1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine yasema Urusi imeanza hujuma mpya upande wa mashariki

10 Februari 2023

Maafisa wa Ukraine wamesema Urusi imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo ambayo yamekuwa kitovu cha mapigano katika wiki za karibuni.

Ukraine-Krieg | Folgen eines russischen Raketenangriffs in Kramatorsk
Picha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Tathmini hiyo imetolewa na viongozi wa majimbo ya mashariki katika wakati ambapo hii leo rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy anakamilisha ziara yake kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels alikokwenda kusaka mshikamano na kuomba msaada zaidi wa silaha.

Serikali mjini Kyiv ilitabiri kuwa Urusi itazidisha hujuma zake katika wiki za kuelekea kutimia mwaka mmoja tangu Moscow ilipotuma vikosi vyake kwenye ardhi ya Ukraine Februari 24 mwaka jana.

Wakuu wa serikali kwenye majimbo ya mashariki mwa Ukraine ikiwemo Donetsk wamesema wanaamini kwamba Urusi tayari imeanzisha mashambulizi hayo ili kutafuta mafanikio ya kujitapa itakapotimia mwaka mmoja tangu ilipoivamia Ukraine.