1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Ukraine yatengeneza njia za muda za kusafirisha nafaka

19 Julai 2023

Ukraine imesema inajenga njia ya meli ya muda ili kuendelea kusafirisha nafaka baada ya Urusi kujiondoa kwenye makubaliano ya nafaka yaliyofikiwa kwa uratibu wa Umoja wa Mataifa kupitia ujia salama wa bahari Nyeusi.

Ukraine I Volodymyr Selenskyj
Picha: Sergei Supinsky/AFP

Katika barua iliyoandikwa Julai 18 na kuwasilishwa kwenye shirika la kimataifa la usafirishaji la ISO mapema hii leo, Ukraine imesema imeamua kujenga njia hiyo ya muda iliyopendekezwa inayopitia baharini.

Ukraine imesema kwenye barua hiyo kwamba njia nyingine itakayoijenga itapita kwenye maji ya eneo hilo na Ukanda maalumu wa kiuchumi wa Romania ambayo inapakana kwa karibu na Bahari Nyeusi

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema makubaliano hayo ya nafaka yanaweza kuendelea bila ya Urusi na Ukraine inaangazia machaguo ya kuendeleza wajibu wake wa kusambaza chakula. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kyiv, Zelenskiy ametoa mwito kwa Umoja wa Mataifa na Uturuki kuchukua hatua muhimu za kuendeleza mpango huo na kuongeza kuwa Ukraine haitaogopa kusafisirisha nafaka bila ya Urusi.

"Tunawataka washirika wetu, Umoja wa Mataifa na Uturuki wasiogope kufanya kila linalowezekana ili hata bila Urusi tuweze kuutumia ukanda wa Bahari Nyeusi. Hatuogopi. Makampuni ya meli yalitufuata na kusema kwamba wako tayari kuendelea kupeleka nafaka ikiwa Ukraine itaruhusu meli kuondoka bandarini na Uturuki kuziruhusu kupita Ujia wa Bosporus."

Urusi, jana usiku iliishambulia bandari ya Bahari Nyeusi ya Odesa ikiwa ni mara ya pili mfululizo baada ya kujiondoa kwenye makubaliano hayo ya nafaka siku ya Jumatatu. Kyiv imesema mapema leo kwamba Urusi imeharibu karibu tani 60,000 za nafaka zilizokuwa zinasubiri kusafirishwa katika shambulizi hilo la jana usiku.

Soma Zaidi: Mashambulizi yaliyoilenga bandari ya Odessa yalaaniwa

Ukraine imeahidi kuendelea kusafirisha nafaka licha ya Urusi kujitoa kwenye makubaliano ya kusafirisha nafaka kupitia Bahari Nyeusi.Picha: Gleb Garanich/REUTERS

Mataifa matano ya Ulaya yanuaia kuendeleza marufuku ya nafaka kutoka Ukraine.

Huku hayo yakiendelea, mataifa matano ya Ulaya yamesema yananuia kuongeza muda wa marufuku ya nafaka kutoka Ukraine ili kulinda maslahi ya wakulima wao. Mawaziri wa kilimo wamesema mataifa hayo wamesaini azimio la pamoja mjini Warsaw, Poland kabla ya majadiliano ya Umoja wa Ulaya kuhusiana na suala hilo yaliyopangwa kufanyika wiki ijayo mjini Brussels.

Azimio hilo lililosainiwa na Poland, Slovakia, Hungary, Bulgaria na Romania linasema, wataendelea kuruhusu nafaka za Ukraine kupitishwa kwenye barabara zao, reli ama mito ili kufika kwenye maeneo yenye uhitaji kote ulimwenguni na hasa baada ya Urusi kujitoa kwenye makubaliano ya nafaka ingawa wamesisitiza wataendeleza marufuku hiyo kwa mwaka huu mzima.   

Katika hatua nyingine Ikulu ya Kremlin imeyashutumu mataifa ya magharibi kwa kufumbia macho kile ilichotaja kuwa mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na Ukraine ndani ya Urusi, ikiangazia ukimya wa mataifa hayo dhidi ya mashambulizi ya droni zinazorushwa chini ya maji yaliyofanywa na Ukraine kwenye daraja la Crimea.

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari hii leo kwamba Moscow kwa mara kadhaa imeshuhudia namna mataifa ya magharibi yanavyoshindwa kuikemea Ukraine kwa ugaidi.

Aidha Peskov amezungumzia tukio la moto katika kambi ya kijeshi iliyoko Crimea, uliosababisha maelfu ya wakaazi kuondolewa. Amesema tayari rais Vladimir Putin amearifiwa juu ya tukio hilo linalotokea siku mbili baada ya shambulizi la Ukraine kwenye daraja la Kerch ambalo ni muhimu kwa kupitisha vifaa vya kijeshi kutoka Urusi hadi Ukraine. Bado mamlaka hazijaelezea chanzo cha moto huo, lakini baadhi ya vyombo vya habari vya Urusi vimearifu kwamba kulisikika milipuko katika eneo hilo na picha zilizoonesha moshi mzito uliotanda angani.

Soma Zaidi: Shambulizi la Ukraine laharibu daraja la Crimea: Urusi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW