1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yashutumu mashambulizi ya Urusi

2 Machi 2022

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameshutumu hatua ya kuongezeka kwa mashambulizi ya Urusi kwenye miji yenye msongamano wa watu kama kampeni ya wazi ya ugaidi,

Ukraine | Gebäudebrand nach mutmasslichem Angriff auf Charkiw
Picha: Ukraine Emergency Ministry press service/AFP

Akizungumza baada ya shambulizi kufanyika kwenye uwanja mkuu wa mji wa Kharkiv na mnara wa Televisheni kwenye mji mkuu, Kiev Jumanne na kusababisha mauaji, Zelensky amesema hakuna mtu atakayesamehe wala atakayesahau. Ameliita shambulizi hilo kama ugaidi usiojificha na uhalifu wa kivita.

Zelensky ameishutumu Urusi kwa uvamizi huo akisema inataka kuwamaliza wananchi wa Ukraine, nchi yao na historia yao. ''Hawafahamu chochote kuhusu mji wetu mkuu wala historia yetu, lakini wana amri ya kuifuta historia yetu. Kuifuta nchi yetu. Kutumaliza sisi wote," alifafanua Zelensky.

Urusi yadai kuudhibiti mji wa Kherson

Huku hayo yakijiri wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa wanajeshi wake wameudhibiti mji wa Kherson ulioko kusini mwa Ukraine.

Msemaji wa wizara hiyo, Igor Koneshenkov amesema kuwa mgawanyiko wa vikosi vya Urusi vimechukua udhibiti kamili wa Kherson, ulioko kaskazini mwa Rasi ya Crimea, ambayo ilinyakuliwa na Urusi mwaka 2014. Huo utakuwa mji wa kwanza kuwa chini ya Urusi, tangu nchi hiyo ilipoanzisha uvamizi wake Ukraine.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky Picha: Ukraine Presidency press service/AFP

Ama kwa upande mwingine, Rais wa Marekani Joe Biden ameonya kuwa iwapo kiongozi wa Urusi haitokabiliwa vikali kutokana na uvamizi huo, basi uvamizi huo unaweza usiishie kwenye nchi moja.

Rais Biden ameitumia hotuba yake ya kwanza kuhusu hali ya taifa la Marekani kuangazia azimio la Jumuia ya Kujihami ya NATO ambayo imeipatia silaha jeshi la Ukraine na kupitisha vikwazo vikali ambavyo amesema vinamuacha Rais wa Urusi, Vladmir Putin akiwa ametengwa na ulimwengu zaidi kuliko ilivyowahi kutokea.

Biden: Tumejifunza kupitia historia

Biden amesema kupitia historia wamejifunza kwamba iwapo dikteta hatochukuliwa hatua kali kutokana na uchokozi wake, anaweza kusababisha machafuko zaidi, kwani ataendelea kusonga mbele na gharama ya vitisho kwa Marekani na ulimwengu wote vinaendelea kuongezeka.

Aidha, Biden amesema nchi yake inafuata nyayo za Canada na Umoja wa Ulaya kuzipiga marufuku ndege za Urusi katika anga yake kutokana na uvamizi huo. Ameongeza kusema kuwa wizara ya sheria ya Marekani itaanzisha kikosi maalumu cha kuwachunguza mabilionea wa Urusi ambao amewataja kuwa mafisadi waliojilimbikizia mabilioni ya dola katika utawala wa kidhalimu wa Urusi.

Rais wa Marekani, Joe BidenPicha: Jabin Botsford/Getty Images

Wakati huo huo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupiga kura leo kuamua iwapo italaani Urusi kuivamia Ukraine na kuitaka nchi hiyo iwaondoe wanajeshi wake mara moja.

Kura hiyo ya rasimu ya azimio haina mafungamano ingawa kama itapitishwa itakuwa kama karipio kali kwa urusi katika ngazi ya kimataifa na alama ya kutengwa kwake.

Azimio hilo linahitaji theluthi mbili ya kura ili kupita. Kura hiyo inafanyika baada ya nchi 100 kushiriki kwenye mkutano usio wa kawaida wa siku mbili ambao viongozi mbalimbali walivizungumzia vita vya Ukraine.

Ujerumani imejiandaa iwapo Urusi itaacha kusafirisha gesi

Katika hatua nyingine, Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Robert Habeck amesema leo kuwa Ujerumani imejiandaa iwapo Urusi itaacha kusafirisha gesi nchini humo.

Akijibu swali aliloulizwa na kituo cha redio cha Deutschlandfunk, serikali itafanya nini kama Urusi ikiacha kusafirisha gesi, Habeck amesema wamejitayarisha kwa msimu wa sasa ya baridi na joto.

Amefafanua kuwa katika msimu ujao wa baridi Ujerumani itachukua hatua zaidi, akizungumzia sheria mpya iliyopangwa ili kuhakikisha hifadhi ya gesi imejaa kwa ajili ya majira ya baridi.

(AP, AFP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW