Ukraine yatatizika kusafirisha jumla ya nafaka zake
8 Septemba 2022Siku ya Jumatano, Rais wa Urusi Vladimir Putin alizusha hofu ya kwamba nchi yake inaweza kujiondoa katika makubaliano ya usafirishaji wa nafaka baada ya kuituhumu Ukraine kutumia makubaliano hayo kusafirisha nafaka kuelekea Umoja wa Ulaya na Uturuki badala ya mataifa maskini ambayo yanahitaji zaidi chakula, hasa barani Afrika.
Licha ya makubaliano hayo kutekelezwa, mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na hatari ya kutuma meli katika Bahari Nyeusi iliyojaa mabomu ya kutegwa, ukosefu wa meli kubwa na kutengwa kwa bandari kuu, yanasababisha Ukraine kusafirisha kiwango kidogo cha nafaka na hivyo kutofikia malengo yake ya mauzo ya nje ya angalau tani milioni 6 ifikapo mwezi Oktoba.
Hali ya usalama bado ni tete
Alexander Saverys, Kiongozi Mtendaji wa shirikisho la wasafirishaji wa majini CMB lenye makao yake makuu nchini Ubelgiji amesema kwa sasa, hawapeleki meli zao kwenye bandari za Ukraine kwa sababu hawaamini kuwa ni salama, wanasema pia kuwa ni hatari kwa maisha ya mabaharia wao na kuwa kuna hatari ya kukwama bandarini.
Soma zaidi: Hatimaye Meli yenye nafaka yaelekea Lebanon
Makubaliano ya usafirishaji nafaka yaliwezeshwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki mnamo mwezi Julai. Kulingana na data za hivi karibuni kutoka kwa Kituo cha pamoja cha Uratibu (JCC) huko Istanbul, ambacho kinasimamia makubaliano hayo, tani za nafaka zipatazo milioni mbili - hasa mahindi - zimeuzwa nje ya nchi tangu meli ya kwanza kusafiri mnamo Agosti 1.
Malengo ya Ukraine hayajafikiwa
Kulingana na takwimu za Shirika la habari la Reuters, kwa kiwango cha sasa cha mauzo ya nje, itachukua karibu miezi sita ili kusafirisha nafaka zilizobaki kutoka mavuno ya mwaka jana kupitia bandari tatu za Ukraine zilizojumuishwa katika mkataba huo ambazo ni Odesa, Chornomorsk na Pivdennyi.
Kufikia wakati huo, shehena nyengine ya nafaka itakuwa imekusanywa kutoka mavuno ya sasa, ikiwa ni pamoja na tani milioni 20 za ngano na mahindi ambayo yanatarajiwa kufikia jumla ya tani milioni 30.
Soma zaidi:Meli iliyobeba nafaka yasubiri ukaguzi mjini Istanbul
Denys Marchuk, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo la Ukraine amesema wakulima hawana pesa za kuwekeza kwenye mashamba yao kwa kuwa hawawezi kuuza mazao yao, na hii ikimaanisha kuwa upandaji wa ngano katika majira ya baridi utakuwa pungufu karibu kwa theluthi moja ukilinganisha na mwaka jana.
Hali hiyo inaweza kuendeleza mzozo wa chakula duniani ambao mpango wa Umoja wa Mataifa ulilenga kupunguza. Bei ya vyakula duniani ilipanda mara baada ya Urusi kuivamia Ukraine Februari 24 mwaka huu.
Soma zaidi: Zelensky ashuhudia upakiaji wa nafaka Odesa
Mgogoro huo wa chakula ulionekana kupungua kufuatia makubaliano ya usafirishaji nafaka, lakini ngano ya Ukraine bado haijafikia kiwango chake cha kawaida cha usafirishaji hasa barani Afrika.
Meli nyingi zinazoondoka Ukraine ni ndogo mno.
Data ya shirika linalohusika na maswala ya baharini na bidhaa Shipfix, inaonyesha kuwa ukubwa wa wastani wa shehena zinazosafiri kutoka Ukraine ni zenye uwezo wa kubeba karibu tani 20,000 pekee.
Meli kubwa zinazobeba zaidi ya tani 60,000 za nafaka, zinazojulikana kama
Panamax, ambazo zingeshiriki mpango huo katika Bahari Nyeusi, zimepelekwa katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na Marekani na Amerika Kusini.
Mykolaiv yakabiliwa na mapambano
Mpango huu wa nafaka hauijumuishi Mykolaiv, ambayo ni bandari ya pili kwa ukubwa na usafirishaji nafaka nchini Ukraine, hii ni kulingana na data ya usafirishaji ya mwaka 2021.
Soma zaidi: Meli ya kwanza yenye nafaka za Ukraine yaondoka Odesa
Maghala ya nafaka huko Mykolaiv yalishambuliwa na makombora ya Urusi
mnamo Agosti 31 na hii ikidhihirisha hatari iliyopo. Baadhi ya mashirika ya bima yametoa huduma ya kuwezesha usafirishaji nafaka kutoka bandari ya Ukraine, lakini makampuni ya meli bado yana wasiwasi.
(RTRE)