1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yavunjwa moyo na Uswisi kuhusu mpango wa amani

Josephat Charo
1 Oktoba 2024

Ukraine imesema imevunjwa moyo na uamuzi wa Uswisi kuunga mkono mpango wa amani uliopendekezwa na China na Brazili ambao unalenga kuvifikisha mwisho vita na Urusi.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: The Yomiuri Shimbun/AP/picture alliance

Ukraine imeelezea kuvunjwa moyo na hatua ya Uswisi kuunga mkono mpango wa amani uliowasilishwa na China na Brazil unaolenga kuvimaliza vita vyake na Urusi vilivyodumu kwa zaidi ya miaka miwili na nusu.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Ukraine imesema wanapata shida kuelewa mantiki ya uamuzi huo, ikidokeza kwamba Ukraine ilikuwa imeandaa mkutano wa kimataifa nchini Uswisi mwezi Juni ambapo masharti yake yaliwekwa wazi bayana.

Taarifa hiyo imesema mipango yoyote ya amani inayoshindwa kuhakikisha urejesho kamili wa mipaka ya Ukraine haikubaliki na kwamba mipango ya namna hii inaweka mazingira kana kwamba mdahalo unafanyika huku Urusi ikiendelea na vitendo vyake vya kihalifu.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Uswisi ilishiriki mkutano kati ya Brazil na China kandoni mwa mkutano wa Hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York wiki iliyopita ambapo mpango wa vipengele sita ulipendekezwa.

Marekani na washirika wake wa Ulaya wameukataa mpango huo kwa kukosa kurejelea mkataba wa Umoja wa Mataifa na kutokiukwa kwa mipaka ya himaya ya Ukraine.