kati ya jumla ya 33 zilizorushwa kutoka eneo la Belgorod la Urusi kuelekea kaskazini na nyengine kutoka rasi ya Crimea inayokaliwa na Urusi kuelekea kusini.

Vikosi vya Ulinzi vya Kusini mwa Ukraine vimesema Urusi imefanya mashambulizi mengine ya ndege zisizo na rubani kulenga miundombinu ya bandari kando ya mto Danube. Huku jumla ya ndege nne zisizo na rubani zikiharibiwa katika eneo la Mykolayiv na 10 katika mkoa wa Odesa.

Gavana wa Odesa Oleg Kiper aliandika katika chapisho tofauti kwenye Telegram, akisema kwamba miundombinu ya bandari ya Odesa na majengo ya maakazi katika wilaya ya Izmail vimeharibiwa.

Soma piaUkraine yadungua ndege 27 za Urusi zisizoendeshwa na rubani

Urusi ilizidisha mashambulizi kwenye bandari za kusini mwa Ukraine baada ya kujiondoa katika makubaliano ya kuruhusu usafirishaji wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi mwezi Julai.

Kyiv imeonya kwamba Moscow imeanzisha tena kampeni ya mashambulizi ya angani kwenye miundombinu ya nishati ya Ukraine, inayoakisi mashambulizi ya kimfumo ambayo mwaka jana yaliwaacha mamilioni ya watu bila mfumo wa kupasha joto majumbani na maji kwa muda mrefu katika kipindi cha baridi kali.

Mfumo wa nishati wa UkrainePicha: Ukrainische nationale Energiegesellschaft „Ukrenergo“

Katika ziara yake ya kwanza katika makao makuu ya NATO tangu uvamizi kamili wa Urusi, Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky amewataka washirika wake kuendelea kuipa silaha ili kujinusuru wakati wa msimu wa baridi.

Soma pia: NATO: Tunaendelea kuiunga mkono Ukraine

Zelensky amesema amepokea hakikisho kutoka Marekani kwamba msaada wa kijeshi kwa Ukraine utasalia.

"Iliwekwa wazi kuwa Marekani itaendelea kuipatia Ukraine msaada wa mara kwa mara na usioingiliwa na unaohitajika kwa ulinzi wake." alisema Zelensky

Huku haya yakijiri rais wa Urusi Vladimir Putin amewasili nchini Kyrgyzstan hii leo kwa ziara yake ya kwanza ya kigeni tangu kutolewa kwa kibali cha kukamtwa kwake kutoka kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC mwezi Machi.

Katika ziara hiyo ya siku mbili, Putin anatarajiwa kukutana na rais Sadry Zhaparov na kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Madola Huru, CIS, iliyoundwa baada ya kuanguka kwa uliokuwa Muungano wa Kisovieti.

Hii ni ziara ya kwanza ya Putin kwa mwaka huu tangu kutolewa kwa waranti hio ya ICC baada ya kuivamia Ukraine Februari 2022 na kumtuhumu kwa matukio kama ya utekaji na kuwaondosha watoto kwenye maeneo yanayokaliwa na Urusi nchini Ukraine.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW