1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Ukraine yasema itaendelea kujibu mashambulizi

18 Septemba 2023

Jeshi la Ukraine limesema litaendelea kujibu mashambulizi karibu na kijiji cha Klishchiivka baada ya kutangaza kwamba vikosi vyake vimekiteka tena.

Ukrainische Artillerie feuert auf das Dorf Klischtschijiwka in der Region Donetsk
Picha: Diego Herrera Carcedo/AA/Picture Alliance

Jeshi la Ukraine limesema litaendelea kujibu mashambulizi karibu na kijiji cha Klishchiivka baada ya kutangaza jana usiku kwamba vikosi vyake vimekiteka tena kijiji hicho muhimu kilicho karibu na mji unaodhibitiwa na Urusi wa Bakhmut.

Soma pia: Ukraine yadai kuikomboa wilaya muhimu ya mji wa Bakhmut

Kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, mnadhimu mkuu wa jeshi la Ukraine ameandika kwamba vikosi vya ulinzi vinaendelea na operesheni za uvamizi katika maeneo ya jirani ya Klishchiyivka, na vimesababisha hasara kubwa kwa wanajeshi na vifaa vya adui na kuunganisha maeneo mapya, huku vikosi vya Urusi vikijaribu kupenya bila mafanikio karibu na kijiji jirani cha Andriivka.

Kumekuwa kukiripotiwa mapigano makali karibu na kijiji cha Klishchiivka, ambacho kwa muda mrefu kilikuwa chini ya udhibiti wa vikosi vya Urusi, lakini jana Jumapili, Rais Volodymyr Zelenskyalitangaza jeshi la Ukraine limekitwaa tena kijiji hicho katika eneo la Donetsk.

"Kwa kila mtu anayetetea anga ya nchi yetu. Marubani wetu na wahandisi wa Jeshi la Anga, wapiganaji wa vikundi vya zimamoto, wapiganaji wetu wote wa kupambana na ndege za maadui. Ahsanteni kwa kuongeza mara kwa mara idadi ya makombora na droni za Urusi zilizoanguka, Ahsanteni kwa kuwalinda watu wetu na miundombinu yetu. Ahsanteni, wapiganaji!" Alisema Zelensky.

Vijiji vyote viwili viko kilomita kadhaa kusini mwa mji wa Bakhmut, ambao vikosi vya Urusi viliweza kuudhibiti baada ya miezi kadhaa ya mapigano makali.

Soma pia: Putin: Operesheni ya Ukraine haijapata mafanikio

Huku haya yakijiri, serikali ya Ukraine leo imeamua kuwafuta kazi manaibu waziri sita wa ulinzi akiwemo Hanna Maliar, ambaye amekuwa akitoa taarifa za mara kwa mara za yanayojiri katika uwanja wa mapambano. Hata hivyo, Serikali haikutoa sababu ya uamuzi huo. Mapema mwezi huu Ukraine ilimteua Rustem Umerov kama waziri mpya wa ulinzi.

Kesi ya mauwaji ya halaiki

Mahakama ya ICJ Picha: Wiebe Kiestra/UN

Kwa upande mwengine, hii leo Mahakama ya Kimataifa ya Haki itaanza kusikiliza kesi ya Ukraine dhidi ya Urusi juu ya madai ya mauaji ya halaiki yaliyofanywa na Moscow wakati wa  uvamizi wake huku Urusi ikitaka kesi hiyo itupiliwe mbali.

Kyiv ilifunguwa kesi hiyo muda mfupi baada ya Urusi kuivamia Ukraine na  inataka mahakama hiyo kuiamuru Urusi kusitisha uvamizi wake na kulipa fidia.

Mahakama hiyo ilishawahi kuiamuru Urusi kusitisha uhasama nchini Ukraine mnamo mwezi Machi 2022 lakini Moscow iliupuuzia uamuzi huo na ikaendelea na mashambulizi yake mabaya dhidi ya Ukraine.

Soma pia: Vladimir Putin akubali mwaliko wa Kim Jong Un

Katika vikao vya wiki hii, mawakili wa Urusi wanatazamiwa kujenga hoja ya kupinga uhalali na mamlaka ya mamlaka hiyo kusikiliza kesi hii, wakati Ukraine ikitoa wito kwa majaji kuendelea kusikiliza kiini cha madai yake.

 

dpa//AFP