1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yadungua makombora 18 ya masafa marefu ya Urusi

8 Januari 2024

Kamanda mkuu wa jeshi nchini Ukraine amesema Urusi ilitumia makombora ya masafa marefu 59, roketi na ndege zisizo na rubani katika mashambulio makali ya anga dhidi ya nchi yake.

Ukraine Krieg | Luftangriff Charkiw
Picha: Sofiia Gatilova/REUTERS

Kamanda huyo Mkuu wa Ukraine, Valery Salushnyi amesema majeshi ya Ukraine yamefaulu kuzidungua ndege zote nane zisizo na rubani aina ya Shahed, zilizotengenezwa na Iran na makombora 18 kati ya makombora 51 yaliyorushwa na Urusi. Hata hivyo hakuna uthibitisho juu ya kauli hiyo ya Ukraine. Salushnyi amesema miundombinu ya kiraia, ya viwanda na kijeshi imeshambuliwa.

Waokoaji wakimwondoa mtu aliyenaswa kwenye kifusi kwenye eneo lililoshambuliwa kwa kombora la Urusi katika Mkoa wa Dnipropetrovsk, nchini Ukraine. Januari 8, 2024.Picha: State Emergency Service of Ukraine in Dnipropetrovsk region/REUTERS

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imetangaza kwamba imefanya mashambulizi ya pamoja dhidi ya miundombinu ya kijeshi na katika viwanda ndani ya Ukraine.

Na kwamba hili ni shambulio la tatu kubwa katika muda wa zaidi ya wiki moja, wakati huu mashambulizi yalilenga maeneo ya mashariki na kusini mwa Ukraine, ambayo mifumo ya tahadhari ya mashambulizi ya anga ni michache tofuti na iliyowekwa katika mji mkuu wa Ukraine, Kiyv.

Soma Pia:Urusi yafanya mashambulizi katika mikoa ya Kherson na Kharkiv

Urusi mapema leo Jumatatu iliishambulia Ukraine kwa makombora yaliyopiga hadi karibu na maeneo ya mstari wa mbele wa mapigano katika upande wa mashariki, kati na magharibi mwa Ukraine. Raia wanne wamefariki na wengine 30 wamejeruhiwa.

Watu 19 wakiwemo watoto wamejeruhiwa katika mji wa Novomoskovsk kwenye mkoa wa Dnipropetrovsk baada ya Urusi kulishambulia eneo hilo kwa makombora mnamo Januari 8. Mashambulio hayo yamesababisha uharibifu kwenye makazi ya watu.

Mashambulizi ya Urusi katika eneo la Dnipropetrovsk nchini Ukraine. Picha inaonyesha kliniki iliyoharibiwa katika shambulio la kombora la Urusi, wakati wa mashambulio ya Urusi dhidi ya Ukraine.Picha: DNIPROPETROVSK REGIONAL MILITARY/REUTERS

Wahanga hao 19 wanapatiwa matibabu na msaada wa kisaikolojia. Majengo matatu ya serikali, vituo viwili vya gesi, jengo la ghorofa tano na gari viliharibiwa. Daktari katika hospitali ya mji huo amesema watoto watano ni miongoni mwa watu hao 19 waliojeruhiwa kwenye mashambulio ya Urusi.

Amesema kati ya hao watano watatu wamelazwa kwenye wodi ya watoto na wawili wamepelekwa katika hospitali kuu ya mkoa, mmoja akiwa amevunjika taya na mwingine amajeruhiwa kwenye jicho.vWatoto hao ni wavulana wawili wana umri wa miaka 4 na minane. Na wasichana watatu wana umri wa miaka 11, 16 na 17.

Soma Pia:Marekani imesema Urusi ilitumia makombora ya Korea Kaskazini kuishambulia Ukraine

Maafisa wa Magharibi na wachambuzi walitahadharisha hapo awali kwamba Urusi ilikuwa inakusanya makombora yake kwa ajili ya mkakati wake wa mashambulizi ya msimu wa baridi.

Tofauti na msimu wa baridi uliopita, ambapo majeshi ya Urusi yalilenga gridi ya umeme nchini Ukraine, Urusi imesema sasa inalenga sekta ya ulinzi ya Ukraine lakini mashambulio hayo ya kila siku mara kwa mara yanalenga maeneo ya raia kama vile makazi na maduka makubwa, kote nchini Ukraine.

Magari yaliyoharibiwa katika ua wa majengo ya ghorofa. Mamlaka ya eneo hilo inasema ni baada ya mashambulizi ya jeshi la Ukraine katika jiji la Belgorod, nchini Urusi, Januari 5, 2024.Picha: REUTERS

Wakati huo huo Urusi nayo imelazimika kuwahamisha wakazi 300 kutoka mji wa mpakani wa Belgorod kutokana na mashambulizi ya makombora kutoka Ukraine. Hiyo ni idadi kubwa zaidi ya watu waliohamishwa kutoka kwenye mmoja wapo wa miji mikubwa nchini Urusi tangu mzozo ulipoanza.

Majeshi ya Ukraine yamefanya mashambulizi makali kuulenga mji wa Belgorod, ulio takriban kilomita 32 kutoka kwenye mpaka kati ya Urusi na Ukraine.

Vyanzo: DPA/AP/AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW