1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yasema Urusi yajiandaa kuushambulia mji wa Mariupol

Zainab Aziz Mhariri: Bruce Amani
12 Aprili 2022

Siku 47 tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky asema maelfu ya watu wameuawa katika mji wa pwani wa Mariupol na kwamba Urusi inapanga kufanya mashambulizi mapya katika mji huo wa bandari.

Ukraine | Kriegseindrücke aus Mariupol
Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema lengo kuu la Urusi ni kuudhibiti mji wa pwani wa Mariupol iliko bandari kuu ya mashariki, ambapo maelfu ya watu wameuawa. Kauli hiyo imethibitishwa na meya wa mji huo wa Mariupol, Vadym Boychenko ambaye amesema zaidi ya raia 10,000 wameuwawa katika kipindi cha wiki sita ambapo wanajeshi wa Urusi waliuzingira mji huo wa pwani.

Raia katika mji wa Mariupol wakipita kwenye majengo yaliyoharibiwa kutokana na vita nchini Ukraine.Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Rais Zelensky ametoa wito wa kuwekwa vikwazo vikali zaidi dhidi ya Urusi ili kuizuia kutumia silaha za kemikali nchini Ukraine na pia amesema nchi yake haina silaha za kutosha zinazohitajika kuweza kuukomboa mji wa Mariupol ambao upo hatarini kudhibitiwa na vikosi vya Urusi.

Rais huyo wa Ukraine amesema ikiwa hatimaye Urusi itauteka mji huo wa Mariupol, basi inaweza kuwaunganisha vyema wanajeshi wake wanaosonga mbele kutoka eneo la mashariki na wale wanaotoka kwenye eneo la Crimea, na hivyo wataweza kulizingira jeshi la Ukraine katika upande wa mashariki. Mariupol, mji wa bandari ulio kusini mashariki, una takriban wakazi 400,000.

Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Ronaldo Schemidt/AFP/Getty Images

Mkuu wa majeshi wa Ukraine amesema Urusi itajaribu pia kuichukua Popasna, mji mdogo katika mkoa wa Luhansk mashariki mwa Ukraine na pia inapanga kuanzisha mashambulio kwenye mji wa Kurakhove kutokea kwenye mji huo. Amesema kwa sasa vikosi vya Urusi vinajikusanya katika mikoa ya Belgorod na Voronezh iliyo kwenye mpaka wa Urusi na Ukraine.

Kansela wa Austria Karl Nehammer amesema hakuna matarajio iwapo hatua za kidiplomasia zitasaidia kuumaliza mzozo wa Ukraine baada ya mkutano wake na Rais wa Urusi Vladimir Putin. Wakati huo huo Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wameanzisha majadiliano kuhusu awamu ya sita ya vikwazo, lakini wameshindwa kufikia mwafaka, ikiwa ni pamoja na vikwazo vinavyolenga sekata za mafuta na gesi, huku Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi wakitarajiwa kukutana wakati ambapo Marekani imefadhaishwa na msimamo wa India wa kutoegemea upande wowote katika swala la uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Kushoto Rais wa Urusi Vladimir Putin. Kulia: Kansela wa Austria Karl Nehammer.Picha: Mikhail Klimentyev/Stefanie Loos/AFP

Shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF limesema karibu kila watoto wawili kati ya watatu wameyakimbia makazi yao kutokana na mapigano nchini Ukraine. Mkuu wa shirika hilo la UNICEF ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba katika zaidi ya miongo mitatu, hajawahi kuona watoto wengi hivyo wakihamishwa kutoka makwao.

Kwa upande wake Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema operesheni ya kijeshi nchini Ukraine bila shaka itafikia malengo yake ya kuilinda Urusi na kwamba mapigano na majeshi ya Ukraine dhidi ya Urusi yalikuwa hayaepukiki.

Vyanzo:AFP/RTRE/https://p.dw.com/p/49nuB

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW