Ukraine: Misaada ya washirika wetu inachelewa kufika
25 Februari 2024Nusu ya misaada ya kijeshi kutoka nchi za magharibi kwenda Ukraine iliwasili kwa kuchelewa, hatua inayokwamisha uwezo wa Kyiv kukabiliana na mashambulizi ya Urusi na kugharimu maisha ya raia, kwa mujibu wa waziri wa ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov.
Soma: Bunge la Marekani lagawika kuhusiana na msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine
Ukraine ambayo inakabiliwa na upungufu wa silaha, kwa miezi kadhaa imesema kuwa misaada kutoka kwa washirika wake wa nchi za Magharibi inachukua muda mrefu na kuwa na athari kubwa, wakati vita hivyo vikiingia mwaka wa tatu.
Wakati Ukraine ikitoa taarifa hiyo, Urusi imedai kuwa vikosi vyake vimeyadhibiti maeneo mengine muhimu karibu na miji ya Avdiivka na Donetsk. Hatua hiyo inajiri baada ya Rais Vladimir Putin wa Urusi kuamuru wanajeshi wake kusonga mbele zaidi ndani ya Ukraine ikiwa imetimia miaka miwili ya uvamizi wake kamili.