Ukraine yatoa wito kwa NATO kuandaa vikwazo dhidi ya Urusi
1 Desemba 2021Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba ametoa wito wa kuwepo kwa mtazamo wa pande tatu unaohusisha mazungumzo wazi na Urusi, kuweka vikwazo na kuongeza msaada wa kijeshi kwa Ukraine. Wakati wa mazungumzo na mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa wanachama wa NATO mjini Riga nchini Latvia, Kuleba amesema kwamba wana imani iwapo wataungana na kuchukuwa hatua kwa njia iliyoratibiwa, wataweza kumzuia rais wa Urusi Vladmir Putin kuchagua njia mbaya zaidi ambayo ni operesheni ya kijeshi.
Baada ya mazungumzo hayo na mataifa washiriki wa Jumuiya hiyo ya NATO hapo jana, katibu mkuu wa Jumuiya hiyo Jens Stoltenberg, alionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya Urusi iwapo itafanya mashambulizi dhidi ya Ukraine na kuongeza kuwa mataifa wanachama yanaweza kuiwekea vikwazo Urusi. Stoltenberg ameongeza kusema kuwa hali ndani na Ukraine bado haitabiriki na kwamba hakuna uhakika juu ya nia ya Urusi
Ukraine, ambayo imeshuhudia msukumo wake wa kujiunga na muungano huo unaoongozwa na Marekani ukikwama, imekuwa ikipokea msaada wa kijeshi kutoka kwa washirika wa NATO. Taifa hilo lililokuwa jamhuri ya kisovieti ambayo sasa inataka kujiunga na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya NATO, limekuwa kiini cha mvutano kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi huku uhusiano kati ya mataifa hayo ukidorora katika kiwango kibaya zaidi katika muda wa miongo mitatu tangu kumalizika kwa vita baridi.
Hapo jana, rais Vladimir Putin alisema kuwa luteka za kijeshi na hatua nyingine za mataifa ya Magharibi pamoja na Ukraine zinatishia usalama wa nchi yake na kuonya dhidi ya alichokiita 'uchokozi'. Wakati huohuo, Urusi leo imesema kuwa imeanza mazoezi ya kijeshi ya kawaida ya msimu wa baridi katika eneo lake la kijeshi Kusini mwa nchi hiyo ambalo baadhi ya sehemu zinapakana na Ukraine na kwamba wanajeshi elfu 10 wanashiriki katika mafunzo hayo.